DK MWAKYEMBE AVAMIA STENDI KUU YA MABASI YA MIKOANI UBUNGO...

Waziri wa Uchukuzi, Dk Harison Mwakyembe, jana alibukia katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo (UBT) na kufanya ukaguzi wa ghafla wa nauli za abiria wa kwenda mikoa mbalimbali na kusimamia waliozidishiwa nauli hizo kurejeshewa.
Dk Mwakyembe aliyefika kituoni hapo saa 11.30 alfajiri na kuingia katika mabasi moja baada ya lingine kukagua tiketi kwa abiria, pia alisimamia kutozwa faini kwa baadhi ya mabasi kuanzia Sh 250,000 hadi 750,000 kulingana na idadi ya makosa waliyokutwa nayo.
Pia aliwaagiza watendaji wakuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA), kufanya kazi ya ukaguzi kituoni hapo kwa miezi mitatu mfulululizo ili kuondoa matatizo yaliyopo.
"Nawataka sasa wote muache kukaa ofisini na mtoke nje kufanya ukaguzi, muda huu nilipaswa kuwa bungeni mjini Dodoma lakini kazi mliyopaswa kuifanya mimi nawajibika kuifanya, kuanzia sasa nataka kuona kila mtu anafanya kazi yake kikamilifu," alisema Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe alinza ukaguzi huo kimyakimya katika basi la Green Star na kisha kuendelea katika basi la Musoma Express, huku akifuatana na Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima na watendaji wake pamoja na maofisa wa Polisi.
Katika ukaguzi huo aliofanya zaidi katika mabasi yanayokwenda mikoa ya Mwanza, Mbeya, Musoma pamoja na Arusha, Mwakyembe alibaini uwepo wa udanganyifu katika nauli ambapo abiria walikuwa wakitozwa kiasi kikubwa cha nauli tofauti na viwango vilivyowekwa na Serikali.
Mabasi yaliyofanyiwa ukaguzi na kukutwa yakitoza nauli hizo ni pamoja na ya kampuni za Summry, Najimunisa, Musoma Express, ‘RS Bus’, Princess Shabaha, Buffalo pamoja Best Line .
Mwakyembe aliyekuwa amesimama katika mlango wa kutokea mabasi kituoni hapo, aliagiza kusimamishwa kwa kila basi lililokuwa likitoka na kupanda ndani yake na kuwahoji abiria nauli waliyotozwa kwa kila sehemu wanayokwenda, huku akitaka uthibitisho kwa maofisa wa Sumatra alioambatana nao.
"Tunashukuru Waziri kwa kuja kujionea hali halisi, ukweli sisi abiria tunanyanyasika, wamiliki wengi wa mabasi haya wanapandisha nauli bila kufuata utarataibu, ujio wako tunaamini utasaidia kuondoa tatizo hili," alisikika abiria mmoja aliyekuwa amepanda ndani ya basi la RS, lililokuwa likienda Bukoba huku akiungwa mkono na abiria wenzake.
Katika ukaguzi huo, Dk Mwakyembe alibaini kuwepo kwa abiria waliotozwa Sh 60,000 kwa safari ya kwenda Bukoba tofauti na nauli halali ya Sh 51,000 kwa safari hiyo katika basi ya hadhi ya Semi Luxury.
Wapo pia abiria wa kwenda Mwanza waliokutwa wametozwa nauli hadi Sh 45,000 kwa safari hiyo tofauti na Sh 35,000 iliyowekwa na Sumatra.
Kwa abiria wa Singida, walikutwa abiria waliotozwa nauli ya Sh 28,000 hadi Sh 38,000 wakati nauli halali ya Sumatra ni Sh 21,000.
Ukiacha masuala ya nauli pia, Dk Mwakyembe alisimamia utozaji wa faini kwa mabasi yaliyobainika kuwa na dereva mmoja na kusema mabasi hayo yamekuwa chanzo cha ajali nyingi zinazosababishwa na uzembe wa madereva.
"Ajali nyingi zinazoendelea kutokea hapa nchini kwetu kwa asilimia 75 zinasababishwa na uzembe wa madereva, hatutaki kuona maisha ya Watanzania yakiendelea kupotea kwa uzembe huu,"alisema Dk Mwakyembe ambaye jana mchana alitarajia kukutana na viongozi wa Sumatra, pamoja na wadau mbalimbali wa sekta hiyo kwa ajili ya mazungumzo.
Kaimu Mkurugenzi wa Sumatra, Ahmad Kilima, alisema kwa sasa wanajipanga kufanya kazi hiyo kwa nguvu zote ili kuwabaini wamiliki wa mabasi hao wanaoendelea kuvunja utaratibu wa usafirishaji kwa makusudi.
Alisema ufinyu wa wafanyakazi wa ofisi hiyo kwa kiwango kikubwa ndiyo uliosababisha kufanyika kwa ukaguzi wa kusuasua, hivyo wanajipanga kuongeza wafanyakazi ili kuhimarisha shughuli za ukaguzi.
Hatua ya Dk Mwakyembe kutembelea kituo hicho ni muendelezo wa utaratibu aliojiwekea tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo ambapo hadi sasa tayari ametembelea kufanya ukaguzi wa ghafla katika Mamlaka ya Reli Tanzania na Zambia (Tazara), Shirika la Reli (TRL) pamoja na Kampuni ya Ndege ya ATCL.

No comments: