WAHITIMU 700 WA UDAKTARI KUPUNGUZA MAKALI YA MGOMO MWEZI UJAO...

Wakati madaktari walio mafunzoni kwa vitendo wakiingia katika mgomo usio halali, wanafunzi 700 wa vyuo mbalimbali vinavyotoa Shahada ya Kwanza ya Udaktari, wanatarajiwa kumaliza masomo yao mapema mwezi ujao na kwenda katika mafunzo kwa vitendo katika hospitali mbalimbali nchini.
Madaktari hao 700 watarajiwa kutoka katika vyuo kama Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba Muhimbili (MUHAS), Herbert Kairuki, Chuo Kikuu cha Afya na Tiba (IMTU), Chuo Kikuu cha Bugando, kwa kutaja vichache.
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussein Ali Mwinyi alilithibitisha kwamba ni kweli madaktari hao watarajiwa 700, wanakamilisha masomo yao mapema mwezi ujao na wataingia katika mafunzo kwa vitendo kwa mwaka mmoja.
"Ni kweli tunatarajiwa kuwa wanafunzi hao 700 wanasomea udaktari kumaliza masomo yao mapema mwezi ujao katika vyuo mbalimbali nchini. Wapo wanaomaliza kutoka Muhas, IMTU, Bugando, Kairuki," alisema Dk Mwinyi juzi.
Dk Mwinyi alisema kwa mujibu wa taratibu, madaktari hao watarajiwa watapangiwa katika hospitali mbalimbali nchini zikiwamo za Serikali na zile za binafsi.
"Zamani walikuwa wanakwenda katika hospitali za Serikali pekee, lakini kwa sasa utaratibu ni katika hospitali zote, za binafsi kama Aga Khan na zile za Manispaa," alieleza Dk Mwinyi.
Hatua hiyo ya kumaliza masomo na kujiandaa kuanza mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi hao wanaotarajiwa kuwa madaktari, inakuja wakati wenzao wapatao 357 wakiwa wamepelekwa katika Baraza la Madaktari Tanzania kutokana na kushiriki mgomo usio halali.
Kwa mujibu wa Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachriss Mwamaja, madaktari hao wameripoti wizarani mwishoni mwa wiki tayari kujua utaratibu unaofuata baada ya mgomo, suala linaloelezwa kuwa kinyume cha misingi ya taaluma hiyo.
Msemaji huyo alisema baada ya kuripoti wizarani, watapewa barua kwenda kwa Baraza la Madaktari Tanzania ambako huko watajieleza kutokana na kushiriki mgomo huo ambao ulianza Juni 23, mwaka huu, ukiwashirikisha madaktari hao walio mafunzoni ambao, kimsingi hawalipwi mshahara, bali posho.
"Hadi leo (Ijumaa iliyopita) kuna idadi kubwa ya madaktari walioripoti hapa, hatua hiyo inatoa nafasi nyingine kwao kwenda kujieleza mbele ya Baraza la Madaktari, kutokana na hatua yao ya kushiriki mgomo huo," alisema Mwamaja. Alisema baada ya Baraza kumaliza kupokea maelezo ya madaktari hao, litapeleka ripoti yake wizarani na kumkabidhi Waziri mwenye dhamana kwa ajili ya hatua zingine.
Kwa upande wake, Dk Mwinyi alisema Baraza la Madaktari Tanzania ni chombo cha kisheria, hivyo wanapelekwa huko kwa kuzingatia maadili ya kazi zao.
"Huko wanapelekwa kwa sababu Baraza liko kisheria na watajibu hoja na baraza litaamua hatua za kuchukua kwa mujibu wa sheria za kuanzishwa kwake," alieleza Dk Mwinyi.
Moja ya hoja za madaktari hao waliogoma ni kutaka kulipwa mshahara zaidi na Serikali na katika mapendekezo yao ni kulipwa Sh milioni 3.5 kwa mwezi kwa daktari anayeanza kazi; kiwango ambacho ukijumuisha na madai mengine ya posho kinafikia Sh milioni 7.7.
Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake ya mwisho ya mwezi Juni, aliwaeleza madaktari hao kwamba Serikali haina uwezo wa kulipa kiwango hicho, na kwamba wako huru kutafuta mwajiri mwingine anayeweza kuwalipa, na hivyo hawana sababu ya kugoma.

No comments: