AJALI YA MELI YAUA WANAFUNZI 14 WA CHUO CHA WAISLAMU MOROGORO...

Chuo Kikuu cha Waislamu cha Morogoro (MUM) kimepoteza wanafunzi wake 14 waliokufa kutokana na ajali ya meli ya mv Skagit iliyotokea Julai 18, mwaka huu.
Wanafunzi hao waliopoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyotokea karibu na Kisiwa cha Chumbe ikitokea Dar es Salaam kwenda Visiwani Zanzibar, walikuwa wanasomea Shahada ya Ualimu mwaka wa kwanza katika chuo hicho.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Uongozi wa chuo hicho kupitia kwa Ofisa Habari wake, Saddy Ally, inaonesha kuwa miili miwili ya wanafunzi hao ndiyo iliyopatikana na 12 haikupatikana hadi sasa.
Ofisa Habari wa Chuo Kikuu hicho aliwataja wanafunzi waliokufa na wanakotoka katika mabano kuwa ni Abdalla Soud Mohammed (Mwanakwerekwe-Unguja), Suleiman Habib Ally ( Chakechake- Pemba) na Othman Ali Mwinyihusein( Muyuni – Unguja).
Wengine ni Rashid Fadhil Saleh (Magomeni – Unguja), Rashid Mohammed Juma ( Chake Chake – Pemba), Hassan Faki Seif ( Fuoni- Unguja ), Mangi Haji Haji (Mwanakwerekwe – Unguja), Asha Juma Abdalla (Wete – Pemba), Said Simai Iddi ( Umbuji – Unguja) na Khadija Abdallah Khamis (Wete Pemba).
Wengine waliokufa ni Mgeni Mwinyi Omari (Mpendae – Unguja), Patima Makame Simai ( Fuoni – Unguja), Said Salim Khatib ( Wete –Pemba) na Khamis Ali Suleiman wa Bububu – Unguja.
Baada ya ajali hiyo ya meli, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeendelea kufuatilia ubora wa vyombo vya usafiri majini na sasa imefuta usajili wa moja kwa moja kwa boti ya Seagul, Kalama na Sepider zinazotoa huduma zake katika bandari za Unguja na Pemba pamoja na Dar es Salaam baada ya kubainika kwamba vimechakaa na havina sifa kubeba abiria.
Aidha mamlaka ya usafiri wa baharini imeizuia meli ya Kilimanjaro 3 kutoa huduma zake kwa muda kutokana na vifaa vyake vya uokozi vilivyopo pembeni mwa meli kuchakaa na muda wake kumalizika, ikiwemo boti za dharura za uokozi ndogo ndogo.
Akitangaza uamuzi huo mbele ya waandishi wa habari huko Malindi, Naibu Mkurugenzi wa mamlaka ya usafiri wa baharini, Abdalla Kombo alisema boti hizo zimekuwa zikikabiliwa na matatizo ya kuharibika mara kwa mara ikiwemo kuzimika baharini na kusababisha matatizo makubwa.
"Napenda kuwajulisha waandishi wa habari kwamba mamlaka ya usafiri baharini imevifutia leseni ya kutoa huduma za usafiri vyombo vitatu vya usafiri baada ya kubainika kwamba vimechakaa sana na vinahatarisha usalama wa abiria," alisema Kombo.
Kombo aliwataka wamiliki wa vyombo hivyo kuviondoa katika ardhi ya bahari ya Zanzibar vyombo hivyo. Wahusika wameshajulishwa uamuzi huo.
"Tumewataka wamiliki wa meli hiyo kufanya marekebisho makubwa kutafuta vifaa vingine vya kutoa huduma za dharura za uokozi...wakipata vifaa vingine leo basi wataruhusiwa kufanya kazi," alisema.
Pia mamlaka hiyo imeutaka uongozi wa meli ya Serengeti inayotoa huduma zake katika kisiwa cha Pemba kuhakikisha kwamba inachukua idadi kamili ya abiria ambayo ni 350 na sio 800 pamoja na tani za mizigo 50 na si 100.
Kombo aliwaondolea wasiwasi juu ya huduma kwa kusema meli mpya ya kisasa inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu Said Bakhresa wa kampuni ya Azam inatazamiwa kuwasili hivi karibuni na kuanza kutoa huduma zake katika mwambao wa pwani ya Tanzania.
Mabalozi wanazoziwakilisha nchi zao nchini wakiwemo wa nchi za Kiarabu wametoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein wakiahidi kutoa misaada mbali mbali pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kukabiliana na matukio kama hayo ya ajali.
Mabalozi hao waliowakilishwa na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo nchini ambaye ni kiongozi wa mabalozi waliopo Tanzania, walifika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kutoa pole. Balozi wa Umoja wa Nchi za Falme za Kiarabu (UAE), Mallalla Mubarak Suwed EL-Amri pia alifika Ikulu kwa ajili ya kutoa pole na kuahidi kusaidia katika sekta ya usafiri baharini.

No comments: