Idara ya Usalama wa Taifa imesema taarifa ambazo zimekuwa zikiihusisha na matukio mbalimbali likiwamo la kutekwa kwa Dk Stephen Ulimboka ni za uzushi na uongo, zenye lengo la kuharibu jina na sifa ya idara hiyo.
Imesema taarifa hizo zimekuwa zikiunganisha vipande vya taarifa mbalimbali ili kukidhi malengo yaliyokusudiwa na kwamba wahusika wamekuwa wakilitumia gazeti moja linalodai kuandika habari za uchunguzi na kuihusisha idara hiyo.
"Taarifa hizo zimekuwa zikitolewa kwenye vyombo vya habari zikiihusisha Idara hii na matukio ambayo yanaidhalilisha na kuzua maswali mengi kwa wananchi.
"Kati ya tuhuma hizo ni tukio la kutekwa kwa Dk Ulimboka, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari na madai ya kufanywa kwa mipango ya kudhuru baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani," ilisema taarifa hiyo jana.
Kwa mujibu wa taarifa, gazeti la kila wiki limekuwa likirudia tuhuma hizo mara kwa mara kwa madai kwamba ni habari za uchunguzi na kuihusisha Idara.
Ilifafanua kuwa haikuhusika wala haihusiki na matukio yoyote yaliyotajwa katika tuhuma hizo. "Hivyo tunaomba wananchi wazipuuze taarifa hizo," ilisema.
Taarifa hiyo, ilisema matukio yaliyotajwa katika tuhuma hizo yanachunguzwa na Jeshi la Polisi, ambacho ndicho chombo chenye dhamana, na kwa maslahi ya Taifa, si vizuri kuachia upotoshaji huo uendelee.
Iliendelea kusisitiza: "Tunapenda kuwahakikishia Watanzania kuwa uzushi na tuhuma zinazotolewa dhidi ya Idara hazitatuvunja moyo, bali zitatuunganisha na hivyo kutuimarisha katika azma yetu ya kuhakikisha nchi inaendelea kubaki salama kwa kushirikiana na wananchi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama".
Dk Ulimboka alitekwa na kushambuliwa na watu wasiofahamika ambao baada ya kumpiga na kumjeruhi walimtelekeza katika msitu wa Mabwepande wilayani Kinondoni. Kutekwa kwake kuliibua mjadala ukiihusisha Idara ya Usalama wa Taifa kwa kile ambacho kimekuwa kikidaiwa kuwa ni kumnyamazisha kuhusu mgomo wa madaktari.
Katika mazingira hayo, imekuwa ikidaiwa kuwa mmoja wa watu waliokuwa wakifanya mazungumzo naye kabla ya kutekwa ni Ofisa wa Usalama wa Taifa ambaye hata hivyo hadi sasa hakuna taarifa kutoka kwa Ulimboka wala madaktari wenzake ambao wamewahi kutaja jina la mtu huyo.
No comments:
Post a Comment