Watanzania wametakiwa kuunga mkono kwa kuendeleza
juhudi za waasisi wa makuzi ya lugha ya Kiswahili.
Hayo
yalisemwa juzi na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Eckenforde cha Jijini Tanga,
Profesa Joshua Madumulla wakati wa uzinduzi wa Chama cha Lugha na Fasili ya
Kiswahili Tanzania (Chalufakita) uliofanyika katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu
John mjini hapa.
Profesa
Madumulla alisema kuna kila sababu za kuunga mkono kwa kuendeleza juhudi za
waasisi wa makuzi ya lugha ya Kiswahili, wakiwamo Shaaban Robert, Shekhe Amri
Abeid Kaluta, Mathias Mnyampala, Saadan Kandoro, Muhammed Said Abdulla,
Akilimali Snowwhite na wengine.
Pia,
alitaka kutambuliwa na kuheshimiwa kwa lugha na fasili ya Kiswahili ikiwa ni
pamoja na kuenzi kazi zilizofanywa na waasisi wa makuzi ya lugha hiyo na kuyaheshimu
makazi yao ya muda mfupi na mrefu.
“Bado hatujawaheshimu vya kutosha tukiwalinganisha na wenzao wa ng’ambo,” alisema Profesa Madumulla.
Alisema
jambo la msingi ni kutaka kutambulisha nguvu na uwezo wa Kiswahili katika
vipengele mbalimbali vya kijamii huku kipengele cha elimu na taaluma kikiwa
mstari wa mbele katika kutiliwa mkazo.
“Hakuna somo katika dunia hii lisilotumia lugha katika kufunzwa
kwake iwe lugha ya sauti ama ya ishara kwa sasa tumekuza mno ugumu wa masomo
hayo kiasi kwamba tunatanua bila kujitambua ugumu wa masomo,” alisema Profesa Madumulla.
No comments:
Post a Comment