Kituo
cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimesema kinajipanga kutumia wanasheria,
kujadili na kufanyia kazi baadhi ya vifungu vyenye utata vilivyopo katika
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Mkurugenzi
wa Utetezi, Maboresho na Sheria wa LHRC,
Harold Sungusia alisema hayo jana Dar es Salaam.
Alisema
vifungu hivyo ni pamoja na Kifungu cha
25 (2) cha Mamlaka ya Bunge la Katiba na Kifungu cha 22 cha Sheria hiyo.
Kuhusu
utata wa Kifungu cha 25 (2), alisema kifungu hicho kimekuwa na utata kuhusu
Mamlaka ya Bunge la Katiba katika kujadili na kufuta baadhi ya vipengele katika
rasimu ya Katiba.
“Kifungu
hicho kinakuwa na utata kwani hakiko wazi kama Bunge hilo lina mamlaka ya
kujadili na kufuta ama kujadili na kupitisha kile kilichofanywa na iliyokuwa
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,” alisema Sungusia.
Kuhusu
Kifungu cha 22, alisema kinatoa mamlaka kwa Rais kuitisha Bunge Maalumu la
Katiba, lakini hakielezi wazi kama ana mamlaka ya kulifuta linapokwenda kinyume
na matarajio.
Alisema
inavyoeleweka ni kwamba kama sheria inaweza kumpa kiongozi mamlaka ya kufanya
jambo, halafu ikawa kimya kuhusu kufuta jambo hilo. Alisema ni lazima upo
utata, unaohitaji kufanyiwa kazi.
“Katika sheria hiyo hakuna kifungu kinachosema
kama Rais hana mamlaka ya kulifuta Bunge hilo…sheria hiyo imekaa kimtegomtego,
na kifungu chenye kueleza nani mwenye jukumu hilo kilitakiwa kuwepo humo,”
alisema Sungusia.
Alisema
katika sheria hiyo, hakuna kifungu kinachomkataza Rais kufanya hivyo na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali alipaswa kuona hilo na kuandaa muswada wa kupelekwa bungeni kukiweka.
Akizungumzia
sheria hiyo na mamlaka ya kufuta Bunge Maalumu la Katiba, juzi Mwanasheria Mkuu
wa Serikali, Frederick Werema alisisitiza kuwa sheria hairuhusu mtu yeyote,
akiwemo Rais, kuvunja Bunge Maalumu la Katiba.
No comments:
Post a Comment