Maandamano
ya walemavu wa ngozi kwenda Kituo cha Polisi Buguruni jijini Dar es Salaam
jana, yalisambaratishwa kwa mabomu ya machozi na askari Polisi, baada ya
waandamanaji hao kuzingira kituo hicho na kukaidi amri ya kutawanyika.
Waandamanaji
hao walitokea Mahakama ya Mwanzo Buguruni kwenda katika kituo hicho,
kulalamikia uamuzi wa Mahakama hiyo kutoa dhamana kwa mshitakiwa, Ombeni Swai,
mkazi wa Tabata Matumbi, anayedaiwa kutishia kumuua mwenzao.
Kabla
ya maandamano hayo, Swai alifikishwa mahakamani hapo, mbele ya Hakimu Mfawidhi,
Benjamini Mwakasona na kushitakiwa kwa kosa la kutishia kumuua mlemavu wa
ngozi, Mwinyisi Issa.
Karani
wa mahakama hiyo, Edwin Mwandawanda alidai mahakamani hapo kwamba Swai
alitishia kwa maneno kumuua Issa Agosti 16 mwaka huu, saa 7 mchana katika eneo
la Buguruni Wilaya ya Ilala.
Hata
hivyo, mshitakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo Hakimu Mwakasona
aliahirisha kesi hiyo mpaka Septemba 3, mwaka huu na kumwambia mshitakiwa kuwa
dhamana ya kesi yake ipo wazi, ambapo alitakiwa kuwa wadhamini wawili waliotakiwa
wote kuwa na barua zinazotambulika na serikali za mtaa.
Pamoja
na dhamana hiyo kuwa wazi, mshitakiwa hakufanikiwa kutimiza masharti hayo kwa
wakati, hivyo akaendelea kushikiliwa wakati akisubiri wadhamini wake kutekeleza
masharti hayo.
Kitendo
hicho cha mahakama kutangaza dhamana kwa mshitakiwa, kiliamsha hasira kwa
walemavu wa ngozi waliokuwa wamekusanyika nje ya mahakama kufuatilia mwenendo
wa kesi hiyo, iliyotajwa kwa mara ya kwanza.
Baadhi
ya walemavu hao walifanikiwa kupenya mpaka alipokuwepo mshitakiwa na kuanza
kumpiga.
Kitendo
hicho kilifanya Polisi kumpakia haraka kwenye gari na kumpeleka kituoni
Buguruni, kwa nia ya kumnusuru.
Hatua
hiyo haikuwaridhisha albino hao, ambao walijikusanya na kuandamana kwenda
katika Kituo cha Polisi Buguruni, kwa lengo la kutaka kumdhuru mshitakiwa.
Mashuhuda
waliozungumza na gazeti hili, walidai kuwa waandamanaji hao walipotakiwa
kutawanyika, walikaidi, hatua
iliyosababisha Polisi kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya.
Walisema baadhi ya albino walidiriki kupanda ndani ya
gari la polisi aina ya Land Rover
'Defender' na kuanza kumshambulia kwa mateke na ngumi mshitakiwa, jambo
lililowalazimu polisi kuondoka eneo hilo hadi kituo cha polisi Buguruni.
Albino
hao pia walifuata kwa nyuma huku wengine walipanda ndani ya gari hilo hadi
mahali hapo.
Wananchi
waliokuwepo nje ya kituo cha polisi, walikumbwa kwa taharuki. Albino hao
waliendelea kumshambulia mshitakiwa huyo hadi walipofika nje ya kituo hicho,
huku wakizuiliwa na polisi hao, ambao baadae walilazimika kufyatua mabomu ya
machozi kwa lengo la kuwatawanya.
Mwandishi
alimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marry Nzuki, ambaye alikiri kutokea
kwa vurugu hizo. Alisisitiza kuwa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa Polisi kwa
kosa hilo.
"Baada
ya kutawanywa pale kituo cha Buguruni, Mkuu wa Kituo aliwaambia waje katika
ofisi zangu, lakini hadi hivi sasa sijamuona mtu yeyote wala kiongozi wao
kuleta mashitaka yoyote," alisema Kamanda Nzuki.
Wakati
vurugu hizo zikitokea, Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi,
ametangaza kutoa Sh milioni 10 kwa mtu atakayefanikisha kukamatwa kwa watu
walioshiriki kumkata mkono mlemavu wa ngozi, Susan Mungi (35) na kumuua mumewe
wilayani Igunga, Tabora.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Mengi alisema pia IPP itasomesha watoto wa mlemavu huyo.
Katika
mkutano huo uliohudhuriwa pia na baadhi ya viongozi wa Chama cha Albino
Tanzania (TAS), Mengi alisema anafanya hivyo kama mwananchi wa kawaida ambaye
ameguswa na vitendo hivyo vya kinyama, vinavyofanywa dhidi ya watu hao wenye
ulemavu.
Aliomba
Polisi kuwasaka wote waliohusika, kuwakamata na kuwapeleka mahakamani haraka.
Alisema
albino ni watu kama wengine hivyo vitendo vyovyote vya kinyama dhidi yao lazima
vilaaniwe na watu wote.
"Hakuna
albino ambaye amependa awe hivyo, hakuna aliyemwomba Mungu ampatie ulemavu huo,
hawa ni binadamu kama sisi, jamii na serikali kuendelea kukaa kimya juu ya
unyama huu ni jambo linalosikitisha," alisema Mengi. Mengi alisema
waliotumwa kumkata albino huyo wakamatwe.
Susan,
mkazi wa Kijiji cha Buhelele kati ya Nsimbo wilayani Igunga, alikatwa kiwiko
cha mkono wake na wahusika kutoweka nacho.
Katika
tukio hilo, mumewe Mapambo Mashili aliuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kifuani na kichwani wakati akijaribu
kumnusuru mkewe asikatwe mkono wake.
Mtoto
huyo hadi sasa amelazwa katika Hospitali
ya Wilaya ya Urambo. Katika tukio hilo,
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwasa
ametangaza dau la Sh 500, 000 kwa mwananchi atakayesaidia kukamatwa kwa watu
wanaofanya vitendo hivyo.
Tukio
hilo limekuwepo ikiwa ni wiki baada ya mtoto, Upendo Sengerema (15) mkazi wa
Kijiji cha Usinge kata ya Uganza wilayani Kaliua mkoani Tabora, kukatwa mkono
na watu waliokimbia nao.
Katibu
Mkuu Chama cha Albino (TAS), Ziada Nsemo alisema kati ya watanzania milioni 45,
Mengi ni mmoja wa watu waliojitokeza hadharani kukemea vitendo vya kinyama
wanavyofanyiwa. Alisema licha ya polisi kuahidi kuwalinda, wameendelea kuuawa.
Alitoa
mwito kwa albino nchini, kujilinda na kukaa karibu na makundi ya watu ili
wanapovamiwa iwe rahisi kupata msaada kwa sababu ulinzi kwao ni wa shaka na
wanawindwa kila kona.
No comments:
Post a Comment