Mmea
wa asili unaostawi kwa wingi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Kitulo, maarufu kwa
jina la Chikanda, upo hatarini kutoweka kutokana na kuvunwa kiharamu na watu
wanaoamini unasaidia kupunguza makali ya Ukimwi.
Zao
litokanalo na mmea huo linafanana na kiazi mviringo , linadaiwa kuwa na soko
kubwa katika nchi za Zambia na Malawi. Tofauti na viazi vya kawaida, katika
shina lake Chikanda huzaa kiazi kimoja pekee.
Kaimu
Mhifadhi Mkuu wa hifadhi hiyo iliyopo Matamba wilayani Makete, mkoani Iringa,
Pius Mzimbe, alisema uchunguzi waliofanya katika nchi hizo unaonesha viazi
hivyo vya Chikanda hutengeneza dawa kwa matumizi ya binadamu na pia kwa ajili
ya chakula.
Akizungumza
na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo hivi karibuni, alisema wavunaji haramu
huingia kinyemela katika hifadhi hiyo yenye milima mingi na kuvuna mimea hiyo
na huuza kwa Sh 80,000 hadi Sh 100,000 kwa debe katika nchi hizo.
Kwa
mujibu wa Mzimbe, kiazi cha mmea huo, kipo kwenye kundi la nyara za Serikali na
kwamba anayevuna au hata kupanda ndani na nje ya hifadhi akibainika anahesabiwa
amefanya kosa la jinai.
“Yapo
madai kwamba watu wanaohitaji aina hiyo ya kiazi kitokanacho na mmea huo
wamekuwa wakiwatumia wenyeji wa maeneo haya, kufanya uvunaji huo haramu na
hivyo kuathiri uoto wa asili wa hifadhi hii,” alisema.
Hata
hivyo Mzimbe alikanusha kuwepo kwa utafiti wa kisayansi unaothibitisha kwamba
mmea huo una uwezo wa kweli wa kuwatibu watu waliopungukiwa na kinga za mwili
kutokana na Ukimwi.
Katika
kukabiliana na majangili wanaovuna mmea huo, alisema wanatumia kitengo chao cha
ulinzi na intelejensia ambacho kwa kiasi kikubwa kimeanza kufanikiwa
kuwadhibiti.
Mhifadhi
wa Utalii katika hifadhi hiyo, Rimus Mkongwe alisema ndani ya hifadhi hiyo kuna
aina 40 za mmea huo. Hata hivyo alisema unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya
binadamu ni unatoa majani mawili.
Alisema
taarifa walizonazo kutoka katika nchi zinazonunua kiazi kitokanacho na
mmea huo zinaonesha kwamba kinaliwa zaidi na matajiri wakubwa wa nchi
husika.
No comments:
Post a Comment