Rais
Jakaya Kikwete amelitaka Jeshi la Polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya
vyombo vya haki watu wote waliohusika katika ulipuaji bomu lililosababisha kifo
na kujeruhi watu saba mjini Unguja, Zanzibar.
Kikwete
ambaye amesema kitendo hicho ni cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote
wapenda amani Bara na Visiwani, amekitaja kuwa ni cha woga kisicho
na ustaarabu, kisichokubalika katika dunia ya sasa.
Alisema
hayo katika salamu za rambirambi alizotuma jana kwa Rais Ali Mohamed Shein wa
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Bomu
hilo lilirushwa katika shughuli ya kidini iliyokuwa ikifanyika katika eneo la
Darajani , mjini Unguja. Miongoni mwa majeruhi, yumo mhubiri wa amani
ajulikanaye kama Sheikh Ahmed Haidari Jabir wa Zanzibar.
“Hicho
ni kitendo cha kulaaniwa kwa nguvu zote na watu wote wapenda amani Bara na
Visiwani, ni kitendo cha woga na kisicho na ustaarabu na wala hakikubaliki
katika dunia ya sasa,” alisema.
Rais
Kikwete aliongeza, “Hiki ni kitendo kilichofanywa na watu waoga, wasio na
ustaarabu wa aina yoyote ile.”
Alikemea
wanaofanya vitendo hivyo na akahimiza watu kuwa wastaarabu, wavumilivu na
kuheshimu imani na mitazamo ya watu wengine hata kama hawakubaliani nao.
Akiendelea
kulaani, alisema amesikitishwa zaidi na watu hao wasio na ustaarabu ambao
wamefanya kitendo hicho cha kihalifu kwenye shughuli ya kidini ambapo ndipo
mahali panapostahili amani, uvumilivu na unyenyekevu zaidi kwa kuwa ni wakati
ambapo binadamu anapofanya mawasiliano na muumba wake.
Alihimiza
polisi kuwasaka na kuwafikisha mbele ya vyombo vya haki wahusika wa tukio
hilo.
Kwa
mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi na Makosa ya Jinai wa Zanzibar, Yussufu
Ilembo, aliyekufa papo hapo ni Muhammad Mkombalaguha (26), mkazi wa
Tanga.
Kutokana
na tukio hilo, polisi visiwani humo ilitangaza hali ya hatari watu waliohusika
na shambulio hilo. Ilielezwa kwamba uchunguzi umeanzia kwenye mabaki ya vitu
vilivyokutwa katika eneo la tukio.
Miongoni
mwa vielelezo vilivyokusanywa ni pamoja na vipande vya mabaki ya gundi ya
karatasi na vitu vingine ambavyo vinasadikiwa vimetumika kutengeneza bomu
hilo.
Mtu
aliyekufa pamoja na majeruhi, walikutwa na mkasa huo wakati wakitoka Msikiti wa
Darajani baada ya Ibada ya Swala ya Isha inayoswaliwa kuanzia saa 1:45 usiku na
kuendelea.
Baada
ya kumalizika ibada hiyo, walitoka msikitini na kufika eneo la Darajani
wakisubiri gari na ndipo mlipuko mkubwa uliposikika ambao unasadikiwa kuwa ni
bomu.
Katika
hatua nyingine, akiwa mkoani Dodoma juzi, Rais Kikwete aliwataka Watanzania
kuendelea kulinda na kupigania amani iliyopo kwa ustawi na usalama wa
nchi.
Rais
Kikwete alisema hayo juzi kwenye uzinduzi wa tamasha la uzalendo
lililoasisiwa na wasanii wa muziki na filamu nchini ikiwa ni pamoja na uzinduzi
wa video ya wimbo maalumu wa Muungano wa Tanzania na Zanzibar.
Alisema
uzalendo kwa Watanzania ndiyo njia pekee ya kufanya taifa liendelee kutunukiwa
hadhi ya kisiwa cha amani duniani.
Katika
tamasha hilo lililofanyika Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Rais Kikwete alisema
ili kuwaenzi waasisi wa taifa, ni lazima kudumisha misingi ya amani
na kujitolea kizalendo kulilinda na kulitetea taifa kama walivyofanya waasisi
Mwalimu Julius Nyerere na Shehe Abeid Amaan Karume.
Pia
aliwataka wasanii kutumia vizuri talanta walizojaliwa kufikisha ujumbe
wenye uzalendo kwa Tanzania.
No comments:
Post a Comment