Wabunge
leo wanaanza mjadala wa bajeti ya Serikali iliyosomwa mwishoni mwa wiki
iliyopita.
Bajeti
hiyo inajadiliwa huku miongoni mwa maeneo yanayoonesha nafuu ikiwa ni
pamoja na hatua ya Serikali kutangaza kupunguza kiwango cha chini cha Kodi ya
Mapato ya Mishahara (PAYE) hadi asilimia 12 kutoka asilimia 13.
Pia
imeahidi kuongeza kima cha chini cha mishahara, ambacho hata hivyo
hakikutajwa.
Kwa
upande wa makusanyo, Waziri wa Fedha, Saada Mkuya alisema bajeti hiyo ya Sh
trilioni 19.8, Serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi ya
Sh trilioni 12,18.
Kati
ya hizo, mapato ya kodi ni Sh bilioni 11.31 na mapato yasiyo ya kodi, ni Sh
bilioni 859.8. Aidha, mapato yanayotokana na vyanzo vya halmashauri ni Sh
bilioni 458.5.
Katika
jitihada za kuongeza mapato zaidi, Waziri wa Fedha ameondolewa mamlaka ya
kusamehe kodi katika maeneo muhimu, ambapo Waziri Mkuya aliwaomba wabunge
waiunge mkono Serikali, katika hilo ili kurahisisha usimamizi wa kodi
nchini na hivyo kutoa unafuu kwa walipa kodi, na kuongeza mapato ya Serikali.
“Serikali itachukua hatua kuu mbili muhimu.
Kwanza, kutoa taarifa ya misamaha ya kodi kila robo mwaka kwa kuwatangaza
walionufaika na misamaha kwenye Tovuti ya Wizara ya Fedha.
“Hatua
hii itasaidia kuleta uwazi na uwajibikaji katika suala la misamaha ya kodi na
kuwafanya wananchi wajue ni nani anayenufaika na misamaha hiyo,” alisema.
Pili,
alisema Serikali itatoa taarifa ya kina ya misamaha yote ya kodi iliyotolewa na
kuiwasilisha bungeni kila mwaka, ili wabunge wapate nafasi ya kujadili na
kutoa maoni yao.
Hata
hivyo Waziri Mkuya alisema Serikali inaendelea na jitihada za kupata misaada na
mikopo ya masharti nafuu, ambapo inatarajia kupokea Sh trilioni 2.94. Kati ya
fedha hizo misaada na mikopo ya kibajeti ni Sh bilioni 922.1, mifuko ya kisekta
Sh bilioni 274.1 na miradi ya maendeleo Sh trilioni 1.75.
Waziri
Mkuya alisema kwa nia ya kuendeleza miradi ya miundombinu nchini, Serikali
itakopa katika soko la ndani Sh trilioni 3. Kati ya hizo, Sh
bilioni 689.56 ni za kugharimia miradi ya maendeleo na Sh trilioni 2.3 ni
kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva.
Pia
itakopa Sh trilioni 1.3 kutoka masoko ya fedha ya nje kwa masharti ya
kibiashara kwa ajili ya kugharimia miradi ya maendeleo.
Akizungumzia
mgawanyo wa fedha, Mkuya alitaja Sekta ya Elimu kuwa ndiyo iliyotengewa fedha
nyingi kuliko sekta yoyote katika sekta za kipaumbele zilizoteuliwa katika
Mpango wa Tekeleza kwa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Sekta
hiyo kwa mujibu wa Mkuya, imetengewa Sh trilioni 3.466, ambapo kati ya hizo Sh
bilioni 307.3 zimetengwa kugharimia mikopo ya elimu ya juu.
Fedha
zilizobakia zimepangwa kutumika kuimarisha ubora wa elimu ikijumuisha
miundombinu ya elimu. Alisema lengo ni kusaidia upatikanaji wa vifaa vya
kujifunzia na kufundishia, kuimarisha na kujenga madarasa na maabara.
Pia
Serikali katika sekta hiyo, imekusudia kuhakikisha vijana wanapata fursa
za ajira, hivyo juhudi zimewekwa kuimarisha vyuo vya ufundi stadi vilivyo chini
ya Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (VETA).
Sekta
ya pili kwa kupewa mgawo mkubwa ni miundombinu ya usafirishaji, ambapo Sh
trilioni 2,1 zimetengwa na kati ya hizo, Sh bilioni 179.0 ni kwa ajili ya
ununuzi wa mabehewa na ukarabati wa Reli ya Kati.
Aidha
Waziri Mkuya alisema Sh trilioni 1.4 ni kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa
barabara na madaraja. “Azma hii inalenga kupunguza msongamano wa magari mijini,
gharama za usafiri na usafirishaji wa bidhaa na huduma, na hivyo kupunguza
mfumuko wa bei.”
Sekta
inayofuata kwa kutengewa kitita kikubwa cha fedha ni Afya, ambayo Waziri Mkuya
alisema Sh trilioni 1.59, zimetengwa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, kuzuia
magonjwa ya mlipuko, chanjo za watoto, ujenzi wa zahanati na kudhibiti
maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi na malaria.
Sekta
ya Kilimo, imetengewa Sh trilioni 1,08, kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya
umwagiliaji katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya Ukanda wa Maalum wa Kilimo wa
Kusini mwa Tanzania (SAGCOT).
Pia
fedha hizo zimelenga kutumika kwa ajili ya ujenzi wa maghala na masoko; na
upatikanaji wa mikopo kwa ajili ya kukuza uzalishaji wa mazao ya chakula na
biashara.
Waziri
Mkuya alisema Serikali itaendelea kuwekeza kwenye ugani kwa kuimarisha vyuo vya
utafiti katika kilimo na kuhakikisha kunakuwa na maofisa ugani wa kutosha na
mbegu bora.
“Hatua hii itaimarisha uzalishaji wa mazao,
usalama wa chakula na kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya uhakika,” alisema.
Kwa
upande wa Nishati na Madini, Serikali imetenga Sh trilioni 1,09, kati ya hizo
Sh bilioni 290.2 zimetengwa kwa ajili ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA), ili
kusambaza umeme vijijini.
Aidha,
Sh bilioni 151 zimetengwa kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa bomba la gesi
kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam na Sh bilioni 90 zimetengwa kwa ajili ya
ujenzi wa mtambo wa kufua umeme kwa kutumia Gesi wa Kinyerezi I.
“Hatua hii inalenga kuhakikisha upatikanaji wa
umeme wa uhakika na kupunguza gharama zake na hivyo kuvutia uwekezaji na
kuongeza ajira,” alisema Waziri Mkuya.
Sekta
ya Maji imetengewa Sh bilioni 665.1 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu
ya maji mijini na vijijini ikiwa ni pamoja na kuendelea na ujenzi wa
visima katika vijiji 10 kwa kila halmashauri na kukamilisha ujenzi wa bomba la
maji kutoka Ruvu Chini hadi Dar es Salaam.
Katika
Utawala Bora, Serikali imetenga Sh bilioni 579.4 kwa ajili ya kuimarisha
utawala bora, ikiwa ni pamoja na kugharimia Bunge Maalum la Katiba;
vitambulisho vya Taifa; Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014; kuhuisha
Daftari la Kudumu la Wapiga Kura; maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015;
mapambano dhidi ya rushwa na utoaji wa haki kwa wakati.
Akizungumza
jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Profesa
Ibrahim Lipumba , alitaja masuala ya kuzingatiwa wakati wa utayarishaji wa
bajeti kuwa ni pamoja na bajeti kufikia malengo ya uchumi mpana, ukuaji wa pato
la taifa, mfumuko wa bei, akiba ya fedha za kigeni pamoja na thamani ya sarafu.
Profesa
Lipumba alisema bado bajeti iliyowasilishwa bungeni, haijaweka bayana juu
ya ukuaji wa deni la taifa ambalo limekuwa likikua kwa asilimia 20 kwa mwaka
wakati ukuaji wa uchumi ni asilimia 7 kwa mwaka.
Aidha,
alisema licha ya Serikali kusema bajeti imelenga kupunguza gharama za maisha
kwa wananchi, lakini wananchi walio wengi bado wanaona kuwa gharama za maisha
zinaendelea kupanda kwa kasi kubwa kuliko takwimu zinazotolewa na Serikali.
Profesa
Lipumba ambaye ni mchumi, alisema bajeti itabakia kuwa tegemezi kutokana na
mapato ya ndani kuwa madogo ikilinganishwa na matumizi ya kawaida ya Serikali.
Alisema
bajeti kama nyenzo muhimu ya sera za Serikali, inapaswa kuandaliwa kwa
umakini iweze kutekelezwa kwa mujibu wa mahitaji yaliyopo. Alihadharisha
juu ya utegemezi kwa bajeti ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment