Moja ya mitambo ya uchimbaji gesi. |
Wizara ya Nishati na Madini imefikia mwafaka na Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) katika suala la ugawaji vitalu vya gesi asilia na kukubalika Watanzania washiriki kila hatua na ambao wanataka kuwekeza kwenye sekta hiyo wajitokeze.
Katika mkutano uliofanyika jana kati ya Wizara hiyo na TPSF, pande mbili hizo zilikubaliana Watanzania watashiriki katika hatua ya utafutaji na uchimbaji gesi na ambao watakwenda kuomba vitalu kwa mtaji uliopatikana nchini au kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) watapewa kipaumbele.
Mkutano huo ulifanyika baada ya TPSF kuishutumu Serikali hasa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuwa alitoa tamko bungeni kuwa Watanzania hawana uwezo wa kuwekeza kwenye gesi, hivyo vitalu vya gesi asilia vitatolewa kwa wageni tu.
TPSF ilishutumu kauli hiyo ikisema haina uzalendo na yenye lengo la kutumia rasilimali za nchi kunufaisha wageni zaidi na kuacha Watanzania wakitazama. Hivyo kuitaka Wizara isitishe ugawaji vitalu hivyo hadi sera ya gesi itakapokamilika.
Lakini katika tamko la jana, Mkurugenzi wa TPSF, Godfrey Simbeye alisema wameelimishwa na Serikali kuwa kitakachofanyika Oktoba 25 si ugawaji vitalu vya gesi bali ni kuzinduliwa kwa mchakato kwa kutafuta watakaoshiriki katika utafutaji na uchimbaji gesi.
Alisema pia Serikali imewaelimisha kuwa shughuli za uchimbaji gesi zitaanza pale sera na sheria ya gesi vitakapokuwa tayari. Alisema makandarasi wa uchimbaji gesi hiyo watapatikana Septemba mwakani.
Simbeye alisema kwa mujibu wa maelezo ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, Watanzania bado wana fursa nyingi za kushiriki. "Ule wasiwasi wetu leo umeondoka, kwani Watanzania wako huru kushiriki mchakato huu na wenye uwezo wanaruhusiwa kuwasilisha maombi ya vitalu."
Alisema fursa hizo si kwenye uchimbaji tu bali hata kwenye utafutaji gesi. "Sisi tunafurahi kwa msimamo huu wa Serikali, kwani umetuhakikishia Watanzania ushiriki wetu na hata kushirikiana na hao wageni watakaokuja."
Mwenyekiti wa TPSF, Reginald Mengi alisema taasisi yake imeridhika kutokana na walichokuwa wakikitafuta kwani wamekipata, kwamba Watanzania watashiriki katika uchumi wa gesi asilia, ili utajiri huo uwe baraka na si laana kama ilivyo kwenye nchi zingine za Afrika ambako watu wanauana.
"Kwa msingi huu tulivyokubaliana hapa Watanzania hawatapigana, wala kuuana kwa sababu ya gesi, ninachowaomba Watanzania sasa wajipange kushiriki katika uchumi huu mkubwa wa gesi, ili baraka hizo zinufaishe wote na si watu wachache," alisema Mengi.
Maswi kwa upande wake, alisema Serikali imedhamiria kushirikiana na Watanzania kufanya nao kazi bega kwa bega katika hatua zote za mchakato wa kugawa vitalu.
"Leo hapa tumemaliza tofauti zetu sisi na TPSF na kinachofuata sasa ni uzinduzi wa zabuni ambao wote wenye nia watakaribishwa kuleta maombi yao," alisema Maswi.
No comments:
Post a Comment