MAKATIBU WAKUU WATAKA IDADI YA WIZARA IWEKWE WAZI...

Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Makatibu wakuu wa wizara za Serikali wamependekeza Katiba mpya itaje idadi ya wizara zinazotakiwa kuundwa na Serikali badala ya sasa hivi kila Rais kuwa na uhuru wa kuunda wizara zake.
Walitoa maoni yao jana mbele ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambayo ilikuwa zamu yao kutoa maoni. Kundi lingine ambalo lilitoa maoni yake ni Baraza la Mawaziri pamoja na wakuu wa mikoa.
Kikao cha Makatibu Wakuu kilifanyika katika ukumbi wa Karimjee wakati cha Baraza la Mawaziri kikifanyika Ofisi ya Waziri Mkuu huku kikao cha Wakuu wa Mikoa kilifanyika katika Ofisi ya Tume.
Suala hilo la wizara pia lilizungumzwa na makundi na baadhi ya wananchi ambao walitaka Katiba itaje idadi ya wizara na wengine kupendekeza idadi yake.
Kwa sasa kila Rais anayechaguliwa baada ya kushauriana na Makamu wake na Waziri Mkuu huunda wizara kulingana na vipaumbele vya serikali yao.
Baada ya kuunda wizara, Rais na wasaidizi wake hao huteua Baraza la Mawaziri na naibu mawaziri na wakati mwingine kumekuwa na madai kuwa Serikali inakuwa kubwa na mzigo kwa walipa kodi.
Habari zilizopatikana ndani ya kikao cha Makatibu Wakuu zilieleza kuwa makatibu hao pia walipendekeza idadi ya mikutano ya Bunge ielezwe kwenye Katiba badala ya sasa mikutano hiyo kufanyika kila baada ya miezi miwili.
Baadhi ya makatibu walipendekeza mikutano iwe mitatu kwa mwaka na kuepuka mtu kupangua, wakitaka Katiba ieleze Bunge kwa mwaka litafanya mikutano mitatu na si zaidi ya hiyo.
Mikutano ya Bunge hufanyika Februari, Aprili, Juni na Agosti na mkutano wa mwisho kwa mwaka hufanyika Novemba.
Mikutano hiyo hutanguliwa na vikao vya kamati za Bunge ambazo zinakaa kwa wiki mbili kabla ya mkutano kuanza.
Kwa upande wa wakuu wa mikoa, Abbas Kandoro (Mbeya) ambaye alitambulishwa na wenzake kuwa mzungumzaji, alisema hawako tayari kujitetea kama vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya viendelee kuwapo au la.
“Sisi ndio tunaozungumzwa na wananchi, hivyo katika eneo hilo naomba tuwaachie wananchi wenyewe na naamini Tume itaheshimu mawazo yao na tukijitetea hapa hatutawatendea haki wananchi,” alisema Kandoro.
Badala yake Kandoro alisema yeye na wenzake wangependa kuona Katiba mpya inadumisha umoja, mshikamano na uzalendo wa Watanzania.
Pia alisema wangependa kuona Katiba mpya inatamka kuwa nchi itaongozwa kwa sheria na utawala bora. “Kuna shida tunazipata kwa sababu tu watu hawaheshimu utawala wa sheria.”
Vyeo vya wakuu wa mikoa na wilaya vimetolewa maoni mengi na wananchi na baadhi yao wangependa viondolewe kwa vile watendaji wanafanya kazi za kisiasa badala ya maendeleo.
Wengine wanapenda hata kama vikibaki basi wakuu wa wilaya na mikoa wachaguliwe na wananchi wa mikoa husika badala ya kuteuliwa watu ambao hawana uchungu na mikoa wanamofanyia kazi.

No comments: