WALIMU SASA WAGEUKIA KAZI YA UGANGA WA KIENYEJI...

Imeelezwa kuwa baadhi ya walimu mkoani Simiyu hujihusisha na shughuli za uganga wa kienyeji, ujambazi  na uendeshaji wa bodaboda kama sehemu yao ya kujitafutia kipato cha ziada, wakiamini kwamba kutegemea mshahara pekee hautoshi.
Hayo yameelezwa jana na Katibu Tawala wa mkoa huu (RAS), Mwamvua Jilumbi, alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha Bodi ya uteuzi wa wanafunzi kujiunga na kidato cha kwanza mwakani ambacho kilifanyika wilayani Bariadi
Jilumbi alitoa maelekezo hayo kwa maofisa elimu wa wilaya na mkoa ili kufuatilia kikamilifu changamoto zinazowakabili walimu na kuzitafutia ufumbuzi.
“Hali ya walimu katika mkoa wetu sio nzuri, baadhi ya maeneo walimu wamefikia hatua ya kuacha majukumu yao ya kufundisha na kujihusisha na shughuli za uganga wa kienyeji. Wengine wanaendesha bodaboda na wengine hata kujihusisha na matukio ya uhalifu.
“Wakati fulani mwalimu mmoja mkoani Shinyanga aliwahi kushiriki kwenye tukio la kuiba kwenye ofisi ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT) mkoani Shinyanga, lakini kwa bahati mbaya alikutwa na kupigwa risasi mguuni, akakimbilia Dar es Salaam,” alisema.
Alisema Mwalimu huyo alipofika Dar es Salaam alienda kwa chama cha walimu kudai kuwa amefutiwa mshahara wake.
“Walipofuatilia kwa RAS Shinyanga wakagundua kuwa madai ya mwalimu hayakuwa ya kweli, badala yake walikuta vielelezo na ushahidi mwingi wa mambo ya uhalifu aliyofanya,” alisema.  
Jilumbi aliwaagiza Maofisa Elimu wa wilaya za mkoa huo kuacha tabia ya kukaa ofisini na badala yake watembelee wilaya zao ili kuweza kuzibaini changamoto nyingi zinazowakabili walimu na kuzitafutia ufumbuzi kila inapowezekana.
 “Niwaagize maofisa elimu ondokeni kwenye meza zenu, acheni kukaa ofisini. Nendeni maeneo ya vijijini ili mkayashughulikie matatizo ya walimu maana nyie mnawajibika wakati wa mitihani tu lakini sijawahi kuona mnaenda kuulizia kwa mfano ni walimu wangapi wanafundisha na ni wangapi hawafundishi na kwanini,” alisema.
Kuhusu madai ya walimu, Jilumbi alisema alishituka kusikia kuwa wapo baadhi ya walimu mkoani humu wanaoidai serikali kiasi cha Sh milioni 521 wakati kuna fedha za madai ya walimu zilizotolewa kwenda mkoani Simiyu na walimu wakalipwa, zingine zikabaki na kurudishwa hazina.
“Hivi majuzi nilialikwa na CWT kwenda kuwafungulia mkutano wao, lakini nilielezwa kuwa wapo baadhi ya walimu wanaoidai serikali. Nilishangaa kwa sababu serikali ilishatoa kiasi cha Sh bilioni 29 kwa ajili ya kulipa madeni hayo ya walimu. Kama ndivyo ni kwanini sasa fedha nyingine ilirudishwa hazina, hebu nendeni mkawasimamie watu wanaojihusisha na madai ya walimu,” alisema.
Aliongeza: “Hapa ninapata shaka na watumishi wanaohakiki madeni, maana haiwezekani fedha zilizotolewa kwa walimu na serikali zilipwe halafu nyingine zirudishwe hazina wakati uhakiki wa madeni ya walimu sasa unafanywa na watumishi wetu… Na kwanini sisi kama mkoa tuendelee kuwa na madeni?” Alihoji.
Alisema matatizo ya madai ya walimu lazima yashughulikiwe ili kuwaepusha walimu kutoendelea kuchukua maamuzi ambayo wakati mwingine yanavuruga taaluma.
“Si mnajua walimu wamefikia hatua ya kusambaziana ujumbe… Hebu myashughulikie kila mtu kwa eneo lake,” alisema na kuwataka wakurugenzi na maofisa elimu kuhakikisha kuwa walimu wanaoripoti kwenye vituo walikopangiwa na wakisharipoti wanafanya kazi ya kufundisha na si vinginevyo.

No comments: