NJUGA ZA MWAKYEMBE ZAMKOSHA MAGUFULI...

Dk John Magufuli.
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli amempongeza Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe katika hatua za kufufua usafiri wa reli nchini na kusema kuwa hatua hiyo inazipa barabara unafuu.
Aidha, ameitaka Bodi ya Mfuko wa Barabara kutopeleka mgawo wa fedha za barabara kwenye halmashauri ambazo zimeajiri mafundi mchundo badala ya wahandisi waliosajiliwa na kutaka halmashauri zote kuhakikisha zinatumia fedha za barabara kama zilivyopangwa.
Dk Magufuli pia amezitaka wizara ambazo magari yake hayajasajiliwa kuhakikisha zinafanya hivyo huku akizitaka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ndizo zinazoongoza kwa kuwa na magari yasiyosajiliwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara na Bodi ya Wakala wa Barabara (Tanroads) jana, Dk Magufuli alisema hatua ya Waziri Mwakyembe kuvalia njuga suala la kufufua reli linasaidia kupunguza mzigo na unafuu wa uharibifu wa barabara.
“Nchi za wenzetu zilizoendelea, mizigo mingi na watu wanatumia usafiri wa reli, jambo ambalo linasaidia barabara kudumu kwa muda mrefu na ni muhimu kwa uchumi pia. Naomba mnifikishie pongezi zangu,” alisema Dk Magufuli, akielekeza pongezi hizo kwa Dk Mwakyembe.
Dk Mwakyembe ambaye kama Dk Magufuli, wanasifika kuwa miongoni mwa mawaziri wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wanaochapa kazi, alianzisha usafiri wa treni katika Jiji la Dar es Salaam mwishoni mwa Oktoba mwaka huu, na usafiri huo umeungwa mkono na wananchi wengi, na umeilazimu Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kuongeza mabehewa zaidi katika treni hizo mbili za kwenda Ubungo na ile ya Pugu.
Aidha, wiki moja iliyopita, Dk Mwakyembe alizindua upya safari za treni za kwenda mkoani Mwanza baada ya kampuni hiyo ya reli kusimamisha huduma hiyo tangu mwaka 2009. Kurejeshwa kwa safari hizo kumepokewa kwa furaha kubwa na wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Kuhusu suala la Halmashauri, Dk Magufuli aliitaka Bodi ya Mfuko wa Barabara kutopeleka fedha kwa halmashauri ambazo hazijaajiri wahandisi waliosajiliwa.
“Utafiti unaonesha kuwa asilimia 46 ya halmashauri hazijaajiri wahandisi waliosajiliwa, hivyo zile zilizoajiri mafundi mchundo, zisipelekewe fedha ili wajifunze kuajiri watu wenye sifa, maana nao hawa wanachangia matumizi mabaya ya fedha,” alisema Waziri wa Ujenzi.
Aliongeza: “Kagueni miradi yote na muwe wakali ingawa mimi ni mpole, pamoja na Tanroads kufanya kazi nzuri nao si malaika, kuna baadhi ya miradi imekamilika kwa kiwango cha chini. Na mameneja wa mikoa wanaoshindwa kusimamia miradi, wachukuliwe hatua, nadhani hapo watajifunza kufuata sheria.”
Hata hivyo, Magufuli aliitaka Bodi ya Tanroads kuhakikisha inapambana na rushwa hasa katika mizani na kuangalia Idara ya Manunuzi ambao wanashirikiana na makandarasi katika matumizi mabovu ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya barabara.
Pia aliitaka Tanroads kupunguza foleni, kuja na ubunifu wa kujenga barabara za juu (flyovers) na kuacha kuwa na kigugumizi kwani Watanzania hawana muda wa kusubiri na wanachotaka ni matokeo.
“Msiwe wanasiasa, kila kukicha ‘tuko kwenye mchakato’ neno hilo waachieni wanasiasa ndio tumezoea kulitumia, ninyi mfanye kazi kwa vitendo. Sielewi ni kwa nini barabara ya Mwenge-Morocco bado nyumba hazijabomolewa, wanaostahili kulipwa fidia walipwe, na wale wavamizi watupishe,” alisema.
Kuhusu suala la usajili wa magari ya Serikali, Dk Magufuli alisema: “Hadi leo (jana) zaidi ya magari 974 yaliyokuwa na namba za kiraia yamesajiliwa, bado kama magari 746 na wizara zinaongoza ni ya Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi. Message sent” (ujumbe umefika).
Serikali ilitoa siku 27 kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 15, mwaka huu kuhakikisha wizara na taasisi za Serikali zinabadili namba za magari yaliyokuwa kwenye namba za kiraia, lengo likiwa ni kukomesha tabia ya baadhi ya watumishi wa umma kutumia magari kwa matumizi binafsi na kufanya ubadhirifu wa mafuta yanayonunuliwa kwa kodi za wananchi.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Dk James Wanyancha pamoja na kumshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumteua, alisema Bodi yake haitakuwa tayari kuona ubadhirifu unafanywa kwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya barabara.
“Ubadhirifu wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara unachangia wananchi kuichukia Serikali, sasa sisi hatutakuwa tayari kuoana hilo linatokea,” alisema Dk Wanyancha.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tanroads, Hawa Mmanga alisema barabara bora ndizo zitakuwa chachu ya ukuaji wa uchumi na kuahidi kufanya kazi ili kuhakikisha azma ya Serikali inafikiwa.
Katika hatua nyingine, Dk Magufuli amemteua Mhandisi Consolatha Ngimbwa kuendelea kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB). Ngibwa kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Electrics International Co. ltd.
Taarifa iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Balozi Herbert Mrango, ilisema pia Dk Magufuli amewateua wajumbe wanane wa Bodi hiyo.
Wajumbe hao ni Joseph Tango, Samuel Shilla, Lawrence Mwakyambiki, Stephen Makigo, Andrew Masawe, Joseph Nyamhanga, Abraham Senguji na Dudley Mawala.
Bodi hiyo ina jukumu la msingi la kusajili makandarasi, kusimamia mwenendo wao, kujenga uwezo wa makandarasi wa Kitanzania na kulinda maslahi ya watumiaji wa makandarasi.

No comments: