Ikulu ya Zanzibar. |
Mzee alisema hayo jana, alipozungumza katika mdahalo wa kujadili na kutafakari muundo huo wa Serikali, ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT) kwa lengo la kutoa elimu zaidi kwa waandishi wa habari, kuhusu umuhimu wa Serikali ya aina hiyo na changamoto zake.
Pamoja na kutaka waandishi wa habari, kuitangaza vizuri Serikali hiyo, kwa kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta amani na utulivu nchini na kuondosha siasa za chuki na uhasama, pia alitaja changamoto inazozikabili, ikiwemo hiyo ya Muungano.
Akifafanua changamoto hiyo, alisema inatokana na tofauti ya sera zinazotokana na vyama vya siasa katika kuongoza nchi, ikiwemo katika Muungano ambapo sera ya CCM ni Muungano wa Serikali mbili wakati sera za CUF ni Muungano wa Mkataba.
Alisema tofauti ya sera za vyama katika suala la Muungano, linalokwenda sambamba na utoaji wa maoni ya wananchi katika marekebisho ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kiasi kikubwa limeanza kuzusha malumbano na kutishia kuyumba kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Kumejitokeza suala la tofauti ya sera za vyama vya siasa kati ya CCM na CUF katika utoaji wa maoni ya marekebisho ya Katiba...limeanza kuzusha malumbano ambayo yanaweza kuyumbisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Mzee.
Alisema pia lipo tatizo kwa baadhi ya watendaji wa Serikali, kushindwa kuheshimu utendaji wa Serikali hiyo huku wengine wakiifananisha na paa moja katika nyumba ambalo linaweza kuanguka wakati wowote.
Mzee ambaye amewahi kuwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi, alisema wakati umefika kwa baadhi ya taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, muundo wake uwe na sura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa huku akitoa mfano wa Baraza la Wawakilishi.
“Pale katika Baraza la Wawakilishi, muundo wake una shaka...hakuna sura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu Spika anatoka katika Chama Cha Mapinduzi pamoja na Naibu wake na watendaji wengine”, alisema.
Pamoja na changamoto hizo, Mzee alitaja mafanikio makubwa ya Serikali hiyo, ambayo yanapaswa kutangazwa na vyombo vya habari, kuwa ni kuimarika kwa utulivu wa nchi na washiriki wa maendeleo kurudisha misaada yao katika nyanja mbalimbali.
Alisema zipo baadhi ya nchi za Bara la Afrika, zilizounda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini zimeshindwa kupata mafanikio mazuri katika kipindi kifupi, ikilinganishwa na Zanzibar, kwa kuwa viongozi wake wakuu wamekuwa wakilumbana mara kwa mara.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa inafikia umri wa miaka miwili tangu kuasisiwa kwake, lakini nawaomba waandishi wa habari waeleze mafanikio yake kwa wananchi, ikiwemo kurudi kwa amani na kuondoka chuki na siasa za uhasama,” alisisitiza.
No comments:
Post a Comment