TANESCO YAOMBA KUPANDISHA TENA BEI YA UMEME...

Mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo eneo la Ubungo, Dar es Salaam.
Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limeomba kupandisha gharama za umeme kwa asilimia 81.27 kutoka Sh 196 ya sasa hadi Sh 359 kwa uniti moja ya umeme ili litoe huduma bora za upatikanaji wake.
Jana ilikuwa siku ya wadau na wananchi wa kawaida iliyotengwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kujadili maombi hayo ya Tanesco katika mkutano wa taftishi, uliofanyika kwenye Ukumbi wa Karimjee jijini Dar es Salaam.
Lakini cha ajabu, wananchi ambao wamekuwa wepesi kulalamika juu ya bei hizo mpya, hawakufika kwenye mkutano huo na badala yake ni watendaji wa taasisi mbalimbali na wanahabari ndio waliokuwepo.
Mara ya mwisho, Tanesco ilipandisha gharama za umeme Januari mwaka huu, ikiomba kupandisha bei hizo kwa asilimia 155, kutokana na madai kuwa wanatumia mitambo ya dharura inayogharimu fedha nyingi.
Hata hivyo, Ewura ilipandisha gharama hizo kwa asilimia 40.29, licha ya kuwa bei hiyo ilikuwa iwe kwa miezi sita, Ewura waliongeza muda kutokana na mahitaji ya Tanesco.
Hali hiyo ya wananchi kutofika kwenye mjadala huo, ilimshtua hata Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki, ambaye alionesha kusikitishwa na hali hiyo.
Sadiki alisema licha ya matangazo mengi yaliyotolewa ne Ewura kwenye vyombo vya habari, lakini idadi ya wananchi walioitikia mwito huo, ilikuwa ni ndogo mno.
“Wananchi bei zikipandishwa ni wepesi wa kulalamika, lakini walitakiwa wafike leo watoe maoni yao, cha ajabu wameshindwa kufika”, alisema kwa masikitiko Mkuu huyo wa Mkoa.
Katika mkutano huo, wengi walikuwa ni waandishi wa habari, maofisa wa Ewura na Tanesco na wadau kutoka Shirikisho la Wenye Viwanda na Chama cha Wafanyabiashara Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA).
Wakati Tanesco inaomba kupandisha kiasi hicho cha bei ya umeme, Mshauri Mwelekezi aliyekodiwa na Ewura baada ya kufanya utafiti na kukokotoa hesabu zake, amependekeza bei ya umeme ipande hadi kufikia Sh 254 kwa uniti moja kiasi ambacho ni asilimia 29.5.
Mtaalamu huyo katika maoni yake, amependekeza kuwa bei ipande kwa Sh 288.39 kwa wateja wa majumbani ambao wako kundi la D1, wateja wa T1 ambao ni wa majumbani na wafanyabiashara ndogo iwe Sh 306.52, wateja wa T2 Sh 167 na wateja wa T3 iwe Sh 134.
Wadau wachache ambao walifika kwenye mkutano huo, walipinga maombi hayo ya Tanesco, kwa maelezo kuwa shirika hilo halijafanya jitihada za kupanua wigo wake wa mapato, badala yake limekuwa likikimbilia kwa wateja mara inapotokea ongezeko la gharama.
Ewura imetenga siku 14 kwa wadau mbalimbali kutoa maoni yao na wale ambao hawakupata muda wa kufika kwenye mkutano huo, wanaweza kutoa maoni yao na kuyawasilisha Ewura kwa barua au kwa njia yoyote ya mawasiliano kabla ya kuchukua uamuzi  wa kupandisha au kutopandisha bei  ya umeme.
Bei hiyo mpya inatakiwa ianze kutumika Januari mwakani na kwa hali ilivyo ni wazi kuwa gharama hizo zitaongezeka, kutokana na pendekezo la mshauri huyo pamoja na utetezi wa Tanesco, ambao hata hivyo umepingwa na wadau waliofika kwenye mkutano huo kuwa hauna nguvu.
Akitetea hatua hiyo ya kupandisha umeme, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesm Mramba, alipinga pendekezo hilo la Ewura ambalo limetolewa na mtaalamu mshauri, kwa maelezo kuwa halikuzingatia hali halisi ya Tanesco ilivyo kwa sasa.
Mramba alisema sababu za Tanesco kuomba kupandisha umeme kwa asilimia 155 mwaka jana, bado ziko pale pale ambazo ni ukame, aliofanya mabwawa ya maji yaendelee kukauka na  kuilazimisha Tanesco kutegemea umeme wa mafuta, ambao ni wa kampuni binafsi.  
Alisema pia mkopo wa Sh bilioni 408, ambao Serikali ilikuwa iweke dhamana, haukupatikana na kuifanya Tanesco kuendelea kuwa katika hali mbaya ya kifedha. Alisema licha ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh bilioni 136, ambazo awali ilikuwa ni mkopo, lakini bado hali ni mbaya.
Alisema licha ya kuwepo kwa mitambo inayotumia maji; lakini hakuna maji. Pia alisema licha ya kuwepo mitambo ya kutumia gesi ya Ubungo na Tegeta, gesi inayotoka Songosongo kwa sasa, haitoshelezi kuzalisha megawati nyingi za umeme, badala yake uwezo wa mitambo hiyo ya gesi ni megawati 329 tu.
Kwa hali hiyo, alisema watalazimika kuendelea kutumia mitambo ya IPTL kuzalisha megawati 100, ambayo kwa siku Tanesco inatumia Sh bilioni 1.4 kwa ajili ya mafuta, Agreko megawati 100 sawa na Sh bilioni 1.5 kwa siku kununua mafuta.
Kwa mitambo ya Symbion ambayo inazalisha megawati 160, Mramba alisema fedha zinazotumika kununua mafuta ni Sh bilioni 1.5 kwa siku.
“Gharama zote kwa siku ni Sh bilioni 5.2 kwa ajili ya kununua mafuta peke yake na gharama hizi ni nje ya Sh bilioni 27 ambazo zinalipwa na Tanesco kila siku kama Capacity Charge,” alisema Mramba wakati akitetea uamuzi wa kuomba kupandisha gharama za umeme. Kwa maana hiyo gharama za mafuta na Capacity Charge kwa siku ni Sh bilioni 32.
Mramba aliendelea kudai kuwa iwapo bei ya umeme haitapanda, ikifika mwishoni mwa 2013 Tanesco itakuwa na hasara ya Sh bilioni 878,065, kwani gharama za uzalishaji zitakuwa kubwa kuliko mapato.
Alisema kwa sasa uendeshaji wa shirika hilo ni mbaya, hali ambayo imeilazimu Serikali kutoa Sh bilioni 138 kama ruzuku.
Pia, alisema hadi kufika Oktoba mwaka huu, Tanesco imelimbikiza deni la Dola za Marekani milioni 250 kutoka kwa  wazalishaji wa umeme na wadau wengine, ambao wanaisambazia vifaa mbalimbali.
Lakini, alisema iwapo bei itapanda, mapato ya shirika yatakuwa ni Sh trilioni 2, kiasi ambacho ni sawa na gharama za uzalishaji wa umeme.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uchumi wa Ewura, Felix Ngamlagosi, alisema bei zilizotolewa na mtaalamu mwelekezi, zimezingatia gharama za usambazaji, uzalishaji na usafirishaji na miundombinu ya Tanesco iliyopo.

No comments: