MRISHO NGASSA ASAINI KUCHEZEA YANGA, AITOSA EL MERREIKH...

Mrisho Ngassa.
Ni kama mchezo wa kuigiza vile, lakini ukweli ni kwamba Mrisho Ngassa ameghairi kwenda El Merreikh ya Sudani na sasa amesaini Yanga ya Dar es Salaam kwa ajili ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Habari za uhakika ambazo zimepatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya kuaminika jana usiku,  vyanzo hivyo vikiwa pamoja na Ngassa ni kwamba mshambuliaji huyo amefuta mpango wake wa kwenda Khartoum, Sudan kujiunga na El Merreikh na kuweka wazi nia yake ya kuchezea Yanga.
“Kuna mazungumzo na Ngassa yanaendelea hapa, ameamua mwenyewe kwa hiari yake aachane na mipango ya kwenda Sudan badala yake anataka acheze Yanga, huo ndio ukweli ulivyo.
“Lakini mkataba wake na Yanga utaeleza wazi kwamba atajiunga na timu yetu mara tu baada ya kumaliza mkataba wake wa kucheza kwa mkopo katika klabu ya Simba. Kwa maana hiyo atavaa rasmi jezi za Yanga msimu ujao.
“Tumebishana kidogo, lakini hatimaye tumekubaliana tumchukue kwani kama akienda El Merreikh itakuwa ngumu kumrudisha Yanga, wakati mwenyewe anataka acheze Yanga,” kilisema chanzo hicho usiku jana wakati wakiwa na Ngassa.
Kwa mujibu wa chanzo hicho ambacho hakitaki jina lake litajwe ni kuwa Ngassa yupo huru kuzungumza na timu yoyote kwani mkataba wake na Azam umebaki miezi sita, ingawa pia Simba inadai iliingia naye mkataba mwingine wa mwaka mmoja pale mkataba wa sasa wa mkopo utakapomalizika.
Ngassa kwa upande wake alipoulizwa kwanza alionekana kushtuka kisha akasema hawezi kufanya uamuzi wa kwenda Yanga wala kuzungumza nao lolote kwa sasa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Abdallah Bin Kleb alipotafutwa jana simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.
Wiki iliyopita Azam ilitangaza kumuuza Ngassa kwa timu ya El Merreikhn kwa dola za Marekani 75,000, ambapo juzi klabu hiyo ilisema mchezaji huyo atakuwa akilipwa dola za Marekani 4,000 (Sh. Milioni sita za Tanzania) kwa mwezi.
Lakini mauzo ya Ngassa kwenda El Merreikh yanaonekana kuzigonganisha Azam na Simba, huku Simba ikilalamika kutotendewa haki kwa madai Azam ilipaswa kuwataarifu kabla ya kumuuza Sudan.
Tayari Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage ameliandikia barua Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupinga mauzo ya mchezaji huyo na kuliomba shirikisho hilo lisitoe Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC).
Kutokana na mshahara huo kwa kipindi cha miaka miwili Ngassa atavuna Sh. Milioni 144 na ukichanganya dola za Marekani 50,000 (Sh.milioni 80) atakazopata kwa kusaini mkataba huo Ngassa atakuwa ametengeneza Sh, milioni 230 kwa miezi 24.
Kama Azam ingefanikiwa kumuuza Ngassa El Merreikh, Yanga pia ingepata sehemu ya mgawo kwa mauzo hayo kwani wakati inaiuzia Azam mwaka 2010 iliweka kipengele katika mkataba kwamba ikitokea Azam ikamuuza itabidi Yanga ipewe asilimia tano ya mauzo hayo.

No comments: