ELIMU YA TANZANIA SASA IKO TAABANI...

Hili ni moja ya madarasa katika Shule ya Msingi Ruvu Darajani, mkoani Pwani.
Wasomi na wanasiasa wamekiri kuwa elimu ya Tanzania iko taabani kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi wanaoshindwa katika mitihani na wanaofaulu ambao hawajui kusoma, kuandika na kuhesabu.
Ili kurejesha ubora wa elimu, washiriki wa Kongamano la Uhuru na Mustakabili wa Taifa letu miaka 50 ijayo lililoandaliwa na Chama cha Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA) jana Dar es Salaam, walipendekeza ualimu iwe fani inayolipwa zaidi mshahara kuliko fani zingine na vijana wanaopata daraja la kwanza na pili ndio wakasomee fani hiyo.
Akitoa mada, Mhadhiri wa Udsm, Dk Kitilya Mkumbo alisema elimu inayotolewa nchini ni ya kibinafsi kwani inaandaa watoto wasome waje wapate kazi, wapate fedha ili wanunue magari na mashamba.  
Dk Mkumbo alisema elimu ya sasa inalenga kufaulisha mtihani, na matokeo yake kile kinachotarajiwa cha kuchambua mambo ni madogo na kutoa mambo ambayo ni mepesi mno na kuridhika na mafanikio madogo madogo.
“Tunatoa mfumo wa elimu ambao sio wabishi kwa vile sio wadadisi wa mambo,” alisema Dk Mkumbo na kuongeza kuwa Tanzania kwa sasa inatoa jamii isiyoamini katika sayansi ndio maana watu wanakimbilia Loliondo kwenye kikombe cha Babu badala ya kwenda hospitalini.
“Ili tutoke hapo ni lazima tukazanie kutoa elimu ya kilimo. Ajabu ni kwamba kilimo katika nchi hizi hakifundishwi, lazima watoto wetu wasome kilimo kuanzia shule ya awali hadi chuo kikuu wakimaliza wakalime na tudhamirie kuilisha Afrika Mashariki,” alisema mhadhiri huyo.
Alisisitiza kuwa Taifa ni lazima liwekeze katika walimu kwani nchi zote ambazo zimepiga hatua katika maendeleo waliwekeza katika walimu.
“Nchi yetu hii tumeamua kutelekeza walimu, ili uingie huko ni lazima ufeli ni lazima tubadilishe mfumo huu na tunatakiwa kuwekeza katika walimu,” alieleza.
Alionya kuwa nchi isipowekeza katika walimu bora tusahau kuwa na elimu bora. Pia alitaka Jamii iwaheshimu walimu la sivyo elimu haiwezi kwenda popote. 
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba alisema kama Tanzania inataka kuboresha elimu, Serikali ihakikishe inaifanya kazi ya ualimu iwe inalipa zaidi kuliko fani zingine kwani kufanya hivyo vijana wote wanaopata daraja la kwanza watakimbilia huko.
Alisema nchi zingine duniani wanafanya hivyo.
“Tufanye hivyo  kuanzia sasa ni taaluma inayolipa kama ilivyo TRA. Walimu wanatusaidia kutengeneza kizazi cha siku za mbele ni lazima walipwe vizuri,” alisema January na kuongeza kuwa inasikitisha kuwa vijana waliofeli ndio wanapelekwa kwenye ualimu.
Naye Dk Martha Qorro alisema kushuka kwa elimu kunatokana na wanafunzi kufundishwa lugha wasiyoifahamu hivyo kufanya wafeli katika mitihani. 
“Tubadilisheni lugha na tutumie lugha inayofaa ili watoto waweze kufahamu elimu wanayopata.  Tukitumia lugha isiyofahamika suala la maadili na kilimo haliwezi kufundishika vizuri. Kama wananchi hawawezi kushiriki yale tunayojifunza vyuoni, elimu ya sasa haijalisaidia Taifa,” alisema Dk Qorro.
Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe alisema viongozi wetu walisoma vizuri ila sasa hivi wanachuo wengi wanasoma katika mazingira magumu. Alisema viijana wana haki ya kusoma bure, kama walivyosoma maprofesa, “ila hatuna mtu wa kutuhamasisha sasa ni heri wasomi mtuhamasishe kwa hilo.”
Kwa upande wake, Dk Qlein Mtembei alisema elimu imeporomoka kwa sababu wanafunzi hawapati maarifa na uelewa kama inavyotakiwa na hivyo wanashindwa kuwa wagunduzi na wabunifu.
 Alisema Tanzania ilikosea katika lugha ya kutolea elimu tangu mwaka 1962? Alihoji. “Kwa nini mtu umfundishe mtoto historia kwa kutumia Kiingereza. Watu wanakosa uzalendo kwa vile hawaelewi kutokana na kufundishwa Kiingereza,” alisema Dk Mtembei. 
Alihoji. “Yaani mtu awe raia mwema ni lazima afundishwe kwa Kiingereza? Lugha ya Kiingereza ni muhimu hakuna anayebisha, lakini haipaswi kutumika kufundishia.” Aliongeza kuwa wanafunzi wanatumia muda mrefu kujifunza lugha ya kufundishia na kujifunza somo lenyewe. 
Dk Mtembei alisema elimu kwa sasa haimuandai mtoto kuwa mgunduzi, mvumbuzi na akasema “tunaomba tupatiwe sekondari moja tu ya mfano. Mturuhusu tufundishe masomo yote kwa Kiswahili, tunaamini wanafunzi watafaulu vizuri.”

No comments: