KANISA LA KKKT HAPAKALIKI, WAUMINI HAWAMTAKI ASKOFU MKUU...

Askofu Mkuu Thomas Laizer.
Mgogoro umeibuka kati ya baadhi ya waumini na viongozi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati baada ya kuweka mali za Kanisa rehani na kuchukua mkopo ambao sasa unahatarisha mali hizo kunadiwa.
Hali hiyo imesababisha baadhi ya waumini wa dayosisi hiyo kuwatupia lawama viongozi wakuu wa kanisa hilo akiwemo Askofu Mkuu, Thomas Laizer na Katibu Mkuu wake, Israel Karyongi na kuwataka wajiuzulu.
Viongozi hao wanadaiwa kuwa ndio chanzo cha kufikia hali hiyo na kwamba wamekuwa wakitumia miradi ya kanisa hilo kwa manufaa yao binafsi na kusababisha kuwa hatarini kunadiwa na benki.
Habari za kutoka ndani ya Dayosisi hiyo, zinadai kuwa miradi inayodaiwa kuwa fedha zake zimetumika vibaya ni Hoteli ya Corridor Springs na Hospitali ya Rufaa ya Selian, ambayo kwa pamoja iligharimu Sh bilioni 11 kutoka katika michango ya waumini na misaada kutoka kwa wafadhili.
Hata hivyo, wakati ikidaiwa kuwa fedha hizo zimetokana na michango ya waumini na wafadhili, kuna madai mengine kuwa zilikopwa katika moja ya benki nchini kwa ajili ya uanzishwaji wa miradi hiyo.
Kutokana na hatari ya kunadiwa kwa miradi hiyo, waumini zaidi ya 600,000 wa Dayosisi hiyo wiki moja iliyopita wametakiwa kuchangia Sh 20,000 kila mmoja ili kuokoa jahazi. Kama waumini wote hao wakitoa mchango wao kama ilivyotarajiwa, zitapatikana Sh bilioni 12.
Wakizungumza mara baada ya ibada Jumapili iliyopita, baadhi ya waumini walionesha wazi kutilia shaka hatua ya viongozi hao kuwachangisha michango wakati awali waliambiwa kuwa miradi hiyo ilidhaminiwa kwa asilimia 100 na Shirika la Peace House la Marekani.
“Tuliambiwa awali kuwa miradi hii ambayo iligharimu Dola za Marekani milioni 7, sawa na Sh bilioni 11 za Tanzania, ilidhaminiwa na Shirika la Peace House la Marekani,leo wanatuambia walikopa fedha benki (anaitaja).
“Haikubaliki hapa kuna ufisadi umefanyika, tunataka Mzee Laizer (Askofu) na Katibu Israel Karyongi wakae pembeni,” alisema mtoa habari wetu.
Chanzo cha kukopa fedha hizo benki inadaiwa wakati miradi hiyo ikiwa katika hatua zake za kukamilika, wafadhili wa miradi hiyo walibaini hujuma iliyokuwa ikifanywa na viongozi wa Kanisa, wakajitoa kufadhili kulitaka Kanisa kurejesha fedha zao.
“Wafadhili walipojitoa wazee hawa wakaenda benki kukopa fedha ili kuwarejeshea wazungu hao fedha zao lakini kwa sharti kuwa miradi hiyo iwe dhamana ya mkopo hadi watakapomaliza kulipa.”
“Lakini cha kushangaza wakati wanakopa hawajashirikisha washarika mpaka hapo walipokiuka mkataba na benki kugundua kuwa hawana uwezo wa kulipa mkopo kwa wakati ndipo wanatuambia sasa… tunashangaa ndio maana tuna wasiwasi,” aliongeza muumini mwingine ambaye hakutaka jina lake liandikwe.
Kutokana na hali hiyo ya kukiuka masharti ya mkopo, mtoa habari huyo alidai benki hiyo iliandika barua kwa Dayosisi hiyo kuelezea kusudio la kuzikamata mali hizo za washarika kabla ya Januari mosi mwakani.
“Bila aibu wanakuja na kuwatangazia washarika kuwa tunadaiwa na ikifika Desemba 31 kama hatujalipa deni hilo, hoteli itauzwa kwa mnada. Hii haikubaliki lazima hatua zichukuliwe haraka na watakaobainika kuhusika wafikishwe mahakamani,” alidai muumini ambaye ni mzee wa Kanisa katika Kanisa la Mjini Kati.
Washarika hao wamemtaka Askofu Laizer kumfukuza kwanza kazi Karyongi, ambaye ndiye Mwenyekiti wa Bodi ya Hoteli ya Corridor Springs ndipo na yeye atafakari nafasi yake.
“Huu ni uzembe wa hali ya juu katika kusimamia mali zetu na hapa kuna mgongano wa kiuongozi kati ya Askofu na Katibu ambaye pia ni msimamizi wa mali zetu,” alidai msharika huyo.
Alituhumu uongozi wa Kanisa kwa kukiuka mkataba na benki iliyotoa mkopo ambao katika kipengele kimojawapo, unailazimisha kanisa kutumia benki hiyo peke yake katika kurejesha fedha zake, lakini viongozi wamefungua akaunti katika benki moja ya biashara ya nchi jirani yenye matawi yake nchini.
Akijibu tuhuma hizo, Karyongi alisema hakuna tishio la kukamatwa kwa mali za kanisa, lakini alikiri kanisa linadaiwa na benki Sh bilioni moja na si Sh bilioni 11 kama inavyodaiwa na deni hilo ni malimbikizo ya nyuma.
Aliwatupia lawama baadhi ya waumini akidai ndio wanaotaka kutumia mwanya huo kulivuruga kanisa hilo. Kuna watu huko mitaani wanataka kutumia waraka wa Askofu wa kuwachangisha washarika kuleta vurugu katika Dayosisi,” alisema na kuongeza:
“Lugha iliyotumika katika waraka tuliowasomea washarika imetafsiriwa vibaya, ni kweli tunadaiwa na benki ila tuliwahadharisha washarika ndio maana tulisema huenda vitu tulivyoweka dhamana vikakamatwa.”
Katibu huyo aliongeza kuwa deni pekee ambalo imelazimu kuomba michango ya waumini ni la hoteli na haihusiani na hospitali.
Pia alisema kukamatwa kwa mali za kanisa kwa sasa si jambo kubwa linaloweza kusababisha mgogoro katika dayosisi kama inavyodhaniwa na watu.
Kuhusu tishio la waumini kugoma kuchangia kulipa deni hilo, Karyongi alisema hakuna jambo kama hilo.
“Hizi ni mali zao, watagomaje? Mimi sina taarifa hizo na wakuu wa majimbo wako hapa hakuna anayejua kuhusu kugoma kwa waumini,” alisema.
Kuhusu kutakiwa kuachia nafasi zao ili kupisha uchunguzi, Karyongi alisema ni jambo lisilowezekana.“Askofu atatoa huduma mpaka mwaka 2016 na bado ana uwezo wa kufanya kazi zake kwa mujibu wa katiba yetu, hata mimi hakuna sababu, kwa nini nijiuzulu katika nafasi yangu?” Alihoji katibu huyo kwa lugha ya uchangamfu.
Wakati katibu huyo akijinasibu, taarifa zinadai kuwa huenda akachukuliwa hatua katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Dayosisi kilichotarajiwa kukutana jana jijini hapa.
Kwa mujibu wa chanzo chetu ndani ya kikao hicho pamoja na mambo mengine, uamuzi wa kuwachangisha washarika utajadiliwa na kama italazimika baadhi ya wakuu wa dayosisi watachukuliwa hatua.
“Tunasubiri kwa hamu kubwa taarifa ya Katibu na kuijadili kwa kina, endapo tutaona inafaa atalazimishwa kukaa kando,” alidai mtoa habari wetu. 

No comments: