MIZENGO PINDA AWASHUKIA WAKUU WA WILAYA MPYA...

Mizengo Pinda.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda amepiga marufuku wakuu wa wilaya mpya na watumishi wa Serikali walioajiriwa katika wilaya hizo, kuishi nje ya makao makuu ya wilaya hizo.
Amewataka waache kuishi katika makao makuu  ya mikoa, kwa visingizio  visivyo  na tija,  vikiwemo uhaba wa nyumba za watumishi.
Pinda alitoa  agizo hilo juzi mjini Inyonga katika makao  makuu  ya Wilaya mpya ya Mlele Mkoa wa Katavi. Alikuwa akihutubia mkutano  wa hadhara  baada ya kupewa taarifa, kwamba baadhi ya wakuu wa wilaya  mpya, wanaishi mijini, wakitoa kisingizio cha uhaba wa  nyumba  za  kuishi  watumishi.
“Naagiza wakuu wote wa wilaya  na watumishi katika wilaya mpya, zilizoanzishwa  kuishi katika  vituo  vyao  vya kazi na sio  kukaa mijini.
Kila mtu aende  kwenye  kituo chake cha kazi,  hata kama hakuna maji wala nishati ya umeme, kwa sababu akikaa mjini  lini  mtapata uchungu  na  kuhakikisha  vituo vya  kazi  vinapatiwa  huduma  hizo muhimu  za kijamii?” Alisema.  
Alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Mlele, Ngemela Lubinga kwa kuhamia na kuishi katika  makao  makuu ya  wilaya hiyo   licha ya kukabiliwa na  changamoto  nyingi  ikiwemo  uhaba mkubwa wa  nyumba za watumishi.
Aliuhakikishia  uongozi wa  Wilaya  hiyo mpya  ya Mlele   ili kukabiliana na uhaba huo wa nyumba  za watumishi, Shirika la
Nyumba (NHC)  linatarajia  kujenga  nyumba 250 mkoani Katavi,  ambapo kati ya hizo, 20  zitajengwa mjini Inyonga.
Katika hatua  nyingine, Pinda  alisema  kuwa  halmashauri za Nsimbo na Mlele zitaanzishwa hivi karibuni, hivyo wilaya hiyo kuwa na  halmashauri mbili  za kiutawala. Lengo la hatua hiyo ni   kusogeza  huduma  muhimu  za kijamii  karibu na wananchi.
Akitoa  sababu  za  kuanzishwa kwa  halmashauri  hizo, alisema ni kutokana na ukubwa  wa eneo la kilometa za mraba 26,000,
sawa na nchi jirani ya Burundi, yenye ukubwa  wa kilometa 27,000 za mraba.
Pia, aliahidi kutoa trekta moja kwa kikundi cha vijana katika Kata ya Ilunde ili waondokane na kilimo cha jembe la mkono na waboreshe uchumi wa eneo hilo.
Alitoa ahadi hiyo wakati akizungumza na wakazi wa Kijiji cha Ilunde kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Ilunde katika siku ya pili ya ziara yake jimboni kwake Katavi wilayani Mlele.
Pinda ambaye ni Mbunge wa Katavi alisema atawapatia
trekta hilo kama mkopo ili nao warudishe trekta jingine, likopeshwe kwa kikundi kingine.
“Hapa naanzisha ‘Kopa trekta lipa trekta’. Litakuja likiwa na majembe yake,” alisema Waziri Mkuu huku akishangiliwa.
“Ni lazima tuondokane na kilimo cha jembe la mkono kwa sababu hakina tija... na zaidi nasisitiza kuondokana na kilimo cha matuta kwa sababu kinatumia nguvu nyingi na kupoteza eneo kubwa ambalo lingetumika kupanda mazao,” alisisitiza.

No comments: