ALIYEDAIWA KUFUGA MISUKULE ANUSURIKA KUUAWA BUKOBA...

DC Bukoba, Zipora Pangani.
Milio ya mabomu ilitawala mji wa Bukoba juzi usiku baada ya baada ya redio moja ya kijamii, kueneza uvumi wa mwalimu mmoja wa Shule ya Msingi Kashai amekamatwa akiwa na misukule.
Taarifa hizo zilihamasisha mamia ya wananchi kuzingira Mtaa wa National Housing usiku huo, wakitaka kuteketeza nyumba ya mtuhumiwa, hali iliyolifanya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kagera kuimarisha ulinzi mtaani hapo.
Pia askari polisi waliojihami na silaha wakishirikiana na mgambo, walifunga njia zinazoingia katika mtaa huo huku wananchi wakikaidi kuondoka na kusababisha mabomu kufyatuliwa kwa nia ya kuwatawanya.
Polisi limeitupia lawama redio hiyo, kwa kueneza uvumi uliosababisha itumie nguvu kubwa kuwadhibiti wananchi waliokuwa na hasira kwa kufyatua mabomu, na risasi hewani usiku kutawanya mamia ya wananchi, waliokusanyika kwa lengo la kumdhuru mtuhumiwa na kuteketeza nyumba yake.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Richard Ngole, mtuhumiwa Bernadetha Katabarwa alitembelewa na mdogo wake, Benedikta Bukende akiwa na watoto wake wawili, akitokea kwenye maziko ya mumewe katika kijiji cha Bushagara, kitongoji cha Kizigo wilayani Muleba.
Ngole alisema pia Bukende baada ya kuondoka na watoto hao na kwenda kwa dada yake baada ya shughuli za msiba, ndugu wa marehemu walitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Kamachumu kuwa watoto Denis Bukende na Gloria Bukende, walichukuliwa kwa shughuli za ushirikina na kupelekwa mjini Bukoba.
Polisi wa Kamachumu, Sajini Wilbart akiongozana na ndugu wa marehemu, juzi, alisema  walifika Shule ya Msingi Kashai ambako walimkuta mwalimu anayetuhumiwa na kukiri kuwa watoto hao walikuja kumtembelea na walikuwa nyumbani pamoja na mama yao.
Alisema baada ya kufanyika mazungumzo shuleni Kashai, walikubaliana kuwa awapeleke nyumbani ili ndugu hao waondoke kurudi Kamachumu wakiwa na watoto pamoja na mama yao.
Hata hivyo, wakati wa harakati za kuwachukua watoto hao pamoja na mama yao, mamia ya wananchi walianza kukusanyika, wakihamasishwa na taarifa zilizokuwa zikivumishwa kwenye redio moja ya kijamii ya hapa  kuwa kuna mwalimu aliyekamatwa na idadi kubwa ya misukule nyumbani kwake.
Baada ya ndugu kuondoka na watoto hao wakiwa na mama yao kwenda Kamachumu, mtuhumiwa aliokolewa na askari Polisi huku nyumba yake ikiwa imeanza kuteketezwa ambako Kikosi cha Zimamoto kilifika na kuzima moto huo huku polisi wakifunga njia zote zinazoingia katika mtaa huo.
“Askari wamelala kwa ajili ya ulinzi wa nyumba. Leo (jana) asubuhi wananchi wameanza kurusha mawe, tumemwomba Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Kamati ya Ulinzi na Usalama itumike, isionekane amani inakuwepo kwa sababu ya Polisi,” alisema Kaimu Kamanda.
Aidha, Kamanda huyo alisema jana asubuhi Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Zipora Pangani, alipokwenda katika mtaa huo uliokuwa bado umezingirwa na wananchi wenye hasira, alishindwa kuendelea kuzungumza na kulazimika kuondoka baada ya kuanza kuvurumishiwa mawe.
 “Tukio hili lina mwendelezo kutoka Kamachumu wilayani Muleba, Mkuu wa Wilaya alipofika asubuhi amerushiwa mawe hata OCD wetu amepigwa mawe,” alisema Ngole.
Pamoja na Jeshi la Polisi kupiga kambi katika mtaa huo hadi jana asubuhi, vurugu ziliendelea katika mtaa huo huku polisi wakilipua mabomu kadhaa, na kwamba wanawashikilia watu zaidi ya 10.
Limesema mwanamke aliyefiwa na mumewe alikuwa akiishi Dar es Salaam na alikwenda Kamachumu kumzika mumewe, na kabla ya kurudi, alifika Bukoba kumsalimia dada yake akiwa na watoto wake.

No comments: