RAIS KIKWETE AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA DARAJA LA KIGAMBONI...

Muonekano wa daraja la kisasa la Kigamboni utakapokamilika ujenzi wake mwaka 2015.
Rais Jakaya Kikwete amekanusha uvumi wa wanasiasa kwamba amemwuzia Rais mstaafu wa Marekani, George W. Bush eneo la Kigamboni na kuwataka Watanzania kuwa makini na wanasiasa wa aina hiyo ambao kazi yao ni kueneza uongo.
Pia amewaondoa wasiwasi wananchi na kuwaahidi kwamba ahadi zote alizotoa wakati wa kampeni mwaka 2010 na zilizo kwenye Ilani ya CCM, ziliwekwa kwa malengo na wataalamu hivyo lazima zitatekelezwa kabla hajamaliza muda wake mwaka 2015.
Akiweka jiwe la msingi ikiwa ni ishara ya kuanza ujenzi wa Daraja la Kigamboni Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema baada ya baadhi ya wanasiasa kuona mpango wa kuboresha Kigamboni na kuufanya mji wa kisasa, wameamua kuzusha uongo huo ambao hauna ukweli.
"Najua kuna uongo mwingi unaozushwa mitaani, eti mimi nimeuza Kigamboni kwa Bush, sasa nashangaa jamani Bush Kigamboni afuate nini au ndio huo uzushi wa kuwapo mafuta?" Alihoji Kikwete.
Aliwahadharisha wananchi kujiepusha na waongo ambao aliwaita wana viwanda vya kuzalisha uongo na kubeza maendeleo ya nchi, hata kama maendeleo hayo yanapaswa kupongezwa kwa kuwa tu ni wapinzani.
"Muwe makini, watu kama hawa hawapendi maendeleo ya nchi yetu wala kuyafurahia, sitoshangaa kusikia wamebeza hata ujenzi wa Daraja hili la Kigamboni, ili mradi tu waoneshe upinzani, watu wa aina hii hawajui dhamana ya vyama vya siasa na wala hawana dira," alisema.
Alitaka wanasiasa nchini pamoja na vyombo vya habari kuweka mambo mema ya nchi mbele na kuondokana na dhana ya kubeza kila kitu kwa hofu ya kuisifia CCM. "Ila nawaambia wana bahati mbaya pamoja na kubeza kwao, wataumiza vijiba vyao vya roho kwa kuwa tutashinda kwa maendeleo," alisema.
Aliongeza kuwa Serikali ilianzisha mpango wa mji wa kisasa Kigamboni, ikiwa ni mkakati wa kujenga miji ya pembeni itakayokuwa na huduma zote kwa wakazi wake ili kupunguza msongamano katikati ya majiji nchini.
Alisema kupitia mkakati huo wanatarajia mji mmoja ukijengwa uwe na kila kitu kuanzia shule, masuala ya afya, benki hadi ofisi na hadi sasa Kigamboni na Mabwepande, ndio maeneo ambayo mkakati huo utaanza kutekelezwa. "Yaani lengo letu mtu akija Posta basi aje kutembea au ameikumbuka sana Kariakoo na si kuja kutafuta huduma za kibenki au afya," alisema.
Kuhusu utekelezaji wa ahadi, Rais Kikwete alisisitiza kuwa kila kilichomo kwenye Ilani ya CCM lazima kitekelezwe, kwa kuwa ahadi hizo zilifanyiwa tathmini na kuandaliwa na wataalamu ambapo alitoa mfano wa ahadi ambazo tayari zimetekelezwa kama vile ujenzi wa shule za kata, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Daraja la Kigamboni.
"Najua wenzetu haya yanawaudhi sijapata kuona, wanatamani hata daraja hili lisijengwe, bahati mbaya watapata tabu, najua yapo mengi tumeahidi lakini tutayashughulikia," alisema.
Pamoja na hayo, Rais Kikwete alisema Serikali yake inafahamu kuwa barabara ndio mishipa ya fahamu ya nchi, hivyo inajitahidi kujenga barabara za kutosha na kwa sasa inaongeza barabara za kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam ambako kwa sasa kuna barabara moja pekee.
Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli, alilishukuru Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia miradi mbalimbali ya maendeleo nchini na kumtaka Rais Kikwete angalau amtunukie nishani Mkurugenzi wa NSSF, Ramadhan Dau kwa kazi anayofanya.
"Bahati mbaya mheshimiwa umekuwa ukitoa nishani kwa wanajeshi tu, hata mawaziri au wakurugenzi wanaofanya vizuri nao wanastahili nishani, tafuta basi hata ya kiaina umpe Dau, ameonesha mfano katika maendeleo ya nchi," alisema.
Aidha, alisema kama ilivyo katika barabara kwa upande wa madaraja hadi sasa madaraja makubwa na madogo 4,880 huku mengine mengi yakiwa kwenye mchakato wa ujenzi ambapo katika ujenzi wa Daraja la Kigamboni aliwahadharisha wakazi wa Kigamboni kutotumia daraja hilo kama sehemu ya utalii au harusi.
Dau alisema daraja hilo litakalogharimu Sh bilioni 214.6 ni la kuning’inia lenye urefu wa meta 680 ambapo NSSF itagharimia asilimia 60 na Serikali asilimia 40 pamoja na malipo ya fidia kwa wananchi watakaoathirika na ujenzi huo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale alisema daraja hilo litakuwa na njia sita, tatu kila upande. Upande wa Kurasini litaunganishwa na barabara ya Nelson Mandela kupitia barabara ya juu eneo la Tazara kilometa moja kutoka usawa wa daraja kwenda Ubungo.
Alisema magari yatakayopita kwenye daraja hilo linalotarajiwa kukamilika Machi 2015, yatalazimika kulipia lakini waenda kwa miguu na waendesha baiskeli watapita bure.
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka alisema wizara yake inatarajia ujenzi wa daraja hilo utazalisha ajira takribani 3,000 za moja kwa moja na ambazo si za moja kwa moja na kuwataka vijana kuchangamkia fursa hiyo.
Alisema NSSF imekuwa ikiwekeza katika miradi mbalimbali ikiwa ni juhudi za kuboresha mafao ya wafanyakazi ambapo baada ya ujenzi wa nyumba za bei nafuu Kigamboni, sasa inatarajiwa kujenga barabara ya Chalinze- Bagamoyo na iko mbioni kujenga kiwanda cha mbolea cha kutumia gesi.

No comments: