MUFTI SIMBA ASEMA PONDA NA WENZAKE NI WAHUNI...

Mufti Issa Shaaban Simba (kushoto) akiongea na waandishi wa habari.
Mufti Simba awaita Ponda na wenzake ni wahuni
Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa bin Shaaban Simba, ametaka Waislamu nchini kupuuza baadhi ya watu aliowaita ‘genge la wahuni’ wanaoendesha chokochoko za kutaka kumng’oa madarakani, huku akivitaka vyombo vya Dola kuchukua hatua kali dhidi yao.
Aidha, amesema mkutano uliopangwa kufanywa leo na kikundi hicho kupinga filamu inayotajwa kumdhalilisha Mtume Muhammad (S.AW), hauna tija kwa vile tayari Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), limeshazungumzia suala hilo na kumwandikia barua Rais wa Marekani, Barack Obama kulaani filamu hiyo.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Shekhe Simba alisema kikundi hicho kinachojitambulisha kama Jumuiya na Taasisi za Kiislamu chini ya uongozi wa Shekhe Ponda Issa Ponda, kimejivika vazi la kuendesha wanachokiita harakati za Kiislamu na hakitaki kufuata utaratibu wowote wa dini na mamlaka za Dola.
"Hiki si kikundi kinachowakilisha Waislamu wote wa nchi hii, bali ni kigenge cha watu wachache wenye kufuata madhehebu ya Mawahabi ambao kwa mujibu wa itikadi yao, wanaamini kwamba Mwislamu yeyote asiyefuata itikadi yao, si Mwislamu na hafai kuwa kiongozi wa ngazi yoyote," alisema Mufti.
Alisema vurugu za kikundi hicho hazikuanzia Bakwata, kimekuwa kikifanya hivyo sehemu mbalimbali mikoani, kwa kuvamia na kuteka misikiti na kuondoa viongozi waliochaguliwa kihalali na hatimaye kupora na kuhodhi rasilimali za misikiti hiyo.
"Nikiwa Kiongozi Mkuu wa Waislamu katika nchi hii, nawataka Waislamu wa Tanzania kutambua kuwa vitendo vya vurugu na ghasia na uvunjaji wa sheria vinavyofanywa na Ponda na kikundi chake, kamwe havina uhusiano wowote na dini ya Kiislamu.
"Ni vitendo vinavyokiuka maadili ya Uislamu na kuupa sura mbaya miongoni mwa jamii na mataifa mbalimbali, hivyo nawahadharisha Waislamu wa madhehebu yote kujitenga na matendo ya uvunjaji wa sheria wa kikundi hiki cha watu wachache," alisisitiza Mufti.
Pamoja na hilo, alisema Waislamu wako tayari kuilinda Bakwata kwa nguvu zote dhidi ya watu wanaotaka kuivamia na kuonya waliopanga kufanya uvamizi huo.
Akizungumzia kauli ya Ponda aliyetaka kuwapo ukomo wa nafasi ya Mufti, Shekhe Mkuu alisema kanuni na taratibu za dini hiyo tangu enzi za Mtume Muhammad (S.A.W.), hakuna utaratibu wa uchaguzi wa viongozi wa ngazi hiyo kama ilivyo katika nafasi zingine ndani ya Bakwata.
Aidha, alivipongeza vyombo vya Dola na Serikali kwa namna vilivyoshughulikia ghasia za kikundi hicho kwa busara, hekima na subira katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, huku akivitaka kuangalia utaratibu wa kushughulikia watu wanaoleta vurugu kwa kujifanya viongozi wa taasisi mbalimbali.
Shekhe Ponda akijibu alisema kauli za Mufti dhidi ya kikundi hicho hazina ukweli wowote na zimepanga kuficha ukweli unaomhusu, kuwa kiongozi huyo si mwadilifu katika nafasi yake.
Alisema baadaye mwezi huu wanatarajia kufanya mkutano mkubwa wa Waislamu nchi nzima, wenye lengo la kuwaeleza matatizo yaliyo nchini ya uongozi wa sasa wa Bakwata.
Kuhusu mkutano uliopangwa kufanywa leo kulaani filamu inayomdhalilisha Mtume, Ponda alisema utafanywa kama ilivyokusudiwa, ili kuieleza dunia ni namna gani suala hilo lilivyokera Waislamu.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alisema wajibu wa Jeshi hilo utaendelea kubaki palepale kwa kulinda utaratibu wowote uliopo kisheria.
Alisema vitendo vya uvunjifu wa amani likiwamo suala la kutaka kumng’oa Mufti bila utaratibu, halitavumiliwa, kwani polisi wamejipanga kupambana na watakaothubutu kufanya vurugu hiyo.

No comments: