JUU: Jumba ambalo lilinadiwa baada ya Evander kushindwa kulipa mkopo wa benki. JUU KULIA: Evander Holyfield. CHINI: Evander na mkewe, Janice. CHINI KULIA: Binti yake, Emani.
Bingwa wa zamani wa ndondi za uzito wa juu duniani, Evander Holyfield amejikuta kwa mara nyingine kwenye matatizo baada ya kupandishwa mahakamani kwa madai ya kushindwa kulipa zaidi ya Dola za Marekani 500,000 kwa ajili ya matunzo ya mtoto.Idara ya Huduma za Jamii ya Georgia ilifungua mashitaka dhidi ya mwanamasumbwi huyo mstaafu kwa niaba ya binti yake mwenye miaka 18, Emani, ambaye alikuwa akimdai karibu Dola za Marekani 373,000 kwa ajili ya matunzo.
Lakini kwa mujibu wa nyaraka za mahakama zilizopatikana, kiasi hicho kimeongezeka hadi kufikia karibu Dola za Marekani 564,000. Baada ya kufikishwa mbele ya Jaji wa Georgia, bondia huyo mwenye miaka 49 aliamriwa mara moja kuanza kulipa Dola za Marekani 2,950 kwa mwezi.
Katika kutekeleza hukumu hiyo, Evander alilipa papo hapo kiasi cha Dola za Marekani 17,700, na kufanikiwa kupunguza kiasi anachodaiwa hadi kufikia Dola za Marekani 546,201.
Lakini huo si mwisho wa matatizo ya Evander. Kwa mujibu wa ripoti, Jaji pia aliamuru kuwa asilimia fulani kutoka chanzo kikubwa cha mapato ya bondia huyo kidhibitiwe ili kulipia deni hilo.
Hili ni sakata la hivi karibuni kabisa katika milolongo la matatizo ya kifedha yanayomkabili bondia huyo ambaye alijizolea umaarufu kutokana na tukio la kunyofolewa kipande cha sikio katika pambano lake dhidi ya Mike Tyson mwaka 1997.
Matatizo ya Evander yalianza mwaka 1999 wakati mke wake aliyedumu naye kwa miaka miwili, Janice, alipofungua madai ya talaka baada ya bingwa huyo wa uzito wa juu kukiri hadharani kwamba alizaa watoto wawili nje ya ndoa yao, kwa mujibu wa taarifa kutoka Houston Press.
Kwa ujumla, Evander ambaye alitalikiwa mara tatu ana watoto takribani 12 kutoka kwa wanawake sita tofauti, akiwamo mtoto wa kiume aliyezaa na Janice.
Mwaka 2008, bondia huyo ambaye anamiliki mali inayokadiriwa kufikia Dola za Marekani milioni 250 kutokana na maisha yake ya ndondi, alitangaza kufilisika mjini Georgia.
Miaka miwili baadaye, Janice Holyfield alifungua madai katika mahakama ya Texas akidai kupatiwa Dola za Marekani 280,000 kwa ajili ya gharama za matunzo ya mtoto na riba kutoka kwa mume wake huyo wa zamani mzinifu.
Julai mwaka huu, mpiganaji huyo mkongwe, alitimuliwa kutoka kwenye jumba lake lenye ukubwa wa futi za mraba 54,000, vyumba 109 lililoko huko kusini mwa Atlanta baada ya kushindwa kulipa mkopo kwa kampuni ya JP Morgan Chase aliyosaini nayo mkataba, ambapo baadaye lilipigwa mnada na kuuzwa kwa Dola za Marekani milioni 7.5.
Kwa mujibu wa gazeti la Florida Times-Union, Evander hakuwa na uwezo wa kulipa Dola za Marekani milioni 14 za malipo ya mkopo wa nyumba alizokopa benki.
No comments:
Post a Comment