YASEMAVYO MAGAZETI YA LEO...

                   HABARI ILIYOSISIMUA                                          
Mchungaji Ambilikile Mwasapila akijaza dawa kwenye vikombe kijijini kwake Loliondo.
IDADI kubwa ya wagonjwa waliokwenda kutafuta tiba kwa Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwaisapile, Loliondo wamepoteza maisha.
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambayo sasa itatangaza matokeo ya utafiti wa tiba hiyo ya ‘Kikombe cha Babu’ imesema wengi ni wale wenye Ukimwi walioacha matumizi ya dawa za kurefusha maisha (ARVs).
Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya  na Ustawi wa Jamii, Regina Kikuli, aliiambia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali  (PAC) jana Dar es Salaam, kwamba hadi sasa Serikali inafanyia utafiti watu 206 ambao walipata kikombe hicho.
Utafiti unaofanywa na Wizara hiyo inataka kubaini kama kweli dawa hiyo ina uwezo wa kuponya Ukimwi, kisukari, saratani  na magonjwa mengine sugu.
Wanaofanyiwa utafiti huo walipata ‘kikombe’ hicho baada ya kuugua kisukari na Ukimwi. “Kwa sasa ni vigumu kusema dawa hiyo inaponya au haiponyi, tusubiri utafiti wa kitaalamu.
“Baada ya miezi miwili tutatangaza matokeo kwa umma,” alisema Kikuli na kuongeza kuwa utafiti huo unafanywa katika hospitali mbalimbali nchini chini ya usimamizi wa Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR).
-HABARILEO, Aprili 5, 2012

No comments: