DARAJA REFU ZAIDI DUNIANI SASA LAKAMILIKA...

Kazi ya ujenzi wa daraja la Anzhaite ilianza rasmi Oktoba, 2007 na sehemu kubwa ya ujenzi hiyo ikikamilika mwishoni mwa mwaka jana.
Daraja hilo lenye kimo cha futi 1,102 na urefu wa futi 3,858, ndilo daraja refu zaidi duniani kwa sasa.
Ujenzi wake umekusudia kupunguza msongamano wa magari eneo la Jishou katika kitongoji cha Hunan na lilitarajiwa kufunguliwa rasmi jana kwa ajili ya waendesha magari.
Madereva wanaweza kuona mandhari nzuri ya Dehang wakati wakikatiza urefu wa futi 3,858 wa barabara ya angani inayounganisha vilele viwili vya milima.
Daraja hilo, ambalo linaangazwa kwa taa 1,888 wakati wa usiku, ni la nne linalokatiza juu ya ziwa na kuonekana kuunganisha vilele viwili vya milima.
Kwa wakati mmoja kwenye daraja hilo, magari madogo na malori yanaweza kupita kwenye barabara mbili zenye kuchukua mistari minne ya magari upande mmoja na kwenda kwa spidi ya takribani kilomita 50 kwa saa.
Waenda kwa miguu nao pia wanaweza kutembea sambamba kwenye njia maalumu chini ya barabara.
Daraja hilo ni sehemu muhimu kwa Barabara kuu ya Jishou-Chadong, yenye kilomita 64 ambayo ina mahandaki 18 tofauti ambayo yanafikia nusu ya umbali wake.
Inaaminika kuwa daraja hilo litasaidia sana kupunguza msongamano wa magari ambao umekithiri sehemu za milimani ambazo zina barabara nyembamba zenye miteremko mikali.
Daraja limeshikiliwa kwenye msingi wenye upana wa futi 78.
Kabla ya daraja hili, China pia ndio ilikuwa ikishikilia rekodi ya kuwa na  daraja refu zaidi duniani la Danyang Kunshan Grand ambalo lina umbali wa maili 100 lililojengwa miaka miwili iliyopita kwa ajili ya treni za umeme inayounganisha miji ya Beijing na Shanghai.

No comments: