TAKUKURU SASA KUDHIBITI MIAMALA YA SIMU ZA WAGOMBEA MAJIMBONI

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inatarajia kusambaza vijana wa kazi katika majimbo yote nchini, kuwashughulikia wote walioonesha nia ya kugombea nafasi mbalimbali za uchaguzi, ambao wanatoa rushwa ili kupata wafuasi.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Dk Edward Hosea,  alisema hayo jana alipokuwa akijibu agizo alilopewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika katika semina ya wabunge wa Mtandao wa Wabunge wa Afrika wa Kupambana na Rushwa (APNAC), tawi la Tanzania.
Mkuchika alimtaka Dk Hosea asisubiri kipenga cha kampeni kuanza, bali asambaze vijana wake kwenye majimbo ya uchaguzi  kwani viashiria vya rushwa vimeshaanza.
“Kazi imeanza, waambie vijana wako wasisubiri Oktoba, waanze kazi sasa maana kuna viashiria vya rushwa, waingie wafanye kazi,” alisema Mkuchika.
Alisema semina hiyo imekuja wakati mzuri wanapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu Oktoba mwaka huu, hivyo ni vyema wabunge wakumbuke wana wajibu wa kulinda maadili na kuepuka vitendo vya rushwa.
Akijibu hoja mbalimbali za wabunge baada ya kuwasilisha mada ya rushwa na uchaguzi, Dk Hosea alizungumzia  hatua zitakazochukuliwa na Takukuru kwa watoa rushwa kupitia njia ya mtandao, ambapo alisema kwa uchaguzi huu ni vyema watoa rushwa kwa njia hiyo waache.
Katika swali lake, Mbunge wa Nkasi, Ali Keissy (CCM), alihoji njia zitakazotumika kubaini wanaotumia njia ya mtandao kutoa rushwa, ambapo Dk Hosea alisema wanajua hilo na watalifuatilia kwa kuwa wana uwezo wa kufanya hivyo.
Dk Hosea alisema miamala yote inayofanywa na wagombea itafuatiliwa na kutoa rai kwa wagombea kuacha kutoa rushwa, kwani watakaobainika sheria itachukua mkondo wake.
“Nyie mnaotumia mitandao ya simu kutoa rushwa,  mwaka huu mtaumia vibaya acheni, tuna uwezo wa kudhibiti vitendo hivyo, tumesomesha vijana wetu na tuna vifaa vya kufuatilia,” alisisitiza Dk Hosea.
Alisema uchaguzi wa mwaka huu utakuwa tofauti na wa mwaka 2010, kwani wamejipanga vizuri kuhakikisha vitendo vya rushwa vinadhibitiwa.
Moja ya mbinu zitakazotumika kwa mujibu wa Dk Hosea, ni kubadilisha magari yao yanayotumika kwenye uchunguzi kwa kuwa yaliyopo yameshazoeleka.
“Niwaambie tu tutatumia magari mengine maana haya ya sasa mmeyazoea, mnayajua  na wengine walinunua yanayofanana ili iwe rahisi kwao kutoa rushwa wakiwa ndani…sasa watu hawatayatambua kama ni ya kwetu au la,” alisema Dk Hosea.
Akijibu swali la Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka (CCM), aliyehoji kusafishwa kwa baadhi ya watuhumiwa wa sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow kama hakuharibu uchunguzi wa Takukuru, Dk Hosea alisema hakuna kilichoharibika.
“Sisi hatusafishi mtu na mafaili yetu hatujayafunga na wala hatuna mpango wa kuyafunga, tunafanya kazi kwa mujibu wa sheria na kazi yetu ya kuwachunguza inaendelea na tukimaliza tutakabidhi kwa mamlaka nyingine,” alisema Dk Hosea.
Alisema kusafishwa kwa baadhi ya watuhumiwa wa tukio hilo hakujaharibu uchunguzi wao na kwamba wao wanaendelea na kazi yao na hakuna aliyewaingilia kwenye kazi yao, hivyo watahakikisha wanaikamilisha.
Akijibu hoja ya Mbunge wa Viti Maalumu, Assumpta Mshana (CCM), aliyehoji kwa nini Takukuru isiwahamishe maofisa wake waliokaa muda mrefu kwenye eneo moja la kazi kutokana na wao kuzoeleka eneo hilo, Dk Hosea alisema jambo hilo linafanyika na ofisi hiyo ndiyo inayoongoza kwa uhamisho wa vituo vya kazi vya watumishi.
“Tunafanya hilo, na sisi ndio ofisi inayoongoza kwa kuhamisha watumishi vituo vya kazi, ila nayo ni gharama kubwa, kuanzia Januari mwaka huu hadi sasa tumeshatumia Sh bilioni moja  kuhamisha watumishi vituo vya kazi,” alisema Dk  Hosea.
Alifafanua kuwa mtumishi mmoja anahamishwa kwa Sh milioni saba na uhamisho ni sehemu ya kipaumbele kwao ili wasizoeleke sehemu moja, lakini tatizo kubwa ni ufinyu wa bajeti.
Akijibu hoja ya mbunge wa Nyamagana, Ezekiel Wenje (Chadema) na Mbunge wa Kibondo, Felix Mkosamali (NCCR-Mageuzi), waliyehoji tangu kuanza kutumika kwa Sheria ya Gharama ya Uchaguzi mwaka 2010, ni watuhumiwa wangapi wameshafikishwa mahakamani, Dk Hosea alisema watuhumiwa 24, wameshapelekwa mahakamani.
Alisisitiza kuwa  katika sheria hiyo wenye jukumu la kufahamu gharama halisi ya uchaguzi zilizotumika kwa mgombea au chama ni la Msajili wa Vyama vya Siasa  pamoja na Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) na sio Takukuru kwani kazi yao ni kuchunguza masuala la rushwa na kuchukua hatua.
“Kama mgombea atasema kiasi tofauti na kile halisi cha gharama ya uchaguzi alichotumia, mwenye wajibu wa kufuatilia hilo ni CAG na Msajili wa Vyama vya Siasa, sisi tunafuatilia masuala yanayohusu rushwa,” alisema Dk Hosea.
Awali akiwasilisha mada kuhusu Rushwa, Uchaguzi na Maadili, Dk Hosea alisema sababu za wagombea kutoa rushwa ni nyingi ikiwemo kutojiamini kwa wagombea, hofu ya kushindwa  na kuwa na malengo  na maslahi binafsi.
Alisema katika uchaguzi huu sheria zote za uchaguzi zitatumika sambamba, ikiwa ni pamoja na Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010 ambayo inataka vyombo vya moto  vya chama lazima visajiliwe kwa majina ya chama.
“Mwaka huu tutawakamata wengi, kama chombo cha moto ni cha chama ni lazima kisajiliwe kwa jina la chama na si jina la mtendaji mmoja mmoja wa chama (kiongozi), kadhalika fedha kama una marafiki wa chama fedha zitumwe kwenye akaunti ya chama na si ya mtu binafsi,” alisisitiza Dk Hosea.
“Ningekuwa mimi msajili wa vyama ningeanza na hili la kuwa na akaunti maalumu ya chama sio fedha za chama zinaingia kwenye akaunti ya kiongozi wa chama, tena fedha za kusaidia chama kwenye kampeni ni lazima  chama kiseme wamepewa na nani na kiasi gani,”alisema Dk Hosea.
Alisisitiza kwa wabunge kuwa makini na kusoma sheria zote za uchaguzi ili wazielewe na kuzifuata pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa kwani kutoa rushwa kosa na kunafanya kupatikana kwa viongozi wasio na sifa za uongozi wala uzalendo.

No comments: