Siku chache
baada ya Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta kutaka uangaliwe uwezekano wa
kushusha nauli za vyombo vya usafiri nchini, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa
Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imesema inatekeleza agizo hilo na kwamba nauli za
daladala na mabasi ya mikoani zitashuka wakati wowote kuanzia sasa.
Imeongeza
kuwa, licha ya bei ya mafuta kupanda kidogo jana, hakutaathiri kushuka kwa
nauli, kwani ukokotoaji utafanyika kwa wastani wa bei ya mafuta ilivyoshuka
kwani haitapanda kwa kiasi kikubwa kwa mara moja.
Hayo
yalisemwa jana na Meneja Mawasiliano wa Mamlaka hiyo, David Mziray aliyesema
wanatekeleza agizo la Waziri Sitta aliyetaka nauli zishuke kufikia kesho,
lakini wamechelewa kutokana na muda wa kuwasilisha maoni kwa wadau waliopewa
siku 14 kufikia ukomo leo.
“Tunawahakikishia
wananchi kuwa baada ya kumaliza siku za kupokea maoni ya wadau hususan wamiliki
wa mabasi ya daladala waliopewa siku 14, mchakato huu utakwenda haraka na
mapema iwezekanavyo tutatangaza nauli hizo mpya,” alisema.
Mziray
alisisitiza kuwa hakuna sababu ya kutoshusha nauli, bali wanafuata taratibu na
kanuni hivyo kuwataka wananchi kuwa na subira kwa siku chache zijazo.
Wiki hii,
Waziri Sitta aliwataka Sumatra kuharakisha mchakato huo wa kushusha nauli
ufanyike haraka iwezekanavyo na ifikapo
kesho wawe wametangaza nauli hizo mpya, kwani kwa muda mrefu bei za mafuta
zimeshuka kutoka zaidi ya sh 2,200 hadi chini ya Sh 1,800.
Awali,
wadau wa usafiri walipendekeza kupunguzwa kwa nauli za mabasi yaendayo mikoani
kwa viwango vya kati ya asilimia 15 na 25 huku wakitaka nauli za daladala
zipungue kutoka Sh 400 hadi Sh 300 kwa njia ya umbali wa kilometa 10.
Walitaka
kwa mabasi ya kawaida kwa Moshi na Arusha (Sh 17,000 badala ya Sh 22,700),
Mwanza (Sh 32,369 badala ya Sh 42,000), Mbeya (Sh 23,365) badala ya Sh 30,700),
Bukoba (Sh 40,756 badala ya Sh 55,000) na Dodoma (Sh 12,678 badala ya Sh
16,700).
Katika usafiri
wa daladala wamesema wanataka iwe Sh 300 kwa kilometa kuwa Sh 31.39 kwa usafiri
wa kilometa 10 badala ya Sh 400 na kilometa 15 iwe Sh 450 na maeneo mengine
kupungua kwa Sh 100.
No comments:
Post a Comment