Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu
imependekeza kwa Serikali iongeze adhabu ya faini kutoka Sh milioni tatu na
kifungo kisichopungua miezi sita na kuwa faini ya Sh milioni tano na kifungo
kisichopungua miezi sita kwa wale wote watakaotuma katika mtandao taarifa za
uongo.
Aidha, kamati hiyo imependekeza
katika adhabu kwa watu wanaonyanyasa wenzao kupitia mtandaoni, adhabu yao
iongezwe kutoka kifungo cha mwaka mmoja na kuwa kifungo cha miaka mitano.
Akiwasilisha maoni ya Kamati hiyo
kuhusu Muswada wa Sheria ya Uhalifu wa Mtando wa mwaka 2015, Mwenyekiti wa
kamati hiyo, Peter Serukamba alisema adhabu zilizowekwa katika sheria hiyo
hazitoshelezi kulingana na athari za makosa hayo.
“Kamati imeona umuhimu wa kuongeza
adhabu hizi katika maeneo haya, kutokana na ukweli kuwa kumekuwa na wimbi kubwa
la watu wanaodhalilisha utu wa watu wengine katika mitandao ya kompyuta jambo
lililoathiri watu wengi, familia, jamii na nchi kwa ujumla,” alisema Serukamba.
Alisema kamati hiyo, pia inashauri
uwekwe utaratibu wa Serikali kuchukua hatua za ufuatiliaji kabla ya mtu
aliyenyanyaswa kuripoti. “Hii ihusishe mfumo wa kuweza kumtambua mtu
aliyesambaza picha ama taarifa hizo.”
Awali akiwasilisha maelezo ya
muswada huo, Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame
Mbarawa, alisema kutokana na kukua kwa
matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), kumesababisha kuwepo
kwa changamoto mbalimbali ikiwemo kuibuka kwa makosa ya mtandao.
Alitaja makosa ya mtandao
yaliyokithiri kwa sasa kuwa ni makosa dhidi ya faragha, usalama na upatikanaji
wa taarifa za kompyuta na mifumo ya kompyutam makosa yanayohusu maudhui, makosa
dhidi ya mifumo ya kompyuta na makosa ya kawaida yanayofanywa kwa kutumia
mitandao.
Alisema waathirika na waathirika
wa makosa hayo ni pamoja na Serikali, sekta binafsi, watu binafsi na jamii kwa
ujumla na takwimu kutoka jeshi la polisi zinaonesha kuwa makosa ya uhalifu wa
mtandao yaliyoripotiwa na kuchunguzwa kati ya mwaka 2012 hadi Agosti mwaka jana
ni 400.
Alisema katika kipindi cha mwaka
2010 hadi mwaka 2013, makosa ya uhalifu wa mitandao yalisababisha hasara ya
zaidi ya Sh bilioni 9.8 kwenye taasisi za fedha pekee.
Pia alisema kitengo cha kudhibiti
makosa ya uhalifu wa mtandao kiliripoti kukamatwa kwa watu zaidi ya 500
wakiwemo raia wa kigeni kwa makosa hayo
ya uhalifu wa mtandao.
Alisema sheria hiyo, inapendekeza
kuweka utaratibu wa kuzuia na kudhibiti uhalifu wa mitandao, kuainisha makosa
na adhabu dhidi ya uhalifu wa mtandao, kuainisha kanuni na taratibu za
upelelezi na uendeshaji wa mashaka ya makosa ya uhalifu wa mtandao na kuweka
utaratibu wa ukusanyaji wa vielelezo, ushahidi na kumbukumbu za makosa ya
halifu huo wa mtandao.
Sheria hiyo katika eneo la adhabu
kwa wahalifu wa mtandao pamoja na wasambazaji wa picha za utupu na ngono,
wasambazaji wa taarifa za uongo, za kibaguzi na matusi na watu wengine
wanaofanya udanganyifu unaohusu kompyuta, adhabu ni kwenda jela hadi miaka 10
au kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50.
Katika sheria hiyo, pia mtu
atakayesambaza ponografia ya watoto kupitia mtandao wa kompyuta atawajibika
kulipa faini isiyopungua Sh milioni 50 au mara tatu ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria au
kifungo kisichopungua miaka saba jela au vyote kwa pamoja. Mkosaji pia
ataamriwa kumlipa mwathirika fidia.
No comments:
Post a Comment