YANGA YANUSA RAUNDI YA PILI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

Sahau kuhusu matokeo ya watani wa jadi Jumapili iliyopita ambayo Yanga ilifungwa bao 1-0 na Simba. Yanga imezinduka, na imejibu mapigo kwa ushindi mnono katika michuano ya kimataifa.

Wiki moja baada ya kipigo hicho, Yanga imeiangushia kipigo Platinum FC ya Zimbabwe cha mabao 5-1 katika mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyochezwa leo jioni kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kama Simba shujaa wao ni Emmanuel Okwi, basi shujaa wa Yanga ni Mrisho Ngasa. Winga huyu mwenye kasi, jana alitengeneza nafasi nyingi kwa wenzake kufunga, lakini mwenyewe akafunga mabao mawili kati ya hayo matano.
Ngasa alimtengenezea Amisi Tambwe bao la tatu huku mengine yakifungwa na Salum Telela na Haruna Niyonzima, kiungo wa Rwanda aliyekuwa nahodha jana badala ya Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye aliumia katika pambano la watani wa jadi na kulazimika kushonwa nyuzi saba juu kidogo ya jicho.
Kikosi cha Hans van Pluijm kilianza kuandika bao la kwanza katika dakika ya 32, likifungwa na kiungo mkabaji, Telela baada ya kupokea pasi nzuri ya Niyonzima na kuupitisha mpira juu ya kipa wa Platinum FC, Petros Mhari aliyekuwa ametoka langoni kwake kumkabili mfungaji.
Baada ya kupata bao hilo, Yanga ilichachamaa na dakika ya 42, Niyonzima aliifungia bao la pili akimalizia kazi nzuri ya Simon Msuva aliyepiga krosi iliyosababisha piga nikupige langoni mwa Platinum na mpira kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni kwa shuti la kiufundi la chinichini.
Lakini hata hivyo bao hilo lilidumu kwa dakika mbili tu kabla ya wageni kupata bao la kwanza dakika ya 45 likifungwa na kiungo Walter Musoma aliyefunga kwa mpira wa adhabu ndogo kutokana na Telela kufanya madhambi nje kidogo ya eneo la penalti na kufanya matokeo kuwa 2-1 hadi mapumziko.
Iliwachukua dakika moja baada ya mapumziko, Yanga kuandika bao la tatu mfungaji akiwa Tambwe aliyepokea krosi ya Ngasa, kabla ya Ngasa kufunga bao lake la kwanza dakika ya 56 akimalizia mpira uliopigwa na Telela.
Platinum ambao walionekana kupotezana kabisa uwanjani kutokana na mabao hayo kuingia mfululizo kitu kilichosababisha kipa wao Mhari kumfuata kocha wake Norman Mapeza ili abadilishe safu ya ulinzi ndipo alipotolewa Wellington Kamudyariwa na nafasi yake kuchukuliwa na Simon Shoko.
Katika dakika ya 64, nusura Platinum ijipatie bao la pili baada ya mfungaji wa bao lao la kwanza, Musoma kupiga mpira wa adhabu ndogo uliogonga mwamba wa pembeni na kurudi uwanjani na mabeki wa Yanga kuokoa.
Wakati mashabiki wakiamini matokeo yatabaki hivyo, Ngassa alifunga bao la tano katika dakika ya 90, safari hii akimalizia pasi nzuri iliyochongwa na Kaph Sherman aliyeingia katika dakika ya 68 kuchukua nafasi ya Msuva.
Awali kabla ya kupata mabao hayo, Yanga walipoteza nafasi tano za wazi katika dakika za 15, 17, 20 na 22 kupitia kwa washambuliaji wake Msuva, Ngassa, Tambwe na Niyonzima ambaye jana alionesha kiwango cha juu.
Yanga ilitinga hatua hiyo kwa kuwatoa BDF XI ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2 wakati Platinum ambayo sasa ina kibarua kizito kwao, iliitoa Sofapaka ya Kenya kwa jumla ya mabao 4-2.
Yanga: Ally Mustapha ‘Barthez,’ Juma Abdul/Hassan Dilunga, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Said Juma, Telela, Niyonzima, Tambwe, Ngassa na Msuva/Sherman.

No comments: