WANAJESHI WALIOHUKUMIWA KIFO WAKATA RUFAA


Wanajeshi wawili waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Swetu Fundikira ambaye ni mtoto wa ndugu wa marehemu Chifu Abdallah Fundikira, wamekata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Wanajeshi hao ambao ni ndugu , MT 75854 Koplo Ally Ngumbe wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kikosi cha Kunduchi na MT 85067 Koplo Mohamed Rashid (JKT Mbweni), wamewasilisha rufaa hiyo katika Mahakama ya Rufani.
Katika rufaa yao, wanajeshi hao wana hoja tatu wakipinga hukumu ya kunyongwa hadi kufa iliyotolewa Novemba 20, 2012 na Jaji Zainab Mruke wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Katika hoja zao, wanajeshi hao wanadai Jaji alikosea kisheria kutoa uamuzi kwa kutozingatia kanuni za kuthibitisha mashitaka pasipo kuacha shaka yoyote, ambalo ni jukumu la upande wa mashitaka.
Aidha, wanadai Jaji alikosea kisheria kwa kutoa hukumu inayoegemea ushahidi wa kimazingira, bila kuzingatia ushahidi wa utetezi wa wakata rufaa. Katika hoja nyingine wanadai alishindwa kuchanganua itirafu katika majina kwenye taarifa ya uchunguzi wa chanzo cha kifo.
Awali, wakati hukumu hiyo inatolewa walihukumiwa washtakiwa watatu akiwemo aliyekuwa MT 1900 Sajenti Roda Robert wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Kikosi cha Mbweni, ambaye alifariki dunia mwaka jana mkoani Dodoma wakati akisubiri utekelezwaji wa hukumu hiyo.
Katika hukumu hiyo,  Jaji Zainab alisema upande wa mashitaka umethibitisha kesi yao bila shaka na hivyo Mahakama imeona kuwa washitakiwa wote wana hatia na walimuua marehemu Fundikira kwa kukusudia.
Hata hivyo, alisema hakuna  shahidi aliyethibitisha kuwa aliwaona washitakiwa wanavyomuua Swetu, bali mashahidi watatu walithibitisha kuwaona washtakiwa wakiwa na Swetu kabla ya kukutwa na mauti.
Alisema anawatia hatiani washtakiwa na kuwahukumu kunyongwa hadi kufa kwa kuwa ushahidi wa mazingira umeowanyooshea kidole washitakiwa kuwa wanahusika na mauaji hayo.
Ilidaiwa Januari 23 ,2010 katika eneo la Kinondoni, Dar es Salaam, washtakiwa hao walidaiwa kumuua marehemu Fundikira. Katika kesi hiyo, upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi sita  ambapo katika usikilizwaji wa awali, washtakiwa wote walikana kutenda kosa hilo.

No comments: