Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
Abdulrahman Kinana amezitaka kamati za siasa za wilaya na mkoa za chama hicho,
kutowapitisha wagombea wa chama hicho wanaotumia rushwa, kujenga makundi ndani
ya chama hicho na kuanza kampeni kabla ya wakati.
Amesema hiyo ni siri pekee, itakayokifanya
chama hicho kutenda haki na kushinda kwa kishindo katika uchaguzi mkuu ujao wa
madiwani, ubunge na urais.
Amesema kwa kutambua hilo, ndio maana Kamati
Kuu ya Taifa ya chama hicho,
imewachukulia hatua, wanachama wa chama hicho
wanaotaka kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao lakini wakiwa wameanza
kufanya kampeni mapema, na hivyo kukiuka kanuni na taratibu za chama hicho
katika kuwapata wagombea.
Akiwahutubia mamia wa wajumbe wa Mkutano Mkuu
wa Jimbo la Mpwapwa, Kinana alisema ni dhambi kwa mgombea uongozi wa CCM
kutumia makundi, rushwa na kuanza kampeni mapema kama njia ya kumfanya
kushawishi kupata uongozi na kusisitiza kuwa viongozi wanaotumia mbinu hizo
kamwe hawawezi kuwaletea wananchi maendeleo.
Kinana yupo katika ziara ya kuutembelea mkoa
wa Dodoma, aliyoikatisha kufuatia kifo cha Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
(NEC) ya CCM, Mbunge wa Mbinga Magharibi na Kiongozi wa Kikundi cha Hamasa cha
TOT, marehemu John Komba aliyefariki dunia Februari 28, mwaka huu na kuzikwa
Machi 3, mkoani Ruvuma.
"Ukiona CCM imeshindwa katika uchaguzi
wowote ule wala usihangaike kutafuta
mchawi. Kushindwa kwa mgombea wa CCM mahala
popote pale iwe ni Mpwapwa, Biharamulo au penginepo hutokana na sababu za ndani
ya chama si nje, na sababu kubwa ni kutokana na kuwepo kwa makundi haramu ndani
ya chama.
"Haiwezekani CCM ikashinda kama viongozi
wanaohusika na uteuzi hawatendi haki,
anakuwepo mgombea mzuri, anapendwa na watu,
wanamheshimu, lakini yupo kiongozi fulani hamtaki, hii ndio chanzo cha migogoro
yote inayotokea nchini.Viongozi wa CCM wanakula njama wanasema huyo tusimchague
na badala yake wanakuja na jina la mgombea wa hovyo, hana sifa, mlanguzi au
mlevi.
"Imefika mahala mtu anapewa uongozi ndani
ya CCM kwa sababu ndani ya vikao vya uteuzi kuna ndugu zake, marafiki zake au
watu wanaomhusu.Hili suala la uonevu hatutalivumilia mwaka huu, haiwezekani
watu wa chini wanafanyiwa uonevu na viongozi wa juu wapo kimya. Ukiona kiongozi
huyu anakaa kimya kwa masuala kama haya jua kuna mambo mawili au anapendelea au
kapewa rushwa," alisema Kinana.
Kutokana na hilo, Kinana aliwataka wanaCCM
kuwa wakali kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu huku akisema viongozi wa chama
hicho waliochaguliwa katika nafasi
mbalimbali si wafalme bali ni viongozi
waliochaguliwa kuwaongoza wanachama wa chama hicho.
Katika kile kinachoonesha kukerwa na tabia
hiyo, Kinana aliutaka uongozi wa CCM Mkoa wa Dodoma chini ya Mwenyekiti
wake, Adam Kimbisa, kuwasaka viongozi
wote waliowaonea wagombea katika uchaguzi wa nafasi mbalimbali na kuwajadili
katika vikao vya Kamati ya Siasa ya Wilaya na Mkoa na wakithibitika waondolewe
haraka kwenye nafasi zao.
"Haiwezekani... mtu hafai, hana sifa,
ukiulizwa nini? Kanipa pesa, au ni jamaa yangu mwishowe wanaCCM wanapata hasira
wanakwenda kumpigia kura mgombea wa upinzani, hilo sasa mwisho wake umefika,
tutapambana," alisema Kinana akitolea mfano wa kiongozi wa upinzani katika
mji wa Gairo, aliyechaguliwa kutokana na haki kukiukwa kwa mgombea wa CCM.
Akiongeza Katibu Mkuu huyo wa CCM
alisema;"Sifa ya kwanza ya Kamati ya Siasa ya Wilaya na Mkoa ni kutenda
haki. Nyie mnasikia mnakaa kimya na baadaye mnakuja na visingizio mara ooh lete
barua.Tunakwenda kwenye uchaguzi msingi wa kwanza tenda haki ili wanachama
waamue mgombea udiwani, ubunge na urais wanayemtaka.
"Wakati wa uchaguzi ni wakati wa ajabu
sana, ni wakati ambao mtu mbovu anapewa lundo la sifa na mtu mzuri hapewi sifa
zake. Mtu anatoa fedha ili achaguliwe, ni dhambi
kupokea rushwa, mtu ananunua uongozi! Kuna
maendeleo hapo? Alihoji Kinana.
Katika hatua nyingine, Kinana amesema ni
marufuku kwa kiongozi yoyote wa Kamati ya Siasa ya Wilaya au Mkoa, kubeba jina
la mgombea yeyote kuelekea uchaguzi mkuu ujao na kwamba wanatakiwa kuwabeba
wagombea wote kwa usawa na kusema kiongozi atakayebainika kufanya hivyo
ataondolewa kwenye nafasi yake mara moja.
"Wapo watu ambao tayari wamechukuliwa
hatua kali na Kamati Kuu kwa kubainika kufanya kosa hilo ingawa bado
hatujawatangaza.Wapo watu tumewapa adhabu, unashangaa kuona kiongozi wa CCM
amebeba jina la mtu mmoja tu eti ndiye anafaa kwa ubunge au udiwani au urais,
lazima tutende haki hawa tutawapa adhabu," alisema Kinana.
No comments:
Post a Comment