VIGOGO WA ESCROW WASITISHA BARAZA LA MAADILI


Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma, limesitisha kusikiliza mashauri mawili likiwemo la Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA),  Philip Saliboko (pichani) hadi pale Mahakama Kuu itakapotoa uamuzi juu ya uhalali wa mashauri hayo, kusikilizwa na baraza hilo.

Shauri lingine lililositishwa kusikilizwa na baraza hilo ni la aliyekuwa Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Rugonzibwa Mujunangoma ambaye pingamizi aliloweka lilikubaliwa kutokana na kuwa na kesi ya jinai Kisutu inayofanana na shauri linalomkabili mbele ya baraza hilo.
Baraza hilo lilifikia uamuzi huo, baada ya upande wa mlalamikiwa kuweka pingamizi la kuendelea kusikilizwa kwa mashauri hayo, lakini baraza hilo liliyatupilia mbali mapingamizi hayo yanayomhusu Saliboko, ndipo upande wa mlalamikiwa ulipoamua kukata rufaa Mahakama Kuu juu ya uamuzi huo.
Awali Mwenyekiti wa baraza hilo, Jaji Hamisi Msumi, alipinga na kulitupilia mbali pingamizi lililowekwa na wakili wa Saliboko, lililotaka baraza hilo lisitishe kusikiliza shauri hilo kwa kuwa halina uwezo wa kufanya hivyo kutokana na amri iliyotolewa mwaka jana Mahakama Kuu.
Akiwasilisha pingamizi hilo mbele ya Baraza hilo, Dar es Salaam jana, Wakili wa mlalamikiwa, Jamhuri Johnson, alisema kutokana na zuio lililowekwa na amri iliyotolewa mwaka jana katika shauri namba 51 la Mahakama Kuu, baraza hilo halina uwezo wa kuendelea na shauri hilo linalomkabili Saliboko.
“Katika amri ile inatokana na kesi ya msingi ya IPTL dhidi ya Waziri Mkuu na wenzake saba, ilikataza na kuweka zuio kwa vyombo vyovyote vya umma kujadili suala linalohusiana na IPTL na akaunti ya Escrow, hadi kesi ya msingi itakapoamuliwa,” alisema Johnson.
Alisema anafahamu kuwa tayari baraza hilo lilishatolea uamuzi pingamizi kama hilo lililotolewa na Mbunge wa Bariadi Magharibi Andrew Chenge, lakini bado anaamini zuio hilo linalihusu pia na baraza hilo, hivyo halina uwezo wa kuendelea kusikiliza shauri hilo.
“Najua katika uamuzi ulioutoa awali ulisema baraza lina uwezo wa kusikiliza mashauri haya kwa kuwa amri hiyo ya Mahakama Kuu haijaligusa baraza hili na kwamba vipo vyombo maalumu vimeguswa, ukweli ni kwamba amri ile imezuia vyombo vyote vya umma, na naamini baraza hili pia ni chombo cha umma,” alisisitiza.
Aidha alisema ni vyema baraza hilo likasitisha kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa katika kesi ya msingi hoja kubwa inayolalamikiwa ni masuala ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow na umiliki wa IPTL jambo ambalo ni sawa na shauri lililopo dhidi ya Saliboko mbele ya baraza hilo.
Wakili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Hassan Mayunga kwa upande wake, alisema si vyema baraza hilo kuendelea kupokea mapingamizi hayo ambayo kwa sasa yanatumika kama fursa au kichaka cha kukwepa kuwajibika mbele ya Sheria.
Alisema amri inayozungumziwa ya Mahakama Kuu haihusishi mlalamikaji wala mlalamikiwa huku akisisitiza kuwa eneo linalodaiwa kuwa taasisi zote binafsi zimebanwa na amri hiyo halina ukweli kutokana na amri hiyo kubainisha wazi wale wote ambao hawatakiwi kujadili suala hilo na si baraza hilo.
“Napenda ieleweke Baraza halifanyi kazi kwa niaba ya yeyote aliyehusishwa katika kesi hiyo, amri hii haijazuia dunia nzima, naomba mheshimiwa Mwenyekiti upuuze mapingamizi haya,” alisema Mayunga.
Akijibu hoja hiyo, Jaji Msumi awali alitupilia mbali pingamizi la wakili wa Saliboko kwamba baraza hilo halina uwezo wa kusikiliza shauri hilo na kubainisha wazi kuwa tayari alishatoa uamuzi kama huo katika shauri la Chenge na kuendelea kusisitiza kuwa baraza hilo, halihusishwi katika amri iliyotolewa na Mahakama Kuu.
“Kwanza hatumo kwenye orodha ya vyombo vinavyotajwa katika amri hii, nakataa madai yenu kuwa Baraza halina uwezo wa kusikiliza shauri hili, lakini pia amri ile iko wazi kuwa kinachotakiwa ni kutofanyika kwa jambo lolote litakalosababisha suala hili kufikishwa bungeni,” alisema Jaji Msumi.
Kuhusu shauri la Mujunangoma, pamoja na kukatalia pingamizi linalodai kuwa baraza hilo halina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, pia alikubali kusitisha shauri hilo, kutokana na kuthibitisha kuwa kiongozi huyo ana kesi ya jinai katika Mahakama ya Kisutu yenye mashtaka yanayofanana na yanayomkabili katika Baraza.
“Sheria haikatazi mtu kufunguliwa mashtaka mengine na chombo kingine cha Sheria, ila inakataza kumfungulia mtu huyo, mashtaka yanayofanana katika vyombo viwili tofauti, hiyo inaweza kumfadhaisha mlalamikiwa katika utetezi wake,” alisema.
Mayunga akimsomea mashtaka Saliboko, alidai kuwa kutokana na cheo chake cha Ukurugenzi Mkuu RITA, aliomba fadhila za kiuchumi kutoka kwa James Rugemalira, na kupatiwa Sh milioni 40.4 kinyume na Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Alisema pia kutokana na wadhifa wake huo, alikuwa ni mfilisi wa muda wa mali za IPTL hivyo kitendo cha kupokea fedha hizo kutoka kampuni ya VIP Engeneering and Marketing Limited yenye hisa asilimia 30 na IPTL,  ni ukiukaji wa Sheria ya Maadili inayokataza kiongozi wa umma kujiingiza katika mgongano wa kimaslahi.
Hata hivyo,  baraza hilo leo litaendelea kumhoji Naibu Kamishna wa  Upelelezi wa Kodi (TRA),  Lucy Apollo.

No comments: