Kiongozi wa Jumuiya ya Uamsho na
Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (JUMIKI) Shekhe Farid Hadi Ahmed (45) na wenzake
wanaokabiliwa na kesi ya ugaidi bado wanasota rumande kwa kwa kuwa upelelezi wa
kesi bado haujakamilika.
Kesi hiyo ilitajwa jana mbele ya Hakimu
Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Janeth Kaluyenda.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tumain
Kweka aliomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa kuwa upelelezi bado haujakamilika
pia wanasubiri uamuzi wa rufaa waliyoikata Mahakama ya Rufaa dhidi ya uamuzi
uliotolewa na Jaji wa Mahakama Kuu, Dk Fauzi Twaib.
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) alikata
rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam ulioamuru Mahakama
ya Kisutu kusikiliza na kutolea uamuzi hoja, zilizowasilishwa na Shekhe Farid
na wenzake.
Katika ombi lao, washitakiwa waliomba
Mahakama ya Kisutu ifute mashitaka ya ugaidi dhidi yao, pia walihoji uhalali wa
kushitakiwa Tanzania Bara wakati Zanzibar ni nchi ambayo ina Mahakama Kuu na
kuomba wakashtakiwe katika sehemu walizokamatwa.
Hakimu Kaluyenda aliahirisha kesi hiyo
hadi Aprili Mosi ,2015 kwa ajili ya kuangalia kama upelelezi utakuwa umekwisha
kamilika pia kusubiri uamuzi wa Mahakama ya Rufaa.
Washitakiwa wanadaiwa kati ya Januari
mwaka jana na Juni mwaka huu katika maeneo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
walikula njama ya kutenda kosa kwa kutafuta watu wa kushiriki vitendo vya
ugaidi.
Katika mashitaka mengine, wote wanadaiwa
katika kipindi hicho, huku wakijua ni kosa walikubaliana kuwaingiza nchini,
Sadick Absalom na Farah Omary washiriki vitendo vya ugaidi.
No comments:
Post a Comment