UKWELI KUHUSU MTOTO WA FLORA MBASHA HUU HAPA


Mwimbaji wa nyimbo za injili, Florence Mayala maarufu kama Flora Mbasha amekiri kuwa mtoto aliyejifungua hivi karibuni ni wa Emmanuel Mbasha (32) na kwamba bado anampenda mumewe huyo.

Flora alidai hayo jana katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dar es Salaam akiwa shahidi wa tatu katika kesi ya ubakaji inayomkabili Mbasha baada ya mawakili wanaomsimamia Mbasha, Mathew Kakamba na Ngassa Ganja kumtaka Flora aeleze kama mtoto huyo ni wa mumewe huyo.
Mwimbaji huyo alidai kuwa hakuwahi kufanya mapenzi nje ya ndoa na kuwa anaamini motto huyo ni wa Mbasha.
Pia alidai kwamba mambo mengine ya kifamilia na migogoro ya ndoa yake hawezi kuyazungumzia mahakamani tofauti na kesi iliyokuwepo.
Katika kesi ya msingi, Flora alidai kwamba Mei 23, mwaka jana, aliondoka yeye na Mbasha kwenda studio ambako Mbasha alimuacha na kurudi nyumbani.
Alidai baada ya kumaliza masuala yake ya studio, alirudi nyumbani na kumkuta mdogo wake akiwa amelala huku amejifunika khanga, ndipo alimuuliza hali yake, naye akajibu kuwa anajisikia vibaya bila kumwambia kitu kilichomtokea.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Nassoro Katuga, shahidi huyo alieleza kuwa wakati mambo hayo yote yanatokea, yeye alikuwa na mawazo kuhusu migogoro iliyokuwepo katika familia hiyo.
Flora alidai kuwa Mei 25, mwaka jana, walienda kanisani pamoja na watoto wake na baada ya ibada kumalizika, aliwarudisha nyumbani.
Alidai hakukaa nyumbani kwake siku hiyo, bali alikwenda kwa rafiki yake ambaye anaishi karibu na nyumbani kwake na ilipofika jioni, aliondoka na kwenda Sinza ambako alilala hotelini.
Pia alidai kuwa wadogo zake walimpigia simu na kumweleza kwamba kuna tatizo limetokea nyumbani kwake na kuwaambia kuwa wamfuate hotelini alipokuwa amelala.
“Walipofika hotelini, mdogo wangu aliniambia kuwa Mbasha amembaka na kwamba sio mara ya kwanza kwani siku niliporudi kutoka studio, alikuwa tayari amebakwa, lakini hakutaka kuniambia alitishiwa kuuawa,” alidai Flora.
“Baada ya kunieleza hivyo, niliwaambia waende hospitali kumpima mdogo wangu ambaye alinieleza kuwa alibakwa. Tangu niondoke nyumbani hapo sikurudi na baada ya kusikia kwamba Mbasha amebaka, sikutamani hata kurudi kwani niliona mambo yanazidi kuwa magumu,” alidai mwimbaji huyo.
Pia alidai kuwa chanzo cha yeye kutorudi nyumbani kwake ni kutokana na msongo wa mawazo aliokuwa nao kuhusu mgogoro wake na Mbasha.
Mahakama hiyo iliahirisha kesi hiyo hadi Aprili 16, mwaka huu atakaposikilizwa shahidi wan ne katika kesi hiyo.
Mbasha anakabiliwa na mashitaka mawili ya ubakaji ambayo ilidaiwa Mei 23, mwaka jana, maeneo ya Tabata Kimanga, wilaya ya Ilala, alimbaka motto wa umri wa miaka 17 nyumbani kwake.
Pia ilidaiwa Mei 25, mwaka jana, alimbaka tena motto huyo ndani ya gari kinyume cha sharia za nchi.

No comments: