UFISADI MWINGINE WA MILIONI 700 WIZARA YA NISHATI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imetoa maelekezo kwa Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali(CAG) kufanya uchunguzi wa Sh milioni 699 zinazodaiwa kutolewa na Wizara ya Nishati na Madini kwenda Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambazo zinaonekana kuyeyuka katika mazingira yasiyoeleweka.

Agizo hilo lilitolewa na Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam wakati wa Hesabu za TANESCO.
Kabwe alisema katika ripoti ya ukaguzi wa hesabu wa shirika hilo inaonekana wizara imetoa Sh milioni 699 kwenda Tanesco, lakini shirika hilo limeeleza kuwa halijawahi kupokea fedha hizo, jambo ambalo linaleta utata na kuhoji ni wapi fedha hizo zimekwenda.
“Kamati inamtaka CAG afanye ukaguzi maalum, kwa kushirikiana na Tanesco na Wizara na kisha ilete taarifa ni wapi fedha hizo zimekwenda,” alisema.
Awali akitoa maelezo kuhusu fedha hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya Tanesco, Dk Mighanda Manyihi alisema Tanesco haijawahi kupokea fedha hizo na kumuomba Mwenyekiti wa PAC na kamati kufanya kila linalowezekana ili fedha hizo zipatikane kwani zitakuwa msaada kwa shirika.
“Mwenyekiti, hizo fedha hata siye tunazihitaji sana kuna miradi mingi sana ambayo imekwama, kama fedha hizo zikipatikana zitatufaa sana,” alisema.
Naye Kaimu Ofisa Mkuu wa Fedha, Anetha Chengula akitolea ufafanuzi suala hilo mbele ya Kamati alisema Tanesco haijawahi kupewa fedha hizo na kwamba walishafuatilia hadi wizarani kwa wahasibu wa wizara na kushindwa kutoa vielelezo kuthibitisha kutoa fedha hizo.
Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imeagiza Bodi ya Tanesco kuhakikisha ifikapo Aprili 30, mwaka huu nafasi zote za ngazi ya Menejimenti kuwa zimejazwa na hakuna tena suala la kukaimu kwani bodi ina mamlaka kisheria kufanya hivyo.
Hatua hiyo imekuja baada ya Anetha Chengula ambaye alijitambulisha kama Kaimu Ofisa Mkuu wa Fedha ambapo Mwenyekiti alihoji  Bodi na Menejimenti kwa nini ofisa huyo anaendelea kukaimu wakati Bodi ina mamlaka ya kuteua na kupanga menejimenti kwa mujibu wa Sheria.
Kamati ikitoa uamuzi kuhusu suala hilo, iliagiza Bodi kujaza nafasi zote zilizo wazi katika menejimenti ifikapo Aprili 30 na itakapokamilisha ipeleke taarifa kwa Katibu wa Bunge, pamoja na kuitaka bodi mpya kupitia mikataba yote na kisha kupeleka taarifa kwa Katibu wa Bunge badala ya kusubiri kuitwa tena katika kamati.

No comments: