WASOMI WAIPIGIA MAGOTI CHADEMA IMSAMEHE ZITTO

Wasomi na wachambuzi wa masuala ya siasa nchini, wamekishauri Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumsamehe Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto kwa kuwa bado anahitajika kujenga chama hicho.

Mmoja wa wasomi wa chuo cha Diplomasia, Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Balozi Charles Sanga alisema kuwa pamoja na umuhimu wa kuheshimu katiba ya chama, ameshauri chama hicho kingefanya uvumilivu na sio kuchukua hasira.
Alisema ni vyema uvumilivu ukatumika katika kukijenga chama hicho na sio kufanya maamuzi ya hasira ambayo yanaweza kupunguza nguvu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.
“Kujenga chama cha siasa sio jambo jepesi na la siku chache, ni kitu kinachochukua muda mrefu na huko ndani kuna watu tofauti sasa ni vyema jambo kama hili, Chadema ingefanya uvumilivu, ujenzi wa chama sio lele mama,” alisema na kuongeza:
“Nchi za Kiafrika bado zinajaribu kujenga vyama vyao, kwani ni  changa, tunahitaji kuvilea, tuvumiliane, ila pia sheria mama za vyama zisivunjwe, ila pia sheria za kawaida ziangaliwe tuvumiliane kidemokrasia na sio kuchukua hasira”.
Alisema suala ya Zitto linapaswa kuangaliwa kwa mapana yake na kuangalia pia wananchi wa jimbo lake kwani athari zake ni kuwanyima wananchi uwakilishi kupitia jimbo hilo.
“Wananchi wa jimbo lake wataathirika, mara nyingi hatuangalii maslahi ya wananchi tunaangalia maslahi ya vyama, na hii sio sahihi kidiplomasia, tupime mizani je, aliyoyafanya kwa chama chake miaka yote na taifa kwa ujumla yana uzito kiasi gani ukilinganisha na adhabu aliyopewa?” Alihoji.
Alisema maamuzi ya Chadema yanaweza kukibomoa chama badala ya kukijenga kwani uamuzi wa kumfukuza Zitto, unaweza unakifanya kugawanyika kwani wapo wanachama watakaomuunga mkono Zitto hivyo kukibomoa chama, jambo ambalo sio jema.
Na kusema jambo hilo liwekwe mizani, na kwamba ni vyema vyama vinapofanya maamuzi visifanye kwa hisia na kushauri kama kuna nafasi nyingine zaidi ya hapo Zitto aitumie kukata rufaa.
Msomi mwingine, Benson Bana ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mchambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania, pamoja na Robert Mkosamali, msomi na mchambuzi pia wa siasa hizo walisema, kwa nyakati tofauti pia kuwa, kwa kumvua uanachama Zitto Kabwe, Chadema atajibomoa kwa kupunguza wanachama.
Akizungumzia kipengele cha katiba ya Chadema, kinachokinzana na Katiba ya nchi ya mwaka 1977, pamoja na haki za binadamu, Bana alisema;
"Msajili wa vyama vya siasa ana kila sababu ya kufanya mapitio ya katiba zote za vyama vya siasa kuhakikisha hazina vipengele vinavyomzuia mwanachama au kiongozi wa chama kwenda mahakamani kutafuta haki anayoamini kuwa hawezi kuipata ndani ya chama chake".
Alisema, katiba ya chama hicho inaposema kuwa Zitto amevuliwa uanachama kwa sababu amekwenda kukishitaki chama mahakamani, inakuwa imekwenda kinyume cha katiba ya nchi na haki za binadamu, zinazoelekeza kuwa chombo cha mwisho cha kutoa haki kwa mtu yeyote ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Mahakama.
Alisema, katiba ya nchi ya mwaka 1977 ndio sheria mama inayobeba katiba zote, zikiwemo za vyama vya siasa, kwa hiyo, kuwepo kwa sentensi inayokinzana na katiba mama ni kasoro pia inayoweza kusababisha udhaifu kama huo wa kufukuzana katika vyama.
Alieleza; "Wakati inasemwa kuwa mahakama ndio sehemu pekee ambayo mtu anaweza kukimbilia kupata haki yake ya msingi, wanachama katika vyama vyenye katiba zisizozingatia misingi ya haki za binadamu wanang'ang'ana kufukuzana kwa kosa la mtu kwenda kutafuta haki yake mahakamani.
"...Ni katiba ipi iko juu kimamlaka kati ya hiyo ya Chadema na ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania? Jaji Mutungi ategue kitendawili hiki ili wanachama wasioneane na wasikomoane kwa sababu tu ya chuki, wivu na uadui unaosababishwa na hofu za kuzidiana 'kete' katika uongozi ndani ya vyama".
Aliongeza kuwa, tatizo lililotokea kwa Zitto halipaswi kuwatingisha Watanzania kwa kuwa, nafasi ya kutekeleza majukumu aliyoyaanza kwenye chama hicho ataipata kwingine kokote atakakojiunga kwa sababu ya uwezo wake wa kufanya kazi, mvuto na umaarufu wa kisiasa aliouonesha.
Bana anasisitiza kuwa hatima ya Zitto kisiasa bado ipo juu tofauti na ilivyo kwa CHADEMA ambacho, bila kutarajia kitakuwa kimepoteza watu wote waliokuwa wakimuunga mkono Zitto, ambao ni wengi.
Kwa upande wake, Mkosamali alisema, mahakama ndicho chombo pekee kinachotajwa na katiba ya nchi kuwa ndipo mtu yeyote anapoweza kukimbilia kupata haki yake ya msingi.
"Ni kweli Ibara ya 71 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ndogo ya 1 (e) inasema; "Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika bunge itokeapo mambo yafuatayo;
(f) Iwapo Mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama chake na iwapo chama chake kitakuwa kimemvua uanachama.
Kwa maelezo ya Mkosamali, kulingana na maelezo hayo ya katiba, Zitto amevuliwa uanachama, lakini bado chama chake kupitia mikutano ya ndani, kinaweza kumpa nafasi nyingine kwa kuyajadili mambo hayo kwa uvumilivu ndani ya mikutano yake.
"Kazi ya Zitto katika PAC (Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali) imeonekana, mchango wake katika kukuza demokrasia na siasa nchini nayo imeonekana kwa hiyo kuondolewa kwake katika chama kunaweza kuiathiri kamati hiyo kwa sababu ukali wake na usimamizi wake madhubuti wa majukumu aliyokuwa akiyatekeleza hautakuwepo tena".
Bana na Mkosamali wanamshauri Zitto asikimbilie kuanzisha chama kipya cha siasa sasa hivi, kwa sababu, muda uliopo hadi kufikia uchaguzi mkuu Oktoba ni mfupi usiotosha kukijenga na kukiimarisha chama.
Naye Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi, Julius Malaba alisema jana kuwa, ofisi yake itaipokea barua hiyo na kuifanyia kazi, endapo itawasilishwa kwa kufuata taratibu zinazostahili.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah, amebainisha kuwa endapo Bunge litapata taarifa rasmi ya Chadema kumvua uanachama Zitto, lazima Bunge hilo lifanye kwanza uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili ndipo litoe uamuzi.
Pia amesema sakata la mbunge wa Bunge hilo kuvuliwa uanachama na chama chake si la kwanza, kwani tayari kuna mbunge aliyevuliwa uanachama na chama chake lakini Bunge hilo halikumvua uanachama wake baada ya kumaliza uchunguzi wake. Hata hivyo hakumtaja mbunge huyo.
Akizungumza na mwandishi Dar es Salaam, Katibu huyo, alikiri kusikia habari za Zitto kuvuliwa rasmi uanachama wake na chama chake, lakini alisisitiza kuwa bado ofisi yake haijapokea barua rasmi kutoka kwa chama chake kwa ajili ya kupatiwa taarifa hizo.
“Utaratibu ulivyo, chama huliandikia Bunge kuhusu kumvua uanachama mbunge na Bunge kabla ya uamuzi wowote hufuatilia kwanza sababu za kuvuliwa uanachama huo, ili kujiridhisha kama zilikuwa halali au la,” alisema Kashililah.
Alisema baada ya hapo Bunge hilo huwasiliana na Msajili wa Vyama vya Siasa ili ofisi hiyo ya msajili iweze kupitia Katiba ya chama husika na kupitia sababu za chama husika zinazoweza kumvua uanachama mwanachama wake na kama kweli zimekiukwa.
“Baada ya suala hilo kupelekwa kwa msajili wa vyama vya siasa, Spika wa Bunge, hutoa uamuzi baada ya kuchunguza na uamuzi huo, hupelekwa kwa Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) kwa ajili ya kufanyiwa kazi zaidi,” alisisitiza.
Aidha alisisitiza: “Si lazima Spika atoe uamuzi wa kutengua ubunge wa mbunge husika kwani kama haikuwa halali kwa mbunge huyo kuvuliwa uanachama, Spika hubatilisha uamuzi wake wa kumvua ubunge mhusika,” alisema.
Alisema Spika Anne Makinda katika kipindi chake alishawahi kutoa uamuzi wa kubatilisha mbunge fulani kuvuliwa ubunge hata baada ya chama chake kumvua uanachama.
Akizungumzia suala hilo, Zitto, alisema kwa upande wake bado ni mbunge na anaendelea na kazi yake ya Uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) hadi pale atakapopatiwa taarifa rasmi ya kuvuliwa uanachama na ubunge wake.
“Naendelea na kazi kama vile hakuna kilichotokea, sina taarifa yoyote ya kuvuliwa uanachama wangu wala ubunge, habari hizi nimezisikia kwenye vyombo vya habari, sijaitwa na Mahakama kuambiwa kinachoendelea,” alisema Zitto.
Alisema kwa sasa anaendelea kuongoza kamati hiyo na jana alikutana na menejimenti ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), leo kamati yake inatarajia kukutana na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), pia watakutana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mwanasheria Mkuu kuhusu mapato ya akaunti za madini.
Aidha alisema pamoja na kuendelea kama kawaida na shughuli zake za kibunge bungeni, pia anatarajia kesho kwenda Kigoma kwa ajili ya shughuli za maendeleo jimboni kwake, kabla ya kuhudhuria vikao vya Bunge vinavyotarajiwa kuanza rasmi Machi 17, mwaka huu.
Alisema kwa upande wake, anachukulia suala hilo kama changamoto ambayo inazidi kumkuza na kumkomaza katika medani za siasa nchini na duniani kote.
Kwa upande wake, Ofisa Habari wa Chadema, Tumaini Makene alisema chama hicho kinajitahidi kulifanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia sheria na taratibu zote, ikiwemo kuandaa na kuiwasilisha wakati wowote barua inayomvua uanachama Zitto, ili suala hilo lifanyiwe uamuzi mapema.
“Kwa sasa suala hili la Zitto limewaingia Watanzania wengi, sasa sisi tunataka tulifanyie kazi mapema, ili uamuzi ufanywe mapema na suala hili liishe. Kuna mambo mengi ya maana yanahitaji kujadiliwa kitaifa kama vile masuala ya uandikishaji katika Daftari la Wapiga kura kwa mfumo wa BVR,” alisema.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye juzi alitangaza kuwa chama hicho kimemvua uanachama mbunge huyo, jana alimwambia mwandishi kuwa, jopo la wanasheria wa chama hicho litaifikisha taarifa ya Zitto kuvuliwa uanachama kwa Kamati Kuu ya chama ifikapo Mei, mwaka huu.
Alisema, "Kutokana na utaratibu uliopangwa wa Kamati Kuu kukutana kila baada ya miezi mitatu, suala la Zitto litasubiri kikao kingine cha kawaida cha kamati hiyo kitakachokaa mwezi Mei. Kikao kilichopita kilikaa Februari mwaka huu".
Kwa maelezo ya Lissu, baada ya hapo ndipo wataiandikia barua Tume ya Uchaguzi (NEC) kuijulisha kuwa Zitto si mwanachama wa chama hicho tena au la.

No comments: