TIBAIJUKA, CHENGE, NGELEJA WASIMAMISHWA CCM


Kamati Kuu ya CCM (CC) imewasimamisha uongozi wa vikao vya chama, vigogo watatu wa chama hicho, akiwemo Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kutokana na kuhusishwa na sakata la Escrow.

Wengine waliosimamishwa kuhudhuria vikao vinavyohusu uamuzi wa chama ni pamoja na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi Januari, mwaka huu Zanzibar, kuagiza Kamati ndogo ya Maadili kuwaita na kushughulikia suala la viongozi wa chama hicho, waliokuwemo katika vikao vya uamuzi ya chama hicho waliohusishwa na sakata la Escrow.
Akitoa taarifa ya kikao cha Kamati Kuu ya CCM kilichofanyika Ikulu Dar es Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Nape Nnauye alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya Kamati ya Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho (Bara), Philip Mangula kuwahoji vigogo hao.
Alisema Kamati hiyo ya Maadili iliwasilisha ripoti yake kwa Kamati Kuu jana, ndipo ukafikiwa uamuzi wa vigogo hao kusimamishwa kuhudhuria vikao vya chama vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa Profesa Tibaijuka na Halmashauri Kuu kwa Chenge na Ngeleja.
"Uamuzi wa Kamati Kuu ni kuwasimamisha uongozi wao kwenye vikao vya chama, kwamba wasihudhurie vikao vya chama vya Kamati Kuu kwa yule mjumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa wajumbe wake, kwa kipindi ambacho Kamati hii ndogo ya Maadili wakiendelea kupitia nyaraka mbalimbali zinazohusu suala hili," alisema Nape.
Akizungumzia vigogo sita wa chama hicho waliokuwa kwenye adhabu baada ya kuthibitika kukiuka maadili ya Chama na kuanza kampeni mapema, Nape alisema tathimini ya mwenendo wao bado inaendelea.
Vigogo hao ambao tathimini ya mwenendo wao bado inaendelea, ni pamoja na waliokuwa mawaziri wakuu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Wengine ni Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, ambaye ameshatangaza nia ya kugombea urais, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Stephen Wasira na Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Alisema kanuni za usalama na maadili ya chama iliyotumika kuwahukumu, ni inayosema onyo kali alilopewa mwanachama, maana yake atakaa chini ya uangalizi kwa kipindi kisichopungua miezi 12.
"Sasa baada ya ile miezi 12 kuisha, kamati ndogo ya maadili inaendelea na kazi yake ya kuchunguza mienendo ya hao waliokuwa wamepewa adhabu, katika kipindi chao cha adhabu ya miezi 12 wametekeleza masharti ya adhabu zao," alisema.
Alisema baada ya hapo, kamati hiyo itawasilisha ripoti ya uchunguzi wake kwa Kamati Kuu ambapo kama kutakuwa na taarifa yoyote, itatolewa kwa umma.
Aidha, Nape alitumia fursa hiyo kuwaonya baadhi ya wanasiasa wengine waliojitokeza na kutangaza nia zao za kugombea urais kwa kuvunja sheria na taratibu za chama hicho, wasije kukilaumu chama hicho.
"Kila mmoja ambaye atavunja kanuni katika mchakato mzima wa kutafuta kuteuliwa na Chama Cha Mapinduzi, atachukuliwa hatua, hakuna atakayepona katika mkono wa sheria na taratibu za chama kama atazivunja, ni suala la muda kama kuna mtu anaendelea kuvunja.
“Msisitizo wa Kamati Kuu ni kwamba watu wote wanaotaka uteuzi wa chama, wafuate taratibu ili tusije tukalaumiana baadae, kwa sababu wakati mwingine wanadhani ni suala la Nape au Katibu Mkuu kuwa mkali, hii ni kanuni, hakuna atayepona.
“Hili suala la watu sita lilianza muda mrefu, lakini yapo maneno wako na wengine wanavunja sheria na taratibu lakini, msimamo wa chama hiki hakuna atakayevunja sheria akaachwa salama," alisema.

No comments: