HIVI NDIVYO MAUTI YALIVYOMKUTA KAPTENI JOHN KOMBA


Ni huzuni kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jimbo la Mbinga Magharibi, Taifa, marafiki na familia, baada ya kufikwa na msiba mkubwa wa kiongozi, Mbunge, Kapteni wa Jeshi, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) na msanii mashuhuri wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), Kapteni John Komba.

Msiba huo ulitokea jana wakati Kamati Kuu ya CCM, ikiwa katika kikao cha kawaida, kilichokuwa na ajenda muhimu, ikiwemo ya kujadili makada sita waliokuwa wakitumikia adhabu, baada ya kukiuka maadili ya chama na kuanza kampeni za urais mapema.
Mbali na makada hao, kikao hicho pia kilikuwa na ajenda ya kujadili makada wengine watatu, waliokuwa wakikabiliwa na kashfa ya kupokea fedha zilizokuwa katika iliyokuwa akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa Benki Kuu (BoT).
Lakini kabla hata uamuzi wa kikao hicho kutangazwa, Kapteni Komba aliaga dunia na taarifa za awali zilieleza kuwa alikuwa nyumbani kwake Mbezi Beach, akajisikia vibaya na kukimbizwa katika Hospitali ya TMJ, Mikocheni Dar es Salaam, ambako aliaga dunia wakati akipata huduma.
Taarifa zilizotufikia zilieleza kuwa mtoto wa marehemu, Jerry Komba, alisema kifo cha baba yake kilisababishwa na kushuka ghafla kwa sukari.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Kapteni Komba alikimbizwa katika Hospitali ya TMJ Mikocheni ambako alifariki dunia.
Baada yakifo hicho, taarifa kutoka kwa Katibu wake, Gasper Tumaini, zilieleza kuwa mwili wa Kapteni Komba ulipelekwa katika Hospitali ya JWTZ ya Lugalo, ambako umehifadhiwa ukisubiri taratibu za mazishi.
Muda mfupi baadaye, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  na Mwenyekiti wa CCM,  Jakaya Kikwete alituma salamu za rambirambi kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana.
Katika salamu hizo, Rais Kikwete alisema amepokea kwa mshituko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Kapteni Komba, Mbunge, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) na msanii hodari wa kizazi chake.
“Nimepokea kwa mshituko mkubwa na huzuni nyingi taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Kapteni John Komba, ambacho nimejulishwa kuwa kimetokea mchana wa leo (jana), Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ, Dar es Salaam.
“Kwa hakika, sina maneno ya kutosha kuelezea kwa ufasaha hasara ambayo Taifa letu na Chama chetu kimepata kutokana na kifo cha Kapteni Komba.
“Taifa letu limepoteza hazina kubwa na mtu muhimu. Nimemjua Kapteni Komba kwa muda mrefu sana, nimefanya naye kazi. Alikuwa msanii ambaye kiwango chake cha usanii kilikuwa hakipimiki, alikuwa na sifa kubwa za uongozi, alikuwa mpenzi, mzalendo na mtu mwaminifu sana kwa taifa lake na katika jambo lolote aliloliamini,” amesema Rais Kikwete katika salamu hizo na kuongeza:
“Akiwa mwalimu, lakini hasa akiwa mlinzi wa Taifa katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Kapteni Komba alithibitisha sifa zake za mlinzi wa Taifa, kwa kipaji chake cha kutunga na kuimba nyingi za kuhamasisha wanajeshi wetu katika ulinzi wa nchi yao.
“Alikuwa na uwezo mkubwa wa kisanii kutunga nyimbo za aina zote  ziwe za maombolezo, za kutoa hamasa, za makaribisho, ziwe za kampeni za kisiasa na kijamii ama ziwe za kampeni maalumu. 
“Mheshimiwa Komba alikuwa Mbunge hodari sana na wananchi wa Nyasa wamepoteza mtetezi wa uhakika. Mheshimiwa Komba alikuwa mcheshi, aliyependa sana utani na alikuwa na uongozi mkubwa wa kutambua na kulea vipaji vya sanaa na wasanii, kama alivyothibitisha katika kuanzisha na kulea kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT) na kabla ya hapo.
“Kupitia kwenu waheshimiwa, naomba mnifikishie salamu zangu za dhati kabisa kwa wabunge wote ambao wameondokewa na mwenzao na wananchi wa Jimbo la Nyasa na Mkoa wote wa Ruvuma, ambao wamepoteza mwakilishi na kiongozi wao.
“Ndani ya chama chetu, naomba salamu zangu ziwafikie wanachama wetu wote kwa kupoteza mwanachama mwenzao, ziwafikie viongozi na hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ambayo imepoteza mwakilishi mwenzao na wasanii wote wa Tanzania One Theatre (TOT) ambao Kiongozi wao ameondoka duniani,” alisema Rais.
“Naungana na wanafamilia kuomboleza kifo cha rafiki yetu, ndugu yetu na kiongozi mwenzetu. Napenda wanafamilia wajue kuwa natambua uchungu wao katika kipindi hiki na tahayari yao ya  kuondokewa na mhimili wa familia.
“Niko nao katika maombolezo na katika kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya marehemu Kapteni John Damian Komba. Amina,” alimaliza Rais Kikwete.
Akizungumzia kifo cha Kapteni Komba, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu (NEC), Nape Nnauye alisema, kifo hicho kimeleta mshituko mkubwa katika chama hicho na ni pigo kwao.
"Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, imepokea kwa mshituko mkubwa taarifa za kifo cha Mjumbe wa Halmashauri Kuu, msanii wetu na kada wa siku nyingi na tegemeo kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi,” alisema.
Alimkariri Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Kikwete alipowaambia kuwa “kifo hicho ni pengo kubwa kwa chama hicho na gumu kuzibika hasa kwa wakati huu wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu”.
Alisema wimbo ambao aliutunga katika sherehe za miaka 38 ya chama hicho, uliwasisimua wengi na pengine msisimko huo ulikuwa ni namna ya kuwaaga Watanzania na wanachama wa CCM.
Nape alitoa pole kwa familia ya Kapteni Komba na wanachama kwa ujumla, ambapo alisema Komba ataendelea kubaki katika historia iliyotukuka ya chama hicho.
Miongoni mwa waliotuma rambirambi kupitia ukurasa wake wa Facebook, ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Tanzania Bara, Mwigulu Nchemba.
“Natoa pole sana kwa Wananchi wa Mbinga, WanaCCM na Watanzania wote kwa Msiba Mzito uliotokea wa kifo cha Mpendwa wetu Mh. Kapt.John Komba na Mjumbe wa Halmashauri Kuu CCM Taifa. Pumzika kwa Amani,” aliandika katika ukurasa wake.
Taarifa zingine zilizotufikia, zilieleza kuwa jana mchana, muda mfupi kabla ya kufikwa na mauti, alifanya kazi ya mwisho ya kutumikia jimbo lake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, Kapteni Komba alikwenda katika viwanda vya bati na chuma vya MMI Steel Industries vilivyoko Mikocheni, akalipia mzigo wa mabati unaofikia lori mbili, kwa ajili ya kupeleka jimboni kwake Mbinga.
Inadaiwa baada ya kulipa, aliacha maagizo kwa Keshia kiwandani hapo aitwae Jastin, kuwa madereva watakuja kuubeba mzigo huo na yeye anakwenda   kupima sukari na shinikizo la damu katika Hospitali ya TMJ.

No comments: