SAUTI YA KAPTENI KOMBA KUENDELEA KURINDIMA CCM


Sauti ya Kada wa CCM, aliyekuwa Mbunge wa Mbinga Magharibi na Kiongozi wa Kikundi cha Tanzania One Theatre (TOT),  Kapteni John Komba, huenda ikaendelea kusikika katika vibao vipya ambavyo alishaviandaa.

Akizungumzia msiba huo, katika mahojiano ya ana kwa ana na Naibu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam Media,  Tido Mhando, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete alisema Komba alikuwa akifuatilia malipo ya kusanifu nyimbo za kampeni.
Alisema kabla ya Kapteni Komba kufikwa na mauti, Jumamosi iliyopita ya Februari 28, mwaka huu, asubuhi yake alituma ujumbe mfupi wa maandishi wa simu ya mkononi, kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, akimshukuru kwa kupokea fedha kwa ajili ya kusanifu nyimbo hizo.
Rais Kikwete aliyekuwa akizindua studio za kisasa za Azam Media, alisema siku hiyo walipokuwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM, alipokea ujumbe kuhusu msiba huo, akamuonesha Kinana ambaye alijikuta akisema; “haiwezekani.”
Alisema Kinana alimwambia kwamba asubuhi ya siku hiyo, aliwasiliana na Kapteni Komba, ambaye alimshukuru kwa kupokea fedha hizo za kusanifu nyimbo hizo katika akaunti ya TOT.
“Kifo hiki kimetushitusha kwa sababu alikuwa hajaugua muda mrefu. Tumezoea mgonjwa unakuwa naye muda mrefu, anakusumbua mpaka unakuwa na wasiwasi kuwa kesho anaweza asiwepo, lakini hilo halikutokea kwa Komba.
 “Asubuhi aliwasiliana na Kinana, alikuwa akifuatilia malipo ya fedha za TOT kwa ajili ya kufanya usanifu wa nyimbo za kampeni. Alipopata malipo akampa taarifa Kinana asubuhi kuwa fedha zimeshafika,” alisema.
Mwili wa Komba uliagwa jijini Dar es Salaam Jumatatu ya wiki hii katika viwanja vya Karimjee, ambapo nyimbo zake zilisababisha majonzi makubwa kwa waombolezaji.
Moja ya nyimbo hizo, ni pamoja na ule alioimba katika msiba wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999, ambao ulipopigwa uliibua majonzi na kusababisha viongozi mbalimbali, akiwamo Rais Kikwete, kutoa machozi.
Wimbo huo uliobadilishwa maneno yaliyomhusu Mwalimu Nyerere na kuingizwa yaliyomtaja mbunge huyo wa Mbinga Magharibi, ambapo mbali na Rais Kikwete, ulimliza pia Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Spika wa Bunge, Anne Makinda, Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Yusuf Makamba na waombolezaji wengine.
Sehemu ya mashairi ya wimbo huo uliokwenda kwa jina la 'Nani Yule' ulioimbwa na wanamuziki mbalimbali wa bendi nchini, na kuwatoa watu machozi uliimbwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye.
“Kapteni Komba familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha na nani, nenda baba msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita.”
Komba aliyekuwa na miaka 61, alizikwa kijijini kwake Lituhi, wilayani Nyasa Jumanne Machi 3, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Rais Kikwete ameelezea kutokasirishwa na utendaji wa vyombo vya habari katika uibuaji wa ubadhirifu serikalini, ikiwemo katika sakata la kampuni ya ufuaji umeme wa Richmond na utoaji wa fedha katika iliyokuwa akaunti ya Tegeta Escrow, katika Benki Kuu (BoT).
Akijibu swali la Mhando kuhusu Serikali kuonekana kukasirishwa na vyombo vya habari kuibua maovu, Rais Kikwete alisema hilo hana shida nalo, isipokuwa kunapotokea uchochezi, haitavumilika.
Alitoa mfano wa mauaji ya Kenya na ya kimbari ya Rwanda, ambayo alisema katika matukio hayo yaliyokuwa na athari katika jamii, waandishi wa habari walihusishwa.
Alisisitiza kuwa pamoja na Serikali kulinda uhuru wa habari, lakini ni lazima iwe makini kwa kuwa uhuru huo ukitumika vibaya, una madhara kwa jamii.

No comments: