RAIS KIKWETE AMWAGA CHOZI MAZIKO YA KAPTENI KOMBA


Rais Jakaya Kikwete jana alishindwa kujizuia kutoa machozi, wakati mwili wa Mbunge wa Mbinga Magharibi wilaya ya Nyasa mkoa wa  Ruvuma,  Kapteni John Komba ukishushwa kaburini,  kwenye maziko  yaliyofanyika kijijini  Lituhi.

Kutokana na hali hiyo, ilimlazimu Rais Kikwete kutumia kitambaa chake kujifuta machozi. 
Pia, kutokana na huzuni hiyo, Rais  alishindwa kuzungumza chochote zaidi ya kumiminikwa na machozi.
Rais atamkumbuka Kapteni Komba,  kutokana na kuwa bega kwa bega naye wakati wa kampeni za kugombea urais za mwaka 2005 na 2010 akiwa kiongozi wa kikundi cha burudani cha Tanzania One Theatre (TOT), kinachomilikiwa na CCM.
“Tumepoteza  mtu muhimu, mpiganaji wa kweli ambaye alikuwa akitusaidia kujenga maendeleo ya jimbo letu, tutampata wapi mtu kama huyu? “.
Hiyo ilikuwa ni  moja ya kauli za wananchi wa jimbo hilo, ambao walishindwa kujizuia baada ya mwili wa mbunge wao huyo kushushwa kaburini. Mwili wake ulishushwa kaburini na askari.
Simanzi na majonzi vilianzia katika viwanja vya shule ya msingi Lituhi,  eneo ambalo liliandaliwa kwa ajili ya kutoa heshima za mwisho, ambako wananchi walijitokeza kwa wingi katika huduma iliyoongozwa na  Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, John Ndimbo.
 Akiendesha ibada hiyo ya mazishi,  Askofu Ndimbo  aliwataka waumini kuacha matendo ya kumpuuza mwenyezi Mungu, badala yake watende mema katika maisha yao, kwani hakuna binadamu aliyefunga mkataba na Mungu juu ya kuishi hapa duniani.
“Miili yetu ni hekalu la Bwana na maskani yetu hapa duniani ni ya mpito, inatupasa kufanya kila jitihada kwa mambo ambayo yanampendeza Mungu, hakuna binadamu asiyekuwa na utashi juu ya kifo”, alisema Ndimbo.
Aliongeza kuwa Mwenyezi Mungu anao uwezo wa kumchukua mtu ambaye binadamu walimtegemea kwa namna moja au nyingine hapa duniani. Aliwataka waumini kutenda mema, kwa yale yote yaliyofanywa na aliyekuwa  mbunge wao.
Akielezea wasifu wa Kapteni Komba, alisema kuwa alikuwa ni mtu ambaye  alikuwa tegemeo kubwa kwa Wana -Nyasa kupitia huduma zake alizokuwa akizitoa kwa jamii katika nyanja za kimaendeleo hasa kwa kuijenga wilaya hiyo ambayo ni changa.
Umati mkubwa wa watu kutoka ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma, walihudhuria mazishi hayo wakiwemo viongozi wa CCM na serikali, ambao walifurika kijijini Lituhi kwa lengo la kumsindikiza.
Viongozi na wananchi walipata fursa ya kuuaga na kutoa heshima zao za mwisho kwa mpendwa wao huyo.
Katibu Mkuu wa CCM,  Abdulharman Kinana alisema tumempoteza kiongozi ambaye ana upendo na  mchapa kazi ambaye alikuwa mstari wa mbele kusaidia watu wake.
“Alhamisi iliyopita alikuja ofisini kwangu, tukazungumza akaniambia anataka kupeleka bati jimboni kwake bahati mbaya kafariki, tumepata pigo kubwa ndani ya Chama, daima tutamkumbuka kwa upendo uvumilivu na mchango wake mkubwa katika chama”, alisema Kinana.
Akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya wabunge wa mkoa wa Ruvuma, Mbunge wa Mbinga Mashariki,  alisema wameshitushwa na msiba huo mzito na kamwe hawatamsahau Kapteni Komba, kwani alikuwa kiongozi jasiri, mkweli na mpenda wapiga kura wake.
Akitoa salamu za vyama vya upinzani,  Mbunge wa Lindi Mjini,  Salum Baruani (CUF) alisema wamepokea kifo hicho kwa masikitiko makubwa, kwani alikuwa akimfariji kuwa ipo siku tatizo la mauaji ya albino litakwisha, wataendelea kuwa salama,  ambapo hata yeye wakati akiwa Dar es Salaam alikuwa akimhakikishia ulinzi kuwa yupo salama.
“Ndugu zangu wananchi Komba alikuwa kipenzi cha watu, na hakika ni kiongozi mpenda watu, kambi ya upinzani inasikitika sana kumpoteza kiongozi huyu mahiri na shupavu”, alisema Baruan.
 Spika wa Bunge la Tanzania, Anne Makinda alisema Taifa limempoteza mbunge mpenda wanyonge na aliwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kujiandaa kwa kusali. Pia, aliwataka waache tabia ya kuona mtu aliyekufa amekosa, bali wajenge tabia ya kupendana.
Kapteni Komba alifariki dunia Februari 28 mwaka huu majira ya jioni katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam, wakati akiendelea na matibabu.

No comments: