POLISI WAWAKAMATA WAPIGA RAMLI 225


Jeshi la Polisi nchini limesema limewakamata wapiga ramli  225 katika Mikoa ya Tabora, Geita, Mwanza, Simiyu, Shinyanga Katavi, Rukwa na Kagera.

Kati ya hao, 97 tayari wamefikishwa mahakamani kwa makosa mbalimbali, ikiwamo kukutwa na vifaa vya uganga ambavyo vingine ni nyara za serikali kama vile ngozi ya ngedere, meno ya ngiri, mikia ya tumbili na miguu ya ndege.
Vingine ni  mikia ya nyumbu, ngozi ya simba, ngozi ya fisi, ngozi ya digidigi na wengine walishitakiwa kwa kufanya uganga bila ya kibali.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba (pichani) alitoa taarifa hiyo Dar es Salaam kwa vyombo vya habari kuhusu operesheni ya kupambana na matukio ya mauaji ya albino.
Bulimba alisema watuhumiwa hao walikamatwa katika operesheni kubwa ya kukamata mtandao mzima unaojihusisha na matukio hayo  iliyofanyika katika mikoa yote nchini.
Alisema kuwa tatizo kubwa linalochangia uhalifu huo ni imani mbaya za kuamini ushirikina.
''Wananchi wetu bado wanaamini ushirikina unaosababisha uhalifu huu na ule wa mauaji ya vikongwe unaoendelea nchini,'' alisema Bulimba.
Pia alisema wananchi waache tabia za imani potofu za kishirikina ili kukomesha matukio hayo.
Aliongeza kuwa wananchi wawe wanatoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na wale wanaoeneza imani potofu za kishirikina.
"Jeshi la Polisi linazidi kutoa mwito kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, asasi za kiraia, wazee wa kimila na wananchi kwa ujumla kuendelea kuelimisha jamii kuachana na imani za kishirikina kwani zinarudisha nyuma maendeleo," alisisitiza Bulimba.

No comments: