Siri ya mafanikio ya Padri feki, Josephat
Asenga, aliyekamatwa mkoani Morogoro, katika kuongoza Misa ya Kanisa Katoliki
kwa kufuata taratibu zote maalumu bila kutiliwa shaka, imebainika.
Asenga aliyetumia vitambulisho feki,
alipojitambulisha kwa uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu Maria
Madeko mkoani Morogoro, alipopewa fursa ya kuongoza Misa, alitekeleza wajibu
huo wa kipadri bila kuacha shaka.
Akizungumza na mwandishi, kiongozi mmoja
wa Kanisa Katoliki (jina limehifadhiwa), alithibitisha kuwa Asenga alipofika Parokiani hapo kati ya
Mei na Juni mwaka jana, hakutiliwa shaka hata kidogo kuwa si Padri.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, Asenga
alifika kanisani hapo akiwa amevaa mavazi ya kipadri na kujitambulisha kuwa
yupo nchini kwa mapumziko, akitokea nchini Marekani, alikodai ndipo anakofanyia
shughuli zake za upadri katika Jimbo Kuu la New York.
Mbali na kuvalia mavazi ya kipadri,
Asenga pia alionesha kitambulisho na kusababisha uongozi uamini kuwa ni Padri
na kumpa makaribisho ya Padri mwenzao.
“Alipoonesha kitambulisho tulimwamini na
jinsi alivyokuja na mavazi ya upadri na muonekano wake alionao, haikuwa rahisi
kumtilia shaka,” alisema kiongozi huyo.
Baada ya kupata makaribisho ya kipadri,
Asenga kwa mujibu wa kiongozi huyo, aliomba apangiwe zamu ya kuongoza misa ya
Jumapili iliyofuata na kukubaliwa.
Kiongozi huyo alithibitisha kuwa Asenga
aliongoza vyema misa hiyo, kwa kufuata taratibu zote za kanisa hilo kama
zinavyofuatwa na mapadri wengine.
Kwa kawaida Misa katika Kanisa la
Katoliki, huanzia Sakestia, sehemu
ambayo mapadri na waministranti, ambao ni wasaidizi wao, huvaa majoho na kusali
kabla ya kuingia kanisani wakisindikizwa na nyimbo.
Baada ya kuingia madhabahuni, Padri
hubusu madhabahu kabla ya kualika waumini katika Misa.
Mualiko huo hufuatiwa na maelezo kidogo
na kuanza Ibada ya Kitubio, ambayo waumini hutubu dhambi zao na kujiweka tayari
kusikiliza neno la Mungu.
Ibada ya kusomwa neno, kwa kawaida masomo
matatu kutoka vitabu vya Agano la Kale na Jipya katika kitabu cha Bibilia
Takatifu, Padri huanza kutoa mahubiri.
Mahubiri yakiisha, Misa huendelea kwa
sadaka na baadaye, Padri huongoza waumini kuanza kukumbuka maelezo ya siku
ambayo Yesu Kristo alitoa Sakramenti katika Chakula cha Mwisho kwa wanafunzi
wake akitaka wamkumbuke.
Kwa kawaida, eneo hilo ndipo Padri kwa
mamlaka aliyopewa, hufanya mageuzi ya sakramenti kuwa Hostia Takatifu, kwa
maneno mengine hubariki mkate kuwa Mwili wa Kristo na divai kuwa Damu ya
Kristo.
Kwa Wakatoliki, eneo la mageuzi ni eneo
muhimu na ndio waumini hutuma maombi kimya kimya, wakiamini ndio Kristo
anashuka mwenyewe.
Baada ya kutumikia Kanisa na kukubalika,
Asenga aliaga kuwa anarudi nchini Marekani kwa kuwa muda wake wa mapumziko,
umekwisha na kuagwa na Kanisa.
Wakati uongozi wa Kanisa Katoliki, Parokia ya Mtakatifu
Maria Madeko, ukiwa na imani kuwa Asenga ni Padri na amerejea New York,
kuendelea na Utume, walipata taarifa za kushangaza kutoka kwa baadhi ya
waumini, wakidai wamekutana na Asenga mitaani.
Mbali na taarifa hiyo ya kukutwa mitaani
na waumini wake, taarifa zaidi zilieleza kuwa amekuwa akiishi na mwanamke
katika eneo la Ujenzi, kinyume na desturi za mapadri wa Kanisa Katoliki
duniani, ambao hawaruhusiwi kuoa.
Baada ya taarifa hizo, kwa mujibu wa
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Leonard Paulo, Asenga aliwekewa mtego
na Paroko wa Parokia hiyo ya Mtakatifu
Maria Madeko, Malt Dyfrig Joseph.
Paroko huyo inadaiwa aliwaomba waumini
wamshawishi Asenga afike parokiani hapo na baada ya kufika, alihojiwa na Paroko
huyo na kudai kuwa alipata upadirisho katika Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, baada
ya Paroko huyo kupata maelezo hayo, alifanya mawasiliano na Katibu wa
Jimbo hilo la Dar es Salaam na kujibiwa kuwa hakuna jina la Padri huyo.
Mtego wa pili kwa mujibu wa Kamanda
Paulo, ulifuata kwa Paroko huyo kutoa taarifa Polisi kuhusu uwepo wa Padri
feki, ambaye aliaminiwa kwa kiwango cha kuruhusiwa kuongoza Misa.
Taarifa hizo zinasema Alhamisi ya wiki
hii, saa 10:30 jioni, Asenga alimpigia simu Paroko huyo na kuomba ampangie kazi
ya kuendesha Misa Jumapili ya leo parokiani hapo, na kukubaliwa ambapo Paroko
huyo alimtaka afike kanisani.
Baada ya kufika, taratibu za kujulisha
Polisi zilifanywa na askari walipofika kanisani hapo, walimkamata mtuhumiwa
huyo.
Kwa mujibu wa Kamanda Paulo, baada ya
kufanya mahojiano na Asenga, alikiri kuwa yeye si Padri na walipokwenda nyumbani kwake kufanya upekuzi,
walimkuta akiwa na majoho saba ya upadri.
Taarifa zaidi zilizofikia gazeti hili jana,
zilibainisha kuwa Asenga huenda kwa kutumia mbinu hizo hizo, alishaaminiwa
kuongoza Misa katika mkoa wa Kilimanjaro katika maeneo ya Uru na Moshi na
mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment