Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto
Kabwe amewaaga rasmi wananchi wa jimbo hilo huku akiwataka wananchi hao
kutosononeka kwa uamuzi wake wa kutoendelea kugombea ubunge wa jimbo hilo, bali
wamwombee na kumuunga mkono katika kila uamuzi atakaouchukua.
Zitto aliwaaga wananchi hao kupitia
mkutano wa hadhara mjini Kigoma uliorushwa moja kwa moja na Kituo cha Radio cha
Clouds, ambapo alisema, kipindi cha miaka 10 kinatosha kwa yeye kuwa mbunge wa
jimbo hilo hivyo kwa sasa ni vyema kijiti akapewa mtu mwingine, ili yeye aweze
kusonga mbele katika kuwatumikia Watanzania kwa nafasi kubwa zaidi.
Hatuwezi kuanika kusudio lake la
kuwatumikia Watanzania katika nafasi kubwa zaidi, ingawa alidokeza anaweza kuzungumza
jambo wakati wowote wiki ijayo.
Alisema amezungumza na wazee wa mkoa
huo pamoja na viongozi wa vijiji 45 ambao wamempa baraka juu ya uamuzi wake huo
aliochukua, huku akiwataka wananchi hao kukubaliana na baraka hizo alizopewa na
wazee.
"Nawaomba kwa sasa mniruhusu
nikafanye mambo mengine ili nipishe mtu mwingine ashike hiki kijiti ili
tukimbizane, sina maana sitaendelea kukemea mabaya, nitaendelea kukemea, lakini
kwa njia nyingine," alisema Zitto.
Alisema hata baada ya uchaguzi mkuu
wa Oktoba, mwaka huu ataendelea kukemea mambo mbalimbali ambayo ataona
yanalipeleka taifa pabaya, kwa kuwa anapenda kuona Tanzania inasonga mbele.
"Mimi bado Mbunge wenu na
nitaendelea hadi hapo watakaposema basi inatosha, ninachowaomba msisononeke,
kwani hakuna kiongozi mahiri wa kisiasa asiyepitia kwenye misukosuko.
“Na hata dhahabu haiwezi kuwa dhahabu
kama haijapitia kwenye moto,…ninazidi kuimarika kisiasa, hivyo ninayopitia ni
ya kawaida kwa mtu anayeelekea kwenye mafanikio," alisema Zitto aliyetumia
nafasi hiyo kuwashukuru wanaKigoma kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuwatumikia
tangu mwaka 2005 alipokuwa na umri wa miaka 29.
Alisema kwa kipindi chote cha ubunge
wake, licha ya kupitia katika milima na mabonde ya kisiasa, anajivunia mambo
mbalimbali aliyoyafanya ya kulisaidia taifa ikiwemo kupambana na ufisadi, kwa
kuibukia kashfa mbalimbali kupitia Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC)
anayoiongoza.
Aliwataka wananchi hao kujivunia kuwa
na mbunge kama yeye kwa kuwa kwa kipindi chote amekuwa akiwasilisha hoja zenye
manufaa kwa taifa, kwani kuna wabunge wengine
tangu wachaguliwe kwa kipindi cha miaka mitano hawajawahi kuleta hoja
yoyote.
Aidha, wiki iliyopita Zitto alivuliwa
uanachama wa Chadema baada ya Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam kutupilia
mbali kesi ya madai aliyofungua dhidi ya chama chake, ambapo kwa mujibu wa
katiba ya chama hicho, mwanachama atakayekishtaki chama atakuwa amejivua
uanachama mwenyewe.
Mwanasheria wa chama hicho Tundu
Lissu alipozungumza na waandishi wa habari alisema, uanachama wa Zitto
ulimalizika rasmi baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali zuio la kutaka Kamati
Kuu kutojadili uanachama wake.
Zitto ambaye alikuwa Naibu Katibu
Mkuu wa chama hicho, alifungua kesi hiyo dhidi ya Bodi ya Wadhamini ya Chadema
na Katibu Mkuu wake, akiiomba Mahakama ikizuie chama kujadili uanachama wake,
hadi rufaa anayokusudia kuikata Baraza Kuu la chama kupinga kuvuliwa nyadhifa,
itakaposikilizwa.
Hata hivyo, Zitto amekuwa akisema
yeye bado ni mbunge halali na mwanachama halali wa chama hicho.
No comments:
Post a Comment