Kazi anayofanya Katibu Mkuu wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana katika ziara zake mikoani, sasa ni dhahiri
ameanza kurejesha chama hicho katika misingi ya asili yake ya Ujamaa,
iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Hilo limejidhihirisha katika kauli na
hotuba zake kwa wanachama na wananchi, kwenda kinyume na taswira iliyoanza
kujijengea mizizi, kuwa chama hicho kimeanza kuondoka katika misingi ya Ujamaa,
iliyojengwa tangu kuasisiwa kwake.
Katika moja ya kauli zake alizotoa jana
alipohutubia wakazi wa Mkoka katika wilaya ya Kongwa, akiwa katika ziara ya
kutembelea mkoa wa Dodoma, Kinana alisisitiza umuhimu wa uadilifu wa wagombea
kwa mtindo uliokuwa ukisisitizwa wakati wa Mwalimu Nyerere.
Kwa mujibu wa Kinana, sifa namba moja
inayozingatiwa na wananchi katika kumpata kiongozi wa kuwaongoza, hata kama ni
mchapakazi wa kiwango cha juu, uadilifu utasimama kuwa sifa namba moja.
Alisema kutokana na kumomonyoka kwa
maadili ya uongozi, tofauti na enzi za utawala wa Mwalimu Nyerere, wananchi
sasa hawazingatii suala la uhodari na uchapakazi kama sifa namba moja ya kumchagua
mtu kuwa kiongozi wao.
"Wananchi sasa wanaangalia nani
muadilifu, nani sio mwizi, nani si mlaji, wapo tayari kukusamehe mambo mengine
yote, lakini si suala la uadilifu," alisema Kinana.
Alisema kutokana na kutambua hilo, CCM
itakuwa makini na viongozi wake watakuwa wakali, katika kuhakikisha kuwa watu
wasio waadilifu wanadhibitiwa wasishike nafasi za uongozi kupitia chama hicho,
ili kujenga heshima na imani ya wananchi kwa chama hicho.
Kinana aliweka wazi kuwa moja ya ishara
ya kutetereka kwa uadilifu katika
utumishi wa umma, ni tabia iliyoibuka siku za hivi karibuni, ambapo viongozi
wanaokiuka misingi ya maadili ya uongozi wa umma, wanapoombwa kukaa kando
kutokana na makosa waliyofanya, wanagoma kuondoka madarakani jambo ambalo
halikuwepo zamani.
"Siku hizi ukimwambia mtu kaa kando,
anakataa au anakwenda kukusanya watu wa kumtetea na kumpigania, watu wanafanya
maandamano ya kwenda kutetea watu wasio na maadili ya utumishi wa umma. CCM
kuweni wakali katika hili msikubali hata kidogo," alisema Kinana.
Katibu Mkuu huyo pia alielezea kukerwa na
hatua ya hivi sasa ya mawaziri, kuandaa sherehe na kuchinja ng'ombe na mbuzi,
pale wanapochaguliwa kushika nyadhifa hizo, akisema kitendo hicho kinaonesha
mawaziri wa aina hiyo hawatambui uzito wa dhamana wanayopewa.
Amekerwa pia na hatua ya mawaziri hao
kutotembelea wananchi vijijini na badala yake wamekuwa wakilundikana kwenye ndege
kwenda katika mataifa mbalimbali duniani, kitendo kinachofanya baadhi ya miradi
inayotekelezwa chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM, kutokamilika kwa wakati.
"Unateuliwa Waziri unafanya sherehe?
Unachinja ng'ombe, unachinja mbuzi na unakunywa bia, badala ya kwenda Msikitini
au Kanisani kumwomba Mungu akusaidie!" Alihoji.
Alisema viongozi wa aina hiyo wanafanya
hivyo bila kufahamu kuwa uelewa wa wananchi wa siku hizi ni mkubwa na
wanatambua kila tabia na uwezo wa viongozi wa Serikali.
"Uzuri ni kwamba wananchi wa siku
hizi wanatujua, wanajua nani mwongo, wanajua nani anapiga porojo, wanajua nani
anajali tumbo lake na wanajua nani mchapakazi kwa hiyo watatuhukumu kwa kile
tunachofanya," alisema Kinana.
Juzi Kinana aliunganisha tabia ya
ubadhirifu serikalini na uchu wa kupata mali za haraka, pale alipokuwa akikemea
matumizi mabaya ya dhana ya utawala bora, ambayo imeonekana kutumika vibaya
kutetea wezi.
Alionya wanachama wa CCM kwamba
wakilindana na ‘Iyena Iyena’ zao, hawatafika mbali, na kuwataka wawe wakali
kwani wanaCCM wengi ni masikini na wachache kama 100 au 20 hivi ndio
matajiri.
Alikumbusha kuwa wanaoiba ndani ya
Serikali, wengi wao ni matajiri, ambao ni wachache wanaoishi maisha ya
mbinguni, lakini adhabu wanapata masikini wengi wanaoishi duniani na hilo halikubaliki.
"WanaCCM jumla yetu tupo milioni
saba, lakini hawa wezi wapo kama 100 au 20, tusiyumbishwe na watu hawa
wachache, mimi ni Katibu Mkuu wa Chama cha wakulima
masikini na wafanyakazi masikini,
sitakubali kuona chama changu kinageuzwa dampo la walanguzi," alionya
Katibu Mkuu huyo wa CCM.
Akizungumza kuhusu adhabu kwa watuhumiwa
wa wizi, Kinana alielezea kukerwa na dhana ya utawala bora, ambayo alisema
imekuwa ikitumiwa kama kivuli cha kulinda wezi wa mali ya umma, kwa maelezo
kuwa ni ngumu kuwafukuza madarakani au kuwaadabisha bila kufuata sheria.
"Yapo mambo yamewaudhi Watanzania
wengi. Kwanza ni suala la wizi serikalini. Eti mtu kaiba halafu sisi tunaanza
kupiga maneno mara ooh kaiba au hajaiba? Aondoke, asiondoke?
“Tumwadhibu tusimwadhibu? Ukweli ni
kwamba mtu akituhumiwa, tuhuma peke yake inatosha kumfanya aondoke na kama
hataki, basi tumuondoe kwa nguvu na si kuleta maneno,” alisema na kuongeza kuwa
enzi za Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, dhana hiyo haikupewa nafasi kwa wezi.
"Lazima niseme wazi, Watanzania
wametushangaa sana katika hili, mwingine akiiba kuku si sawa… wakubwa
serikalini wanasema afungwe, lakini huyu aliyeiba fedha nyingi za umma,
tunasema utawala bora!
“Lazima tulikatae hili kwa nguvu zote na
mtu wa kwanza anayepaswa kukasirika ni mwanaCCM, kuweni
wakali acheni kabisa kulindana," alisema Kinana.
Akionesha wazi kukerwa na hali hiyo,
Kinana alisema kinachosikitisha zaidi ni kuona mtendaji ndani ya Serikali
anapoiba, wanajitokeza wanaCCM wengine ili kumkingia kifua asichukuliwe hatua,
jambo ambalo limekuwa likiwakera Watanzania wengi.
"Mtu ameiba wazi kabisa, wanatokea
wanaCCM wenzake utasikia oooh hakujua, ooh tumuonee huruma. Jamani huyu mtu
hakujua kwani hana macho kuona anachokifanya ni wizi?
“Naomba wanaCCM simamieni uadilifu,
mmechaguliwa na wananchi kutokana na imani yao kwenu na kama tunavyofahamu
imani huzaa imani, nataka niahidi CCM tutakuwa wakali sana, ukiiba lazima
uondoke.
"Huu utawala bora ni lazima sasa
tuutazame kwa macho mawili maana ni kama umeegemea upande mmoja. Mtu anaiba
kuku hakuna utawala bora, lakini anaiba mali ya umma, unaambiwa kuna utawala
bora! Mwizi dawa yake ni jela si maneno, lazima tujenge utamaduni wa
kuwajibishana.
"Lazima tuige wakati wa utawala wa
Baba wa Taifa, yeye alisema ukikosea iwe ni sawa na kugusa moto, ukigusa moto
adhabu ni palepale, ilikuwa ukibainika tu unastaafishwa kwa manufaa ya umma,
lakini sasa unaambiwa utawala bora. Mtu akiiba anahamishwa,” alionya.
No comments:
Post a Comment