Uongozi
wa Azam FC umesema umemalizana na makocha wake Joseph Omog (pichani) na Ibrahim Shikanda
na wako huru kuondoka muda wowote kwani hawana wanachodai.
Akizungumza na mwandishi, Meneja wa Azam FC,
Jemedari Said alisema kwa kawaida wakisitisha mkataba na kocha ama mchezaji
humlipa stahiki zake zote.
“Sisi si kama klabu nyingine tunajua majukumu
yetu tukimalizana na mtu tunamlipa haki zake zote kisha anaondoka, sasa makocha
hawa tumeshawalipa kila kitu ni wao tu wana uamuzi wa kuendelea kubaki nchini
ama kuondoka, wako huru hawatudai hatuwadai,” alisema Saidi.
Uongozi wa Azam FC juzi uliwatimua makocha hao
kwa kile inachodaiwa ni kuishiwa mbinu za ufundishaji hali inayosababisha timu
hiyo kuyumba kwenye michuano mbalimbali.
Azam FC imetupwa nje ya michuano ya Ligi ya
Mabingwa kwa jumla ya mabao 3-2 na El Merreikh ya Sudan.
Awali, timu hiyo ilikuwa kwenye nafasi nzuri ya
kufuzu baada ya kushinda mabao 2-0 katika mechi ya kwanza iliyofanyika kwenye
Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, lakini ilifungwa mabao 3-0 katika marudiano
Khartoum.
Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo
wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 27, ipo chini ya Kocha Msaidizi George Nsimbe mpaka
itakapopata kocha mwingine.
Omog, ambaye ni raia wa Cameroon, alianza kazi
Desemba 2013 akichukua mikoba ya Stewart Hall kutoka Uingereza, ameiongoza Azam FC katika mechi 55 kwenye
michuano yote, akishinda 30, sare mara 14 na kupoteza mechi 11.
No comments:
Post a Comment