SERIKALI YASITISHA TIKETI ZA KIELEKTRONIKI UWANJA WA TAIFA

Serikali imesitisha matumizi ya tiketi za elektroniki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi kasoro zilizopo katika matumizi ya tiketi hizo zitakapoondolewa.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa vyombo vya habari, uamuzi huo ulitangazwa Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia mbele ya viongozi wa shirikisho hilo na Benki ya CRDB, ambao ndio wanaoendesha mfumo huo.
Taarifa hiyo ya TFF haikutoa maelezo zaidi, lakini katika siku za karibuni, kumekuwa na malalamiko kuhusu matumizi ya mfumo huo katika viwanja mbalimbali nchini ukiwamo uwanja mkuu wa Taifa.
Mfumo huo ulianza kutumika katika msimu wa 2013/2014 na ulisababisha malalamiko kutoka kwa wadau mbalimbali, wakiwamo mashabiki wa soka ambao si tu walilalamikia usumbufu kuingia uwanjani, lakini hata upatikanaji wa tiketi hizo kwa maana ya ununuzi wake katika maeneo mbalimbali kupitia mtandao wa kielektroniki.
Hivi karibuni, katika mkutano uliopita wa Bunge, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii iliitaka serikali kuangalia upya mfumo mzima wa ukataji wa tiketi hizo kwenye Uwanja wa Taifa.
Iliitaka serikali kuitisha kikao cha wadau wote yaani Benki ya CRDB, TFF, wamiliki wa viwanja, klabu ili kuupitia upya mkataba na kuangalia mfumo mzima wa uendeshaji.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM) akitoa taarifa ya utekelezaji wa kamati hiyo bungeni mapema mwezi uliopita, alisema kamati hiyo ilifanya ziara kwenye uwanja huo Januari 19, mwaka huu na kukagua jinsi mashine za kielektroniki kwenye uwanja huo zinavyofanya kazi.
Alisema wajumbe walijionea jinsi watazamaji wa mpira wa miguu wanavyoingia kwa njia ya kawaida tofauti na maelezo kuwa wanatumia mfumo wa kielektroniki.
“Aidha, mfumo huu umethibitika kuwa hautumiki na kamati haijaridhishwa na utaratibu wa ukataji wa tiketi unaotumika sasa na tunaitaka serikali kuitisha kikao cha wadau ili kupitia upya mkataba huo,” alisema Mtanda.
Alisema kutokana na kamati kutoridhishwa ni vyema kuangalia mfumo huo ili kuongeza mapato kwani bado kuna wanaonunua tiketi hizo kwenye magari na sehemu nyingine.

No comments: