WATANZANIA WAHIMIZWA KULA MAYAI YA KWALE

Watanzania wamehimizwa kutumia mayai ya ndege aina ya kwale na nyama yake kwa kuwa ni chakula bora chenye virutubisho mbalimbali.

Ushauri huo ulitolewa na mfugaji wa kwale ambaye ni mkazi wa Tegeta, Dar es Salaam, Susan Magibo alipokuwa akizungumza na mwandishi.
Magibo alisema ndege hao hivi sasa ni gumzo hapa nchini, kwani inasadikiwa kuwa ni dawa ya magonjwa mbalimbali kama pumu, shinikizo la damu, kisukari na mengineyo.
Vile vile, alisema pia wanaongeza kipato kwa kasi kwa kuwa watu wameanza kuelewa umuhimu wa ndege hao, hivyo kulingana na umri wao huuzwa kuanzia Sh 3,000 hadi 30,000 kwa ndege mmoja.
“Mayai ya ndege hawa ni mazuri sana yakiliwa hasa yakiwa mabichi. Yana virutubisho vingi sana, hivyo yakipikwa vinapungua.
“Kwenye mayai hayo kuna madini ya zink, Omega 3 ambayo yanapatikana kwenye mafuta ya samaki, vitamin B Complex, vitamin A na D na virutubisho vingi mbalimbali,” alisema Magibo.
Aliongeza kuwa mayai hayo, pia ni aina ya chakula chenye alkaline, ambayo ni kinga tosha ya tatizo la kansa.
“Chembechembe za kansa haziwezi kukua kwenye alkaline, hivyo ni vyema watu wote watambue umuhimu wa mayai ya ndege hawa,” alisema mfugaji huyo.
Alisema mtandao wa http://www.quailfarm.co.uk, unaonesha jinsi ya utumiaji wa mayai hayo ili kupata matokeo mazuri kiafya.
Alisema mtandao huo unaonesha kuwa mayai hao, yakitumiwa kama dawa siku ya kwanza na ya pili mtumiaji anapaswa kula mayai matatu, siku ya tatu mayai manne, na siku ya tano mayai matano.
Aliiomba wizara husika ya mifugo na uvuvi, kushirikiana na wafugaji hao ili kutoa elimu kwa Watanzania waweze kutambua umuhimu wa ndege hao, tofauti na inavyotafsiriwa kuwa ni ndege wa porini.

No comments: