HOTELI ZAFUNGWA ARUSHA KWA KUKOSA WATALII

Baadhi ya hoteli za kitalii mjini Arusha zimefungwa, huku mishahara ya wafanyakazi ikipunguzwa kwa asilimia 25, kutokana na kukosa watalii.

Akizungumza wakati wa tafrija ya kuukaribisha mwaka mpya 2015, zilizoandaliwa na Chama  cha Mawakala wa Watalii Nchini (TATO), Mwenyekiti wa chama hicho, Willy Chambulo alisema hali ya biashara kwa miezi hii mbaya na kusababisha kufungwa kwa  baadhi ya hoteli.
Alisema: “Mimi mwenyewe hoteli zangu sita nimezifunga na baadhi ya wenzangu pia wanatarajia kufunga hoteli zao kwa sababu ya kukosa watalii.”
Pia alitoa ombi kwa serikali wakati huu wa ukosefu wa wageni ni vyema wakapunguziwa  nusu ya bei kwa viingilio na kodi za serikali wanazotoza kwa kuingia nchini na hifadhini.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alikubaliana na ombi hilo huku akisema: “Kutokana na hili, sisi Tanzania tumelisikia hili tatizo, hivyo hatutaongeza bei yoyote na ndiyo sababu Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) pia hatujaibebesha sekta ya utalii, ili kuwapunguzia mzigo.”
Nyalandu alisema Serikali pia haitaongeza tozo yoyote ya kuingilia hifadhi za taifa hasa katika kipindi hiki cha upungufu wa wageni.
Alisema kila mwaka Tanzania imekuwa ikipokea watalii 250,000 wanaopitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta nchini Kenya, hivyo tishio la ugaidi kwa nchi hiyo, kumeleta shida pia kwa kupunguza watalii nchini.
Naye Mkurugenzi wa Kampuni ya kitalii nchini ya Leopard, Zuhel Fazal alisema kwa kampuni yao wamepunguza mishahara kwa asilimia 25.
Kwa ujumla biashara ya utalii imepungua kwa asilimia 45 na ili kukabiliana na hali hiyo, wamepunguza marupurupu mengine kwa wafanyakazi kama vile kuwalipia wafanyakazi kodi za nyumba wameziondoa hadi hali itakaporudi tena.

No comments: