WASHITAKIWA WA KESI YA MAUAJI YA MVUNGI WAOMBA KUSIKILIZWA



Washitakiwa wa kesi ya mauaji ya mjumbe wa Tume ya Taifa ya Mabadiliko ya Katiba, Dk Sengondo Mvungi wameiomba Mahakama iwape haki ya kuwasikiliza.

Waliwasilisha ombi hilo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Waliarwande Lema wakati kesi hiyo ilipotajwa na Wakili wa Serikali, Leonard Challo kudai upelelezi bado haujakamilika.
Mshitakiwa Longishu Losingo alidai wapo jela, lakini wanatakiwa kupata haki zao za msingi kwa sababu wanaona Mahakama inaegemea upande mmoja, hoja zao hazisikilizwi.
Hakimu Lema alisema hawezi kuwasikiliza na alishatoa kibali waende kwa Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo. Aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 23, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Longisho, washitakiwa wengine ni Chibago Magozi (32), John Mayunga (56), Juma Kangungu (29), Paulo Mdonondo (30), Mianda Mlewa (40) , Zacharia Msese (33) Msigwa Matonya (30) na Ahmad Kitabu (30).
Wanadaiwa kuwa Novemba 3, mwaka juzi katika eneo la Msakuzi, Kibwegere wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, walimuua Dk Mvungi kwa kukusudia.

No comments: